ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, July 5, 2014

NEYMAR NJE KOMBE LA DUNIA

Neymar nje Kombe la Dunia

Kampeni za Brazil kutwaa Kombe la Dunia kwa mara ya sita zimepata pigo baada ya nyota wao, Neymar kuteguka uti wa mgongo.

Neymar hatakuwapo katika kikosi cha Luiz Felipe Scolari kitakachowavaa Ujerumani kwenye nusu fainali, hivyo watahitaji kazi ya ziada.

Neymar alikanyagwa kwa goti mgongoni na Juan Zuniga wa Colombia dakika za mwisho za mechi baina ya timu hizo Ijumaa hii, ambapo Neymar (22) alionesha kuwa na maumivu makali, akilia hadi wakati akipelekwa nje kwa machela.

Imethibitishwa kwamba amevunjika moja ya mifupa ya vifundo vya uti wa mgongo katika mechi ambayo Brazil walishinda 2-1 na hataweza tena kucheza mechi yoyote ya fainali hizi zinazomalizika Julai 13.

Mwamuzi hakuona rafu hiyo iliyofanywa katika eneo la nyuma la Brazil dimbani, na alikuja kushituka baada ya rafu nyingine kufanyika upande wa Colombia, dhidi ya mchezaji wa Brazil pia.

Kwa nyota huyo wa Barcelona kutoka nje ya mashindano, huenda mchezaji wa Chelsea, Willian anaweza kupewa nafasi, lakini Scolari alikiri kuwa ni pigo kubwa.

Alishasema tangu mwanzo kwamba nyota wake huyo angewindwa uwanjani, na alikuwa akilalamika katika mechi kadhaa jinsi asivyolindwa na waamuzi.

Baada ya kupata huduma ya kwanza, Neymar alipelekwa hospitali Fortaleza, ambapo daktari wa timu, Rodrigo Lasmar alisema hataweza kucheza lakini hahitaji upasuaji isipokuwa lazima atulie sehemu moja ili apone ndani ya wiki kadhaa.

Alikuwa ndio kwanza amepona kutokana na maumivu ya paja aliyopata baada ya mechi ya raundi ya pili dhidi ya Chile na ilidhaniwa angekosa mechi hii ya robo fainali.

Neymar amecheza mechi zote tano za Brazil katika fainali hizi na ndiye kinara wa mabao kwa Samba Boys hao, akiwa na mabao manne, mawili nyuma ya mshambuliaji wa Colombia, James Rodriguez.

Brazil sasa watawakosa wachezaji wao wawili muhimu – Neymar na nahodha Thiago Silva aliyeoneshwa kadi nyingine ya njano Ijumaa hii, n Scolari itabidi aje kivingine kukabiliana na vijana wa Joachim Low kwenye nusu fainali.

UBELGIJI WATAKA KUWEKA HISTORIA

Ubelgiji wamejipanga kuweka historia kwa kuwaharibia Argentina wanapopambana nao Jumamosi hii katika robo fainali ya kwanza.

Kocha Marc Wilmots amewataka wachezaji wake chipukizi kurudia yale ya kaka zao ya 1986 kwa kutinga nusu fainali bila kuwaogopa Argentina wenye Lionel Messi.

Mashetani Wekundu (Ubelgiji) wanakabiliana na Argentina ambao pia walikabiliana nao kwenye nusu fainali na kupoteza enzi za Diego Maradona, na sasa Wilmots anataka vijana wake wacheze soka ya kushambulia licha ya tishio la uwapo wa Messi.

“Tunaweza kuandika historia, Argentina hawatatupelekesha, tutacheza mchezo wetu wenyewe wala si kuwafuatisha, hakuna kupaki basi, tutacheza soka iliyokamilika pasipo kuacha eneo lolote likiwa wazi kwa adui, tutashambulia na kulinda lango kwa pamoja,” anasema raia huyo wa Ubelgiji.

Anatamba na vijana wake kama Eden Hazard na Romelo Lukaku wa Chelsea, Divoc Origi wa Lille, Vincent Kompany wa Manchester City, Marouane Fellaini wa Man United, Thomas Vermaelen wa Arsenal na wengineo.
Argentina wanao akina Messi, Angel Di Maria, Sergio Aguerro, Gonzalo Higuain na wengineo wanaonolewa na kochaAlejandro Sabella.

COSTA RICA WALIA NA ARJEN ROBBEN 

Costa Rica nao wanakabiliana na Uholanzi ambao wanaongoza kwa kufika mara nyingi zaidi hatua ya fainali pasipo kutwaa ubingwa.

Walichukuliwa kama wasindikizaji lakini wakaushangaza ulimwengu wa soka walipofika hatua ya robo fainali.

Hata hivyo, kocha wao, Jorge Luis Pinto amesema tatizo lao kubwa ni udanganyifu wa kujirusha au kujiangusha bila kuguswa kwa winga wa wapinzani wao hao, Arjen Robben.

Kocha Pinto amesema kwamba iwapo Robben atarudia udanganyifu wake lazima aaibishwe Jumamosi hii.
Robben (30) anayecheza Bayern Munich amekuwa akishutumiwa mara kadhaa kwa kujirusha na wiki iliyopita alikiri kwamba alijiangusha pasipo kukwatuliwa walipocheza na Mexico na akaomba radhi.

“Nawaomba sana Fifa na waamuzi wamwangalie Robben, kwa hakika tuna hofu sana juu ya kujiangusha kwake na ameshakiri kufanya hivyo hivyo kumpa kadi nyekundu ni kitendo cha kimantiki zaidi Jumamosi hii,” anasema Pinto.

Fifa hawajamchukulia hatua Robben, wakidai kwamba hakuna kanuni zilizovunjwa na mchezo wa leo unasimamiwa na mwamuzi kutoa Uzbekistan, Ravshan Irmatov.
Mshindi baina ya Ubelgiji na Argentina atakwaana na atakayeibuka kifua juu kati ya Costa Rica na Uholanzi.
CREDIT:TANZANIA SPORTS

No comments: