Askari wa Jimbo la Macau wakiwadhibiti machangudoa waliokamatwa katika oparesheni maalumu.
Munira Mathias, binti wa Kitanzania aliyekuwa akiishi China akitumikishwa kufanya ukahaba, alikimbilia Jimbo la Macau akitokea Guangzhou, baada ya muda wa viza yake kumalizika.
Kama tulivyoona katika gazeti hili jana, Macau nako hakukaa kwani alikimbilia kwa rafiki yake wa Kirusi, baada ya yeye na mwenzake, Candy kutishiwa na mabinti wenzao Watanzania kwa ‘kosa’ la kurekodi ujumbe wa kuomba msaada kisha kuurusha kupitia mtandao wa WhatsApp.
Munira (ambaye si jina lake halisi) aliondoka katika chumba alichokuwa amepanga na kuacha kila alichokuwa nacho, isipokuwa hati ya kusafiria, tiketi ya ndege na kadi ya chanjo ya kuzuia ugonjwa wa manjano.
Itakumbukwa kwamba wakati akikimbia kutoka Guangzhou, tayari Munira alikuwa amemeza vidonge kwa ajili ya kutoa mimba ambayo hata hivyo hakuwa anafahamu baba wa mtoto anayemtarajia, kwani siku alipobakwa na vijana wanne hawakutumia kinga yoyote.
Alitakiwa kumeza vidonge tisa alivyopewa kwa ajili ya kutoa mimba, huku moja ya masharti yake yakiwa ni kutokukutana na mwanaume katika kipindi hicho. Hata hivyo hakuweza kutimiza masharti hayo kwa sababu alikuwa na shida ya pesa, hivyo alikuwa akimeza dawa huku akijiuza. Alikaa kwa rafiki yake wa Kirusi kwa siku nne na wakati huo vidonge alivyokunywa vilikuwa vimeanza kumzidi nguvu, hivyo alikuwa akilegea.
“Nadhani nilikosea masharti, ile mimba haikutoka bali niliona uchafu wenye harufu ukinitoka na nikawaambia ukweli wale marafiki zangu kuwa nina mimba, nikapelekwa tena kwa daktari ambaye alinipa vidonge vingine ambavyo pia havikufanya kazi,” anasema.
Anasema alilazimika kutoa mimba hiyo kwa daktari baada ya kufika Dar es Salaam ambako awali hakuwahi kuwaza kama angerejea, baada ya kuishi China kwa siku 91.
Wale marafiki zake wa Kirusi, waliamua kumvusha aelekee Hong Kong, kisha Tanzania, lakini, alikutana na vikwazo zaidi kwa sababu bado picha yake haikufanana na ile iliyopo kwenye hati ya kusafiria.
“Waliniingiza kwenye chumba maalumu na kuanza kunikagua upya, wakaniambia nifumue nywele nilizosukia, ili wanihakiki,” anasema.
Anasimulia kuwa alifanikiwa kupanda ndege kurudi nchini, akiwa ametimiza siku 91, kuanzia Januari 19 hadi Aprili 10 mwaka huu.
“Ilikuwa ni tukio jingine ambalo sikuwahi kulitegemea maishani. Sikudhani kama ningerudi tena nchini kwangu kwenye amani, sikuamini kwa kweli,” anasema.
Asakwa na mwenyeji
Munira anasema akiwa njiani kurejea Tanzania, alikuwa akiwasiliana na rafiki yake ambaye yupo China bado. Rafiki huyo alimwambia kuwa mwenyeji wake, Jacky alikuwa akimsaka kwa udi na uvumba hivyo awe makini.
“Aliniambia kuwa mwenyeji wangu amesambaza picha zangu Bongo (Tanzania) ili atakayeniona anipige hadi kuniua, kisa sijamaliza deni, ambalo ni Dola 8,500 za Kimarekani (Sh12 milioni),” anasema.
Deni hilo ni malimbikizo ya Dola 200 kwa siku muda wa siku 40, ambazo alipaswa kumlipa mwanamama huyo kutokana na shughuli za ukahaba aliokuwa akiufanya.
Munira anasema alihisi kuwa yule mwenyeji wake atakuwa ametuma watu Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, hivyo aliamua kuwa wa mwisho kabisa kushuka ili kama kuna watu wabaya, wasijue kama amefika nchini siku hiyo.
“Niliposhuka kutoka kwenye ndege, ndugu zangu akiwamo mama na dada zangu walinipokea na mimi nilijizuia nisilie ili wasigundue chochote. Sikutaka wajue kuwa nilipitia shida kubwa... lakini moyoni mwangu najua mwenyewe nilivyokuwa najisikia,” anasema.
Anasema hata hivyo alipohojiwa na mama yake sababu ya kurudi mapema nchini, alimdanganya kuwa hoteli aliyokuwa akifanyia kazi imeungua moto.
Kuhusu maisha ya baadhi ya Watanzania nchini China, Munira anasema wapo wasichana wadogo wa Kitanzania wanapokamatwa au kutaka kusaidiwa kurudi nchini, hukataa wakiwahofia mawakala wanaowapeleka huko.
Mawakala hao huwatisha kuwa wakiwataja au kujaribu kutoroka watawaua. Wengi wanaamini kuwa mawakala hao hutegemea nguvu za ushirikina.
Pamoja na hayo, Munira anasema wasichana wanaofanya biashara ya kujiuza China, hukumbana na ukatili wa kutisha, huku akitoa mfano wa binti aitwaye Habiba ambaye aliingiliwa na Wanigeria kadhaa kwa nguvu na baadaye aliuawa.
Anasema kutokana na hali hiyo, hata yeye anaishi kwa hofu mpaka sasa kwa sababu mawakala wanaosafirisha wasichana wa Kitanzania, wanamtafuta.
“Bado niko kwenye hatari zaidi. Nazidi kusali, kwa sababu bado niliyotendewa hayawezi kufutika katika historia ya maisha yangu na hao wabaya wangu bado wananiwinda,” anasema.
Alikwendaje China?
Munira alizaliwa Oktoba 1991 jijini Dar es Salaam na baada ya kumaliza kidato cha nne alibahatika kusoma kozi ya uhudumu wa hoteli na baada ya kuhitimu aliajiriwa katika hoteli kadhaa kwa nyakati tofauti nchini.
“Nimefanya kazi kwenye hoteli nyingi hapa mjini, lakini nikaamua kujiajiri na nikaanza kununua pochi ambazo nilizisambaza kwenye ofisi mbalimbali, hapa Dar es Salaam,” anasimulia.
Anasema siku moja alifuatwa na mwanamke mkazi wa Sinza, Dar es Salaam ambaye alijitambulisha kuwa anataka kumsaidia kupata kazi nzuri nje ya nchi. Anasema mwanamke huyo aliyeonekana msamaria mwema, kwanza alimuuliza ni fani gani aliyosomea na kumuahidi kuwa angemtafutia kazi.
“Nilipomwambia kuwa nimesomea masuala ya hoteli, alisema kuna kazi nyingi za hoteli nchini China na mishahara ni mikubwa kwa hiyo ningekuwa tajiri baada ya muda mfupi,” anasema.
“Siku moja akaniuliza kama nina hati ya kusafiria, nikamwambia ipo kwenye mchakato wa kutafuta nikipata ningemwambia. Wakati huo kweli nilikuwa natafuta hati hiyo kwa matumizi ya safari zangu nyingine,” anasema.
Anasema alipopata hati ya kusafiria alimweleza mama huyo, ambaye alimwambia kwamba asubiri huku akimpa ahadi kuwa safari huenda ikawa leo au kesho, lakini ahadi hizi hazikutekelezwa.
Siku moja mwanamke huyo, alimwambia kuwa safari yake inakaribia jambo lililomfanya auze vitu vyake vya ndani kwa ajili ya kupata fedha kidogo na kwa sababu nyumbani kwao hakukuwa na nafasi ya kuvihifadhi.
“Nikaamua kupanga hotelini kwa sababu sikutaka kuishi nyumbani kipindi kile, lakini bado nikawa napewa ahadi na yule mwanamke kuwa kesho, kesho, hivyo hivyo,” anasema.
Ushauri wa mama
Anaeleza kuwa kutokana na ahadi kuwa nyingi, mama yake (Mama Munira) alimshauri aachane na safari hiyo akapatwa na hisia kuwa pengine haina mwisho mzuri.
“Mama alinikataza nisisafiri. Aliniambia hiyo safari siyo nzuri, nikamuuliza kwa nini, lakini hakuniambia. Nikaamua kumweleza yule dada kuwa sitakwenda tena kwa sababu mama amekataa. Basi kwa kufanya hivyo nilikuwa nimezua balaa jingine,” anasimulia.
Baada ya kumweleza yule mwanamke, Munira anasema alishangaa anafuatwa na wanawake wanne wakazi wa Magomeni, baadhi yao aliwafahamu na wengine hakuwa akiwafahamu ambao walifika katika hoteli aliyopanga na kuanza kumtukana na kufanya fujo.
Alisema kinamama hao walikuwa wakihoji sababu za kukataa kwake kwenda China, tena dakika za mwisho wakati wao wapo kwenye mchakato wa kumwandalia safari.
“Walifanya fujo kweli hadi uongozi wa hoteli ile ukataka kunifukuza. Yaani walikuwa ni washari, halafu mibonge ya mijimama iliyoshiba kikweli kweli,” anasema Munira.
“Waliniambia niwape Dola za Marekani 350 kwa ajili ya viza na pia niwape hati ya kusaifiria. Wakaja tena siku ya pili wakaniambia safari yangu ni keshokutwa,” anasema.
Aliamua kuwapa kiasi chote cha fedha kilichobaki kwa sababu tu alitaka kusafiri, lakini wakati huo yeye aliamua kuishi kwa rafiki yake kwa kuwa hakuwa na fedha zaidi za kupanga hoteli.
“Niliishiwa pesa kabisa nikabaki na kama laki moja tu, ndiyo maana nikaamua kuishi Gongo la Mboto, kwa rafiki yangu,” anasema.
Safari ya Guangzhou
Munira anasema siku hiyo aliyofika kwa rafiki yake, alipigiwa simu na wale wanawake wakamwambia wanahitaji kuonana naye.
“Nikachukua bajaji kwa Sh15,000 mpaka Magomeni nilipoelekezwa. Nikamkuta huyo dada ambaye alikuwa mgeni kwangu. Alikuwa na mume wake na mimi nilikuwa na rafiki yangu. Nilikuja kujua baadaye jina lake ni Josephine,” anasema.
Anasema Josephine alimdai Sh15,000 ambayo alisema ni kwa ajili ya kukodi gari, kuelekea Uwanja wa Ndege na wakati huo Josephine alikuwa akimjazia kadi ya chanjo ya homa ya manjano.
Anasema alikabidhiwa kadi hiyo na walipofika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, alikuwa tayari ameshapewa masharti kuwa asibebe nguo nyingi, asisuke wala kujipamba sana.
“Tulipofika uwanja wa ndege yule dada akaanza kuniuliza kwamba mimi nitamsaidiaje kwa sababu naye amenisaidia, akawa ananiambia, si umeniona nilivyokusaidia hata fulani na fulani (anawataja majina) nimewasaidia na wewe unanisaidiaje?” anasimulia.
Muda wa kuingia ndani ya ndege ulipofika yule dada alimpa tiketi, lakini akakumbusha tena kuhusu kusaidiwa, ndipo Munira alipoamua kumpa Sh20,000 na baadhi ya nguo zake.
“Lakini, kabla sijaondoka akaniambia nikiulizwa naenda wapi, niseme dada yangu amejifungua na mimi naenda kumwangalia huko China kwa kuwa hana msaidizi,” anasema Munira.
“Jambo la kushangaza ni kuwa alikuwapo msichana mwingine hapo uwanja wa ndege na nilishangaa kuambiwa na mwanamke mmoja kuwa kama naenda China basi nimsaidie mdogo wake ambaye naye anakwenda China,” Munira anasema na kuongeza kuwa alimkubalia.
“Ilitokea tukakaa kiti kimoja, na tukaanza kuzungumza katika mazungumzo yetu nikagundua kuwa naye ameambiwa anaenda China kufanya kazi ya hoteli. Nilishangaa lakini sikushtuka. Mwenzangu alikuwa anaitwa Chantelle,” anasema.
Baridi kali Ethiopia
Baada ya safari ya saa kadhaa, walifika Addis Ababa, Ethiopia ambako ni kituo cha kwanza kabla ya safari ya mojua kwa moja kwenda China, lakini hali ya pale ilikuwa ni ya baridi sana na Munira hakuwa amebeba koti au jaketi.
Munira na Chantelle walisubiri kwa saa tano hivi kabla ya kuondoka Addis Ababa na hata muda wa kuondoka ulipofika, Munira aligundua kuwa pasi yake ya kusafiria ilikuwa haionekani.
“Lakini kwa bahati nzuri baada ya kumwaga vitu vyangu vyote chini, niligundua kuwa pasi yangu ilikuwa imejibana ndani ya begi ndipo niliporuhusiwa kuingia kwenye ndege,” anasema.
Munira na mwenzake, walifanikiwa kufika Guangzhou muda wa saa 9:00 alasiri na huko walikutana na baridi kali kuliko ile ya Ethiopia.
Wakati huo, kila mmoja alikuwa akijaribu kupata mawasiliano ya mwenyeji wake na kwa bahati mbaya, Chantelle hakufanikiwa kumpata mwenyeji wake.
“Nikamwambia Chantelle kwa kuwa tumekuja pamoja halafu wote tumekuja kwa ajili ya kazi za hoteli, wacha nimpigie mwenyeji wangu tuondoke wote hadi utakapompata wa kwako, alikubali,” anasema.
Baada ya kuzungumza na mwenyeji wake aliyefahamika kwa jina moja la Jacky, walielekezwa wakodi teksi hadi katika hoteli moja ifahamikayo kama Nairobian.
Kutoka uwanja wa ndege hadi katika hoteli waliyoelekezwa, ilikuwa ni sawa na umbali wa Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Nyerere na Bagamoyo. Walitakiwa kulipa Yuan 200 ambayo ni sawa na Sh60,000.
Munira anasema, hakumkuta mwenyeji hasa aliyepewa maelekezo yake akiwa Tanzania, bali alipokewa na Mtanzania mwingine aliyeachiwa maagizo na Jacky, ambaye alikuwa amekwenda Malaysia kutafuta viza.
Huo ukawa mwanzo wa maisha yake China, ambayo yalijaa dhiki, mateso na tabu za aina yake. Chantelle kwa upande wake alimpata mwenyeji wake na kuendelea na maisha nchini humo.
3 comments:
nauliza kulikoni mbona mnapigia debe sana issue hizi za machangudoa china au ndo mnataka kuharibu biashara ya watu wanaokwenda china kununua vitu. because nimechunguka kila kukicha story ndo hizi hizi ubalozi uko wapi kuwazibiti madada zetu na kuwasaidia kama nikweli kazi yao inafanya nini mpaka wanachafua jina la taifa letu na wao kuteseka.
to we na majukumu si kuleta story za vijiweni
bongo harudi mtu serikali imelala ukatili kila siku mabomu arusha somalia ilianza kama hivi chamtoto mwisho vita na watoto wanabakwa wanawake wanafanyiwa unyama madawa ya kulewa tumekua kama taifa la Mexico serikali ipo likizo kama haiwezi kuwasaidia wananchi nchini watawajali walionje ya nchi kweli
Tatizo kubwa ni kuamini watu tusiowajua na pia kupenda misheni zisizoeleweka. Mtu anakwambia anakutafutia kazi ya hoteli:
Swali la kwanza kazi gani na Hoteli inaitwaje iko wapi (nchini China)? China ni kubwa sana. Ukishapewa hilo jibu unamkaribisha anayekusaidia kwa ndugu zako na wazazi wako awaeleze na mama yako ajue mwanae huko China atakuwa mikononi mwa nan? Ikiwezekana picha za wahusika wote na vitambulisho na address zao wamuachie mzazi wako. Wakisita wana nia mbaya. Piga simu kwenye Hoteli uliyoambiwa na uulizie kama wana ajiri watanzania (maana kuna wachina, na Mataifa mengi tu wanaotafuta kazi. Maswali mengi yakujiuliza kwamba kwanini mtu akutafutie kazi wewe na hakujui? Maisha magumu jamani tuwe waangalifu.
Post a Comment