ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, July 19, 2014

Kesi ya Mbasha yapigwa kalenda

Emmanuel Mbasha akisindikizwa na wadogo zake Patrick (kushoto) na Onesmo kutoka mahakama ya Ilala jana baada ya shauri lake kuahirishwa. Picha na Salim Shao.

Dar es Salaam. Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam jana ilitumia nusu sasa tu kusogeza mbele kesi inayomhusu Emmanuel Mbasha, huku pia ikishindwa kumsomea maelezo ya awali kutokana na wakili wake kuwa safarini.
Kesi hiyo sasa itatajwa tena Julai 23 mwaka huu.
Hatua hiyo ni baada ya mahakama kuelezwa na mwakilishi wa wakili wa mshtakiwa, Daudi Malima kuwa wakili wa Mbasha, Mathew Kakamba yupo safarini Arusha.
Mbasha, mume wa mwimbaji maarufu wa nyimbo za injili nchini, Flora, anakabiliwa na mashtaka mawili ya ubakaji.
Mbali na kuahirishwa kesi hiyo, mahakama hiyo pia ilimtaka wakili wa mshtakiwa kutoa ufafanuzi kutokana na kutofautiana taarifa zilizowasilishwa mahakamani kati ya mshtakiwa na wakili wake.
Mwendesha mashtaka na wakili wa Serikali, Gloria Mwenda alisema shauri hilo lilikuja ili kusomewa maelezo ya awali.
Baada ya Hakimu Wilbarforce Luhwago kutoa ruhusa ya usomwaji kuendelea, mshtakiwa alinyoosha mkono na kueleza kuwa wakili wake alikuwa njiani kuja mahakamani hapo, jambo ambalo mahakama ilikubali na kuongeza nusu saa ili kusubiri.
Kesi ilipoitwa mara ya pili saa 3:00 asubuhi, wakili aliyejitambulisha kama David Malima, aliieleza mahakama kuwa alikuwa amepokea maelekezo ya kumsaidia wakili wa mshtakiwa, Mathew Kakamba ambaye amesafiri kwenda Arusha.

No comments: