Advertisements

Wednesday, July 23, 2014

Msimamo wa Jumuiya ya Waislamu wa Tanzania wa Washington DC Metro (TAMCO) katika Uchaguzi wa DMV

Ndugu wanajumuiya wa DMV pamoja na watanzania wote kwa ujumla popote mlipo. Bila shaka katika miezi ya hivi karibuni mmekuwa mkifuatilia kwa karibu sana kampeni za uchaguzi za viongozi wa jumuiya wa watanzania wa DMV. Wagombea wa nafasi mbalimbali katika jumuiya wamekuwa wakiwaeleza na kunadi sera zao ikiwamo kukosoana baina yao. Hili ni jambo la kawaida katika kampeni yoyote ile inayowajumuisha wagombea wenye misingi na mitazamo isiofanana.

Hata hivyo kuna baadhi ya wanajumuiya ambao ama kwa kutokujua au kwa makusudi wamekuwa wakiivuta jumuiya ya TAMCO na kuinasibisha na watanzania ambao pia ni waislamu katika kinyang’anyiro hiki cha madaraka jambo ambalo sio la haki kwa pande zote. Tunapenda kuchukuwa wasaa huu kutoa tamko la rasmi kuwaeleza nafasi ya TAMCO katika chaguzi za viongozi wa jumuiya ya watanzania DMV.


TAMCO pamoja na wanajumuiya wake wanasikitishwa sana na baadhi ya watanzania kutumia siasa za chuki kuchochea hisia za kidini ambazo athari yake ni kuubomoa umoja uliojengeka kwa miaka mingi baina ya waumini wa dini za kiislamu na kikristo. Tunapenda ifahamike kuwa nguvu na silaha kubwa ya watanzania popote walipo nje ya Tanzania ni umoja wao bila kujali kabila zao, dini zao au hata daraja zao katika jamii. Tunapenda kuwafahamisha watanzania wote kuwa wanaTAMCO kabla ya huu uchaguzi walikuwa wakishiriki katika mambo mbalimbali ya kijamii, kisiasa na kiuchumi kwa kushirikiana na watanzania wa dini nyingine ilihali hawaasi mafundisho ya imani yao na wataendelea kufanya hivyo baada ya uchaguzi kwisha. Haitakuwa busara kwa wao kukaa nyuma, kutishika au kuwa kimya na kuogopa kushiriki kuisaidia jamii yao kama wazalendo kwa sababu ya uislamu wao kwani huu utakuwa ni usaliti na kinyume na mafundisho ya dini yao.


TAMCO kama jumuiya ya dini haijihusishi kwa hali moja au nyingine katika mchakato mzima wa uchaguzi. Viongozi wake wa sasa waliwaeleza waumini wao tarehe 29 June 2014 kuwa wao kama watanzania wana haki ya kushiriki katika uchaguzi bila ya kushinikizwa kumpigia kura mgombea yoyote. Pia jumuiya iliwakataza wagombea kutumia mikusanyiko ya jumuiya yao kuendesha kampeni ili kuheshimu maamuzi ya kila mwanajumuiya. Ni haki ya msingi ya kila mwanajumuiya kufikiri, kufanya maamuzi na kuchagua kiongozi ambaye anahisi atakuwa na manufaa kwake binafsi na kwa watanzania wote kwa ujumla. Hata hivyo si nafasi ya jumuiya ya TAMCO au viongozi wake kuwaamulia wanaumini wao nani wa kuwaongoza hapa DMV.

TAMCO inawasihi wagombea wote pamoja na wapambe wao warudi nyuma na kutafakari juu ya jumuiya wanayopigania kuingoza. Jee hizi shutuma, kejeli, matusi na dharau zitamsaidia vipi mgombea kuwaunganisha watu na taasisi zao za kiimani ambao hisia zao zinaumizwa kila kukicha? Jee kuna mtanzania yoyote hapa DMV aliyepatwa na shida au aliyekuwa na sherehe ambaye hakusaidiwa na watu wa dini nyingine? Ni mtizamo wetu kampeni zenu zimechupa mipaka na kuna hatari ya kujigawa katika matabaka ambayo athari yake hatutaweza kuikarabati kwa muda mrefu.

Mwisho tunapenda kurudia kuwa TAMCO haijihusishi wala haijawahi kujihusisha katika mchakato wa uchaguzi wa viongozi wa jumuiya ya watanzania DMV. Pia ifahamike kuwa sio kila muislamu anaeishi hapa DMV ni mwanachama wa jumuiya yetu. Tunawaomba ifahamike kuwa wanachama wa jumuiya hii si watanzania pekee bali tuna wanajuimuiya hai wa mataifa mengine kama Kenya, Ghana, Nigeria, Marekani, Comoro, Senegal na kadhalika ambao wamejiunga nasi kiimani. Ni matumaini yetu kuwa mmeilewa nafasi ya jumuiya yetu na wanajumuiya wetu katika uchaguzi wa viongozi wa jumuiya na mtachukuwa wasaa kujirudi na kusisitiza mambo ya msingi yanayotuweka pamoja kama watanzania. Tunasisitiza kwa wagombea wote kuacha kulitumia jina la jumuiya yetu kama daraja la uchaguzi.

Tunatanguliza shukurani,

Uongozi wa TAMCO DMV

July 23rd 2014