ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, July 16, 2014

NSSF yaibeba Yanga

Na Doris Maliyaga, Mwananchi
Dar es Salaam. Wachezaji wa Yanga wameipiga bao Simba baada ya kupata dili la nyumba kutoka Shirika la Hifadhi ya Jamii NSSF.
Wachezaji wote wa kikosi hicho pamoja na benchi sasa wanaweza kukopa nyumba za gharama tofauti kutoka katika mfuko huo zilizopo Mtoni Kijichi ua mradi mpya wa Kigamboni unaoitwa Dege Ego Village. Hata hivyo, Mkurugenzi wa uendeshaji wa NSSF, Crescentius Magoli amesema Yanga wamekuwa wa kwanza kwa sababu wameonyesha nia na klabu nyingine zinakaribishwa.
Akitolea ufafanuazi juu ya upatikanaji wa nyumba hizo, Magoli alisema: “Hii bahati kwenu na mko huru kuchukua nyumba yoyote iliyo katika miradi yetu na kulipia kidogokidogo,” alisema Magoli.
“Unapochukua mkopo wa nyumba za NSSF muda wa malipo ni miaka 15 na utakapolipia kwa muda wa miezi mitatu, utapewa funguo ya kuishi nyumbani kwako huku ukiwa unalipa zile pesa nyingine za deni kidogo kidogo,” alifafanua Magoli.
Katibu wa Yanga, Beno Njovu alisema: “Huu ni mpango mzuri kwani utasaidia kubadilisha maisha kama watapewa nyumba ambazo watazilipa kwa miaka 15... ni bahati.”
“Pia, unafanyika mpango wa kuanza kukatwa kwa misharaha ya wachezaji ambayo itakuwa akiba kwenye mfuko NSSF,” alisema Njovu.

No comments: