ANGALIA LIVE NEWS

Friday, July 11, 2014

Tendwa: Kikwete ameteleza kusemea msimamo wa CCM bungeni

Aliyekuwa Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Mstaafu John Tendwa
Aliyekuwa Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Mstaafu John Tendwa (kushoto) akizungumza na waandishi wa gazeti la Mwananchi, wakati wa mahojiano maalumu ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana. Picha na Edwin Mjwahuzi

Na Ibrahim Yamola na Fidelis Butahe, Mwananchi
Dar es Salaam.  Aliyekuwa msajili wa vyama vya siasa nchini, John Tendwa amesema Rais Jakaya Kikwete aliteleza kueleza msimamo wake na ambao baadaye ulibainika kuwa wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wakati akizindua Bunge Maalumu la Katiba, Machi 21.
Tendwa, ambaye alistaafu Agosti mwaka jana na nafasi yake kuchukuliwa na Jaji Francis Mutungi, alitoa kauli hiyo jana katika mahojiano maalumu na Mwananchi ofisini kwake jijini Dar es Salaam.
Tendwa, ambaye alikuwa Msajili kwa miaka 13, alisema akiwa kiongozi mkuu, Rais Kikwete alipaswa kutoa mwongozo wa uendeshaji wa Bunge Maalum la Katiba.
“Sikuwapo nchini, lakini kwa kadri ninavyoelezwa, kama hiyo ni kauli yake, basi alijisahau kusemea msimamo wa chama chake, (CCM) na sera yake ya serikali mbili katika bunge hilo,” alisema.
“Rais ni mtendaji, alipaswa kutoa guidelines (miongozo) ya jinsi ambavyo Bunge Maalum la Katiba linatakiwa kufanya. Alichokisema, aliteleza.
“Alijisahau na kurudi kwenye chama kwa sababu hiyo ndiyo sera ya chama chake, ” alisema Tendwa.
“Na siyo yeye tu (Kikwete) kwani nimemsikia hata Dk Shein (Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi), akisema kuwa msimamo wa CCM ni serikali mbili,” aliongeza Tendwa.
“Nimemsikia  Makamu wa Pili wa Rais (Balozi Seif Ali Iddi)  akisema hivyo na  Rais wangu (Kikwete) katika mikutano mbalimbali ya hadhara, naye amelisema hilo.”
Madai ya kuibeba CCM
Tendwa ambaye katika uongozi wake wa miaka 13 alikuwa akituhumiwa mara kwa mara na vyama vya upinzani kuwa anakibeba chama tawala, alisema: “Nadhani na yeye (Rais Kikwete) kasema. Nadhani alijisahau kuwa ni kiongozi wa taifa.”
“Rais ni mtendaji na mimi nasema aliteleza. Turudi katika hoja kwa kujadili rasimu iliyoko mezani.”
Kauli hiyo imekuja kipindi ambacho baadhi ya viongozi wakiwamo wa vyama vya siasa nchini, Dk Wilbroad Slaa (Chadema), Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad na pia aliyekuwa mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, pia kumkosoa Rais Kikwete.
Kwa nyakati tofauti, wameeleza kuwa Kikwete ndiye mtu pekee anayeweza kutuliza mvutano ulioibuka katika mchakato huo unaoendelea kwenye Bunge la Katiba.
Ulikoanzia mzozo
Machi 21, wakati akifungua Bunge Maalum la Katiba,  Rais Kikwete aliipinga Rasimu ya Pili ya Katiba iliyowasilishwa na Tume ya Jaji Warioba, akigusia mambo saba ya msingi yaliyomo katika rasimu hiyo na kutaka yatazamwe kwa kina, kubainisha kuwa mengine hayawezi kutekelezeka.
Miongoni mwa mambo hayo ni muundo wa Muungano kuwa wa serikali tatu uliopendekezwa katika rasimu hiyo.
Kikwete, ambaye alisema anatoa maoni yake binafsi, alipinga waziwazi pendekezo la serikali tatu na kuegemea katika muundo wa serikali mbili unaoungwa mkono na CCM, huku akifafanua kuwa idadi ya watu waliopendekeza muundo wa serikali tatu ilikuwa ndogo.
Walilosema wengine
Julai 7, wakati akizungumza katika kipindi chaDakika 45 kinachorushwa na televisheni yaITV,  Maalim Seif alimtupia lawama Rais Kikwete kuwa amechangia kuukoroga mchakato wa katiba kwa kufuata msimamo wa chama chake, badala ya maoni ya wananchi yaliyomo katika rasimu ya pili ya katiba.
Maalim Seif, ambaye alilenga kauli iliyotolewa na kiongozi huyo wa nchi wakati akifungua Bunge la Katiba, alisema kauli ya Rais Kikwete imeondoa imani ya wananchi kuhusu kupatikana kwa katiba inayotokana na maoni yao.
Alisema mchakato huo hivi sasa unamtegemea Rais pekee, huku akisisitiza kuwa hakuna binadamu aliyekamilika na kumshauri kutafuta uwezekano wa kuweka mambo sawa, ili kujenga tena imani kwa wadau wote.
Julai 4, Dk Slaa, wakati akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili jijini Dar es Salaam, alimtaka Rais Kikwete kujitokeza hadharani kutafuta suluhu ya kupata mwafaka wa mchakato wa Katiba Mpya kwa kuwa hakuna mamlaka nyingine zaidi inayoweza kuunusuru.
Naye Jaji Warioba kwa nyakati tofauti amemshauri  Rais Kikwete kuchukua hatua zitakazoondoa matatizo katika Bunge la Katiba ili kuwezesha mchakato huo kukamilika.
Alisema ni muhimu kiongozi huyo mkuu wa nchi kuweka kando tofauti za mawazo na mitazamo ili kupata Katiba Mpya kwa masilahi ya Taifa.
Mwanzoni mwa wiki, mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mbeya na naibu waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Godfrey Zambi alifichua kuwa msimamo wa serikali mbili unaoonyeshwa na wabunge wa chama hicho ni maagizo ya Kikwete.
Awashauri Ukawa
Kuhusu Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Tendwa aliwashauri wajumbe  wote wanaounda umoja huo kurejea bungeni ili kujadili vipengele vinavyogusa maslahi ya wananchi na kuweka kando sura ya kwanza na sita zinazohusu muundo wa Serikali.
Aliwataka wajumbe wanaounda Ukawa kuacha kususia vikao na kutoka  kwenye Bunge  la Katiba kama walivyofanya tangu Aprili 16 na kusema kuwa busara zaidi ndizo zinazotakiwa kutumika kupitia majadiliano  kwa lengo la kumaliza mgogoro uliopo na kuwezesha mchakato kuendelea.
Alisema rasimu siyo katiba bali ni andiko linaloweza kubadilishwa na kuvunjwa vunjwa, hivyo wajumbe wa Ukawa warudi bungeni na kuandaa rasimu ya katiba itakayokwenda kupigiwa kura na wananchi.
 “Unatoka nje na unasema hurudi, wewe ni nani? Kunahitajika hapa uvumilifu wa kisiasa. Watu hawa (Ukawa) na wengine wanatakiwa kuaminiana katika mchakato huu. Warudi bungeni wajadili vifungu vya katiba vinavyowagusa wananchi.
“Wasijadili pekee muundo wa Muungano,  wajadili vifungu vinavyohusu wananchi, kisha iandikwe rasimu itolewe  kwa wananchi kwa muda mwafaka na wao waende  huko  wawaelimishe ili wafanye uamuzi sahihi.
“Hoja ya msingi iwe upigaji kura uwe wa serikali mbili au tatu kwa kuwa vifungu vingine vimekwishaafikiwa,” alisema Tendwa.
Aliongeza kuwa inashangaza kuona tangu wajumbe hao watoke bungeni ofisi ya msajili wa vyama vya siasa haikutakiwa kuendelea kukaa kimya kuhusu Ukawa wanaojitangaza kinyume cha kanuni na sheria.
“Ofisi  hiyo (ya msajili) imekuwa kimya, haisemi lolote kuhusu Ukawa. Hawana uhalali wa kisheria na mamlaka. Kwa hiyo msiwakuze bure bila sababu ya msingi kwani hatujui wameanzia wapi, mizizi yao ipo wapi,” alisema.
Kuhusu lugha  inayotumiwa na wajumbe kwenye Bunge la Katiba, Tendwa alisema ni ya mitaaani na wakati mwingine watoto hutumia lugha nzuri kuliko ya wabunge hao.
“Lugha ya matusi kuingizwa bungeni ni aibu. Hata watoto hawafanyi hivyo, lakini wabunge tunaowategemea kabisa ndio wamekuwa wakitumia maneno ya kibabe na kejeli. Wanatakiwa kujifunza kuwa wanapoingia bungeni lazima lugha za mitaani waziache nje,” alisema.
Bunge la Katiba linatarajiwa kuendelea tena Agosti 5, huku kukiwa na wasiwasi kama wajumbe wa Ukawa watarejea au la baada ya kususia vikao hivyo.
Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta tayari ameitisha kikao cha Kamati ya Mashauriano chenye wajumbe 27 kitakachofanyika jijini Dara es Salaam Julai 24 kwa lengo la kuinusuru katiba hiyo na kuwashawishi Ukawa kurejea bungeni.
Wakati akistaafu, Tendwa alisema anajivunia kuifanya ofisi ya Msajili iwe ya kisasa, akisema aliteuliwa bila ya kupewa adidu za rejea na alitegemea kuwa ofisi hiyo ingekuwa na wanasheria, lakini alijikuta mtu pekee mwenye taaluma hiyo.

No comments: