ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, July 19, 2014

KAGAME ATOA SIRI YA UGONVI NA KIKWETE


RAIS Paul Kagame wa Rwanda ametoboa siri ya kuyumba kwa uhusiano baina yake na Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania.

Katika miezi ya karibuni, uhusiano baina ya Rwanda na Tanzania umekuwa katika hali ya kulegalega, haswa baada ya Kikwete kutoa ushauri wa kutaka serikali ya Kagame ikutane na waasi wa kundi la FDLR kwa ajili ya kutafuta amani ya kudumu.

Akihojiwa na jarida la African Report, Kagame alisema kilichofanya agombane na Tanzania ni kutokana na kile alichokiita “kuingiliwa katika mambo ya ndani ya taifa lake.”

“Kitu nisichokubaliana nacho ni kuingiliwa. Haikubaliki kwamba Jakaya Kikwete na serikali yake wajihusishe, kwa namna yoyote, na watu waliohusika na mauaji ya kimbari. Sioni sababu yoyote ya mtu kujihusisha nao.

“Jambo moja liko wazi kwangu; Sishauri mtu yeyote aingilie katika mambo yangu ya ndani. Huu ni msimamo wangu na haujalishi ni nchi gani; iwe Afrika Kusini, Tanzania, Ufaransa, au Ubelgiji,” Kagame alinukuliwa na jarida hilo akisema.

Katika mahojiano hayo ambayo yametafsiriwa na kuchapwa katika toleo hili, Kagame alizungumza kwa urefu na uwazi kuhusu mambo ambayo yeye binafsi na serikali yake wamekuwa wakituhumiwa kuyafanya na jamii ya kimataifa.

Baadhi ya masuala aliyoyazungumzia katika mahojiano hayo ni endapo atawania urais katika uchaguzi wa mwaka 2017 nchini humo, demokrasia, tuhuma za mauaji ya wapinzani wake kisiasa kama Patrick Karegeya na maoni yake kuhusu chanzo na athari za mauaji ya kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994.

Rais Kikwete alitoa ushauri kuhusu Kagame kukutana na waasi wa FDLR nchini Ethiopia nje ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika; kauli ambayo haikupokewa vizuri na jirani zao hao. CREADIT:RAIA MWEMA

Soma mahojiano kamili katika hapa.
The Africa Report (AR): Miaka ishirini baada ya mauaji ya kimbari, unadhani dunia sasa imeelewa haswa nini kilitokea au kilisababisha kutokea yaliyotokea?

Paul Kagame (PK): Kwa bahati mbaya, jibu ni hapana. Taswira iliyoko nje ni ile kwamba mauaji ya kimbari ni kama yalianguka tu kutoka angani. Bila ya sababu au madhara. Hakuna anayepaswa kuwajibika na pia kuna hali ya kutaka kuonyesha kwamba tukio lenyewe limekuzwa tu. Kwa kweli inasikitisha sana.

AR: Je, kutokueleweka huku kwa tukio hili kumesababishwa na ukweli kwamba waliohusika ni watu waliokuwa wakiishi katika jamii moja – jambo ambalo ni la kipekee katika dunia ya sasa?

PK: Kweli kabisa. Kilichotokea ni tofauti na kile ambacho kimetokea kwa watu wengine. Hii limesababisha kuwapo kwa matukio mahususi ambayo wakati mwingine ni muhimu kuyaeleza.

Hata kama kuna watu wanataka jambo hili lifanywe kama mwiko kulizungumzia, hatupaswi kusahau namna baadhi ya mataifa ya magharibi yalivyochangia kwa kilichotokea –si kwa sababu za kihistoria pekee lakini kutokana na kile kilichotokea wakati wa mauaji hayo ya kimbari.

Leo, ni mataifa hayahaya ya magharibi ambayo ndiyo yanahubiri kuhusu masuala ya utawala bora na demokrasia.

Wangependa Wanyarwanda waendelee kuishi kana kwamba hakuna kilichotokea; jambo ambalo lina faida kwao kwa vile linamaanisha watu wangesahau kuhusu kuhusika kwao kwenye mauaji hayo.

Chukulia mfano wa Ufaransa. Miaka 20 baada ya mauaji ya kimbari, jambo pekee wanalodai kujutia ni kwamba hawakufanya vya kutosha kuzuia mauaji yale yasiendelee. Japo huo ni ukweli, unaficha ukweli mwingine mkubwa zaidi kuhusu namna Ufaransa na Ubelgiji zilivyoshiriki katika kuandaa mazingira ya mauaji hayo na namna pia Ufaransa ilivyoshiriki kabisa katika mauaji hayo.

AR: Unalaumu hizi nchi kwa kupanga mauaji au kwa kushiriki katika tukio hilo?

PK: Vyote ! Uliza waathirika wa mauaji ya Bisesero Juni mwaka 1994 na watakueleza nini askari wa Jeshi la Ufaransa walifanya kupitia kile kilichoitwa Opération. Kule Bisesero na katika maeneo ya jirani yaliyotengwa kwa ajili ya Utoaji wa Huduma za Kibinadamu, Wafaransa hawakuwa watazamaji tu bali pia walishiriki katika mauaji hayo.

AR: Sababu nyingine ya kufanya ugumu wa kuelewa kuhusu tukio lenyewe ni ukweli kwamba unaonekana kama kiongozi wa taifa ambaye si wa kawaida. Uko tofauti kidogo. Unafahamu hili?

PK: Sifahamu kabisa. Kama kuna tofauti yoyote, itakuwa ni kwa sababu ya uzoefu nilioupata katika maisha yangu na historia ya kipekee ya taifa langu. Lakini, kama mtu anazungumzia kuhusu maendeleo na utawala, taifa langu lina changamoto zilezile zilizopo katika nchi nyingi za Afrika.

AF: Ingawa mafanikio yako katika maeneo ya kijamii na kiuchumi yamekuwa yakipongezwa, rekodi yako kama mwana demokrasia imekuwa finyu. Unazungumziaje kuhusu hili?

PK: Unamaanisha demokrasia ipi? Kama unamaanisha ile ya nchi za Magharibi ambayo wanatulisha inayoelezea kuwa Demokrasia inatokana na watu na kwa ajili ya watu na inayochagiza Uhuru wa Kujieleza, Kutoa Mawazo na Kuchagua. Cha ajabu, wakati watu wa Rwanda wanapoamua kutumia uhuru wao wa kuchagua; utasikia watu haohao wa magharibi wakilalama; ‘Hapana, mmekosea. Maamuzi yenu si mazuri kwenu.’

Kilicho wazi ni kwamba wenzetu wanataka ufuate aina ya demokrasia wanayoitaka wao na si demokrasia ya kweli. Kuna nchi nyingine za Afrika ambazo zimejaa ukabila, rushwa, wizi na kila aina ya uovu lakini hazisemwi kwa sababu zimeamua kufuata mambo fulani ambayo yanapendwa na mabwana wakubwa.

Hivyo, kama maana ya demokrasia ni kufuata tu maelekezo wanayotaka mabwana wakubwa, basi mimi mtazamo wangu ni tofauti kuhusu demokrasia.

AR: Muda wako wa kuwa madarakani unamalizika mwaka 2017 na Katiba ya Rwanda inakukataza kuwania tena nafasi hiyo. Msimamo wako ukoje kwenye hilo?

PK: Mara zote nimekuwa nikisema nitaiheshimu Katiba. Hata hivyo, napenda kusema kuwa Katiba ni maelezo kuhusu matamanio ya wanancho katika wakati fulani na kwenye muktadha husika.

Duniani kote, iwe katika nchi ambazo demokrasia imekomaa na katika nchi change, sheria za msingi zimekuwa zikibadilishwa, kufanyiwa mapitio na kurekebishwa kutokana na maslahi ya wananchi.

AR: Vipi kuhusu ukomo wa kubaki madarakani.

PK: Kuhusu hilo, kama ilivyo kwenye mengine, sina jibu la moja kwa moja. Sina uamuzi kuhusu hili na mimi si mwandishi wa Katiba. Kwanini watu wamening’ang’ania sana kuhusu jambo hili? Jambo la msingi unalotakiwa kuliweka akilini ni kwamba mimi ninaheshimu Katiba na nitaendelea kuwa hivyo.

AR: Inaonekana hakuna hata Mnyarwanda mmoja anayeamini kwamba utaachia madaraka mwaka 2017?

PK: Unatakiwa kujiuliza je ni kwa sababu wanadhani kwamba ninataka kubaki madarakani au kwa wanataka niendelee kubaki madarakani? Hili ni swali ambalo unatakiwa kuwauliza wananchi. Jambo moja ni lamuhimu sana kulielewa kuhusu mimi; Kama wananchi watawasilisha kwangu mapendekezo yao kuhusu mojawapo ya hilo, ni wazi iitabidi nifanye maamuzi.

AR: Kuna ugumu kidogo kujenga picha yako ukiwa na umri wa miaka 60 na umestaafu ukitazama ng’ombe wako katika ranchi yako iliyopo pembezoni ya Ziwa Muhazi.

PK: Kwanini isiwe hivyo? Mimi naiona hiyo picha. Hilo ni jambo linalowezekana kabisa.

AR: Tangu mauaji ya mwanasiasa wa upinzani, Patrick Karegeya na shambulizi dhidi ya Jenerali Kayumba Nyamwasa nyumbani kwake nchini Afrika Kusini, uhusiano baina ya Rwanda na Afrika Kusini umezorota. Mlikutana na Rais Jacob Zuma mjini Luanda, Angola Machi 25 mwaka huu, mlizungumza nini siku hiyo?

PK: Mazungumzo yetu hayakuzama kwenye mambo hayo ingawa tuligusia kidogo jambo hilo. Msimamo wangu kwenye suala hilo uko wazi; kwamba kupata hifadhi ya kisiasa kwenye nchi ya nje kunamaanisha wajibu wa kukaa kimya na kuacha vitendo vya kichochezi dhidi ya nchi yako.

Hivyo, kimsingi, mimi sina tatizo na watu kupata hifadhi ya kisasa. Tatizo langu liko kwenye uhuru na wakati mwingine msaada wa ngazi za juu ambao watu kama akina Nyamwasa walioko Afrika Kusini wanaupata ili waweze kuhatarisha hali ya Rwanda na kuchochea ugaidi.

AR: Uliomba serikali ya Afrika Kusini iwarejeshe Rwanda Karegeya na Nyamwasa?

PK: Hakika tulifanya hivyo na taarifa za kumbukumbu kuthibitisha hilo tunazo. Watu hawa waliwahi kushitakiwa wakiwa nchini Rwanda na kukutwa na makosa na kuhukumiwa wakiwa hapa.

AR: Lakini Afrika Kusini haina imani na mfumo wenu wa sheria ….

PK: Huo ni upotofu. Afrika Kusini inatakiwa kuwa makini ili isitoe picha kwamba inaelemea upande mmoja katika suala hili. Nina matumaini makubwa kwamba baada ya muda, serikali ya Afrika Kusini itabaini kwamba itapata faida kubwa sana kwa kutusikiliza badala ya kusaidia kuficha maovu ya wakosaji.

AR: Wakati wa kilele cha mgogoro wenu na Afrika Kusini, mlifukuza mabalozi wa pande zote mbili. Je, mtawarudisha?

PK: Tuko katika taratibu za kuwarejesha.

AR: Tangu Zuma awe Rais wa Afrika Kusini, uhusiano wako na taifa hilo umeyumba. Je, hii ni kwa sababu ameamua kuwa rafiki wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambayo ni hasimu wako wa kisiasa?

PK: Siwezi kujibu kwa niaba yake. Lakini jambo moja liko wazi kwangu; Sishauri mtu yeyote aingilie katika mambo yangu ya ndani. Huu ni msimamo wangu na haujalishi ni nchi gani; iwe Afrika Kusini, Tanzania, Ufaransa, au Ubelgiji.

AR: Karegeya, Nyamwasa lakini pia Mwendesha Mashitaka Mkuu wa zamani, Gerald Gahima pamoja na Théogène Rudasingwa walikuwa karibu sana na wewe kabla hamjatofautiana. Huna wasiwasi na watu hawa wanaoondoka wakiwa na siri zako nyingi.

PK: Siri gani? Hawa watu walikuwa na nyadhifa katika Jeshi, Usalama, Mahakama na katika siasa kupitia RPF wakiwa chini yangu. Huwezi kusema hawa walikuwa karibu yangu kwa sababu nilikuwa nao kwenye taasisi moja. Wamesema kila walilosema, tena kwa muda mrefu, lakini kuna siri gani waliyozungumza zaidi ya upuuzi?

Wakati tulipokuwa tukifanya kazi pamoja, hawakuwahi kupinga lolote nililopendekeza. Walianza kutofautiana name baada ya kuondolewa kwenye nyadhifa zao.

AR: Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania alikumbana na hasira zako wakati alipopendekeza ukutane kwa mazungumzo na wapinzani wako wakiwamo wale wa FDLR. Hukubaliani na mawazo hayo?

PK: Kitu nisichokubaliana nacho ni kuingiliwa. Haikubaliki kwamba Jakaya Kikwete na serikali yake wajihusishe, kwa namna yoyote, na watu waliohusika na mauaji ya kimbari. Sioni sababu yoyote ya mtu kujihusisha nayo.-

2 comments:

Mtanzania, Washington, DC. said...

Kagame is foolish to keep endless grudges. He should learn to forgive and forge ahead with reconciliation. A few lessons in world history can help this dictator. Cases in point: BLACK South Africans have forgiven the White minority, and so did the Civilized Western powers which reintegrated Hitler's germany to Germany we so much admire today, despite her horrible past. Tanzania and other countries merely want to extend a helping hand so that, future generations of Rwandan children can leave in a peace and harmony. It is about time to wake up Paul!

Anonymous said...

Paul Kagame asidanganye watu hapa, sababu kubwa ni Tanzania kupeleka majeshi yake Democratic Republic of Congo(DRC). Hii inazuia Rwanda kuendelea KUIBA rasilimali za Congo na hilo ni pigo KUBWA kwa Kagame.
Hebu fikiria tu kwa mwezi Rwanda ilikuwa inapata karibu $500 millions kwa kuuza rasilimali( eg coltan,diamond, timber kutoka DRC. Sasa unafikiri huyu ndugu atakaa kimyaa..

Kagame anahangaika tu ndiyo maana kulipiza kisasi kwa TZ, kaamua aungane na Museveni na Kenyata kutengeneza "Coalition of the Willing (COW) kuitenga TZ kwenye uchumi.

Ila Kagame lazima atambue kuwa hana ubavu wowote ule wa kucheza na jeshi la TZ au serikali yake PERIOD!!!.