Upande wa utetezi ukiongozwa na mawakili; Rajab Issa na Albert Msando, uliiambia Mahakama ya Wilaya hiyo kwamba, Mbowe alishindwa kufika mahakamani jana asubuhi baada ya gari lake kupata hitilafu na kisha kuachwa na ndege.
“Mheshimiwa hakimu, mteja wangu ameshindwa kufika mahakamani kwa sababu gari lake limepata hitilafu wakati akielekea uwanja wa ndege (Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere-JNIA).
Aliachwa na ndege iliyokuwa inakuja KIA. Kwa hiyo, naomba ichukuliwe kama udhuru na taarifa rasmi ya mahakama,” alisema Wakili Rajab.
Hata hivyo, wakili huyo alimweleza Hakimu Mfawidhi, Denis Mpelembwa, kwamba miongoni mwa mashahidi watakaotoa ushahidi wao mahakamani hapo ni Mbowe mwenyewe pamoja na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, Clement Kwayu.
Baada ya taarifa hiyo, Hakimu Mpelembwa alisema mahakama imepokea rasmi ujumbe huo kama taarifa ya mahakama na kwamba, usikilizwaji wa utetezi wa shauri hilo utaanza Agosti 18, mwaka huu.
“Kwa kuwa mdhamini wa Mbowe yupo, dhamana ya mshitakiwa inaendelea kama kawaida lakini pia naamini upande wa utetezi umejipanga vizuri kuhusu mashahidi na vielelezo.Ushahidi wenyewe utatolewa kwa njia ya kiapo,” alisema Hakimu Mpelembwa.
Katika kesi hiyo ya jinai namba 73 ya mwaka 2011, Mbowe akiwa mmoja kati ya wagombea ubunge wa jimbo la Hai, anadaiwa kumshambulia Nassir Yamin katika Kijiji cha Nshara, Kata ya Machame Kaskazini, Wilaya ya Hai.
Katika uchaguzi huo, Mbowe aliibuka mshindi kwa kupata kura 28,585 akifuatiwa na Fuya Kimbita (CCM) kura 23,349, Hawa Kihogo (UDP) kura 258 na Petro Kisimbo (TLP) 135.
Hatua ya Mbowe kutakiwa kutaja orodha ya mashahidi wake mahakamani na kisha kuthibitisha kutohusika kwake katika tukio hilo, unatokana na uamuzi uliotolewa hivi karibuni na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya hiyo kwamba, mahakama imeona ana kesi ya kujibu katika shitaka la kumshambulia mwangalizi wa ndani katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment