ANGALIA LIVE NEWS

Friday, July 18, 2014

Lowassa, Membe waitesa CCM

Na Raymond Kaminyoge, Mwananchi
Dar es Salaam. Vigogo sita wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), akiwamo Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe ambao walipewa onyo kali na kuwekwa chini ya uangalizi kwa miezi 12 wamezidi kukitesa chama hicho, na katika kuwadhibiti, kimetoa maagizo kwa Kamati ya Usalama na Maadili kufuatilia nyendo zao.
Uamuzi huo ulifikiwa juzi katika kikao cha kawaida cha Kamati Kuu ya CCM kilichofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, kuwa kamati hiyo ifanye mapitio ya mwenendo wa utekelezaji wa adhabu kwa vigogo hao waliotiwa hatiani kwa kufanya kampeni za urais kabla ya wakati.
Vigogo waliopewa adhabu hiyo ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye.
Wengine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja.
Vigogo hao ambao wamekuwa wakitajwa na wakati mwingine wenyewe kuzungumzia nia ya kushika nafasi hiyo, walipewa onyo kali ikiwamo kuwaweka chini ya uangalizi kwa miezi 12 tangu Februari mwaka huu ili kuhakikisha hawajihusishi na vitendo vyovyote vinavyokiuka maadili ya chama hicho.
Vigogo hao walipatikana na makosa ya kuvunja ibara ya 6 (2) (1-5) ya maadili ya viongozi wa chama hicho inayozuia kutoa michango, misaada, zawadi za aina yoyote, kukusanya michango na kufanya kampeni bila ya kupata kibali kutoka kamati ya siasa ya halmashauri ya eneo husika.
Jana, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alisema mwezi ujao kamati hiyo itafanya mapitio ya utekelezaji wa adhabu hiyo ili kubaini iwapo wanaitekeleza au la.
“Kama itabainika kuwa hawatekelezi ipasavyo masharti ya adhabu zao, itapendekezwa kwa Kamati Kuu ili waongezewe adhabu nyingine kufuatana na taratibu za chama,” alisema Nnauye.
Kwa mujibu wa Nnauye, Kamati Kuu imepokea taarifa za kuwapo kwa harakati za baadhi ya wanachama walioonyesha nia ya kuomba ridhaa ya chama hicho kugombea urais.
“Baada ya kutafakari kwa kina Kamati Kuu inawakumbusha kuwa ili wanachama hao wasipoteze sifa za kugombea, ni muhimu wakazingatia katiba, kanuni na taratibu za chama zinazosimamia masuala hayo,” alisema Nnauye.
Tangu wapewe adhabu hiyo, makada hao wamekuwa wakijitokeza hadharani kwa nadra, lakini Makamba na Wassira walikaririwa na vyombo vya habari wakitangaza nia ya kugombea urais.
Hata hivyo, CCM ilisema kuwa Makamba hakukiuka taratibu kwa kutangaza nia hiyo, ingawa Rais Jakaya Kikwete alisema mtoto huyo wa katibu mkuu wa zamani wa chama hicho anataka mambo makubwa na hakumtaarifu nia hiyo.
Yajadili Ukawa
Kuhusu mchakato wa kuandika Katiba Mpya, Nnauye alisema Kamati Kuu imefurahishwa na mazungumzo yanayosimamiwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi kati ya CCM na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kujaribu kuwashawishi wapinzani kurejea bungeni.
“Kamati imepongeza juhudi zinazofanywa na msajili na kwamba ni imani yake kuwa mazungumzo hayo yatazaa matunda ili wajumbe waliosusia Bunge Maalumu la Katiba waweze kurejea kuendelea na mijadala ya mchakato wa Katiba Mpya,” alisema Nnauye.
Wajumbe wa Bunge wanaounda Ukawa walisusia Bunge Aprili mwaka huu ni kutoka vyama vya upinzani vya Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF na baadhi ya wajumbe wa kundi la 201 ili kushinikiza kujadiliwa kwa rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyopendekeza muundo wa serikali tatu badala ya ile ya serikali mbili inayodaiwa kupigiwa debe na CCM.
Wajumbe hao wanasisitiza hawawezi kurudi bungeni hadi watakapohakikishiwa kwamba kitakachokwenda kujadiliwa bungeni ni Rasimu ya Katiba na si vinginevyo.
Kutokana na hali hiyo, Jaji Mutungi ameanzisha mazungumzo na vyama hivyo ili kuwashawishi wajumbe kubadilisha uamuzi wao na hatimaye kurejea bungeni Agosti 5, mwaka huu.

No comments: