Advertisements

Sunday, July 20, 2014

Nyambui: Niliomba nifungwe miaka 100 jela

Suleiman Nyambui
Dar es Salaam. Kocha wa timu ya taifa ya riadha na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Suleiman Nyambui amesema aliomba afungwe miakba 100 jela kama ikibainika anajihusisha na usafirishaji wa dawa za kulevya.
Kocha huyo mpya wa timu ya taifa alisema bado anateswa na ‘mzimu’ wa kashfa ya kusafirisha dawa za kulevya iliyowahi kumkabili, kashfa iliyoichanganya familia yake na yeye mwenyewe.
Nyambui aliliambia gazeti hili katika mahojiano maalumu kuwa, katika maisha yake ya riadha tangu akikimbia miaka 1970 hadi hivi sasa akiwa ni kocha na katibu mkuu, hakuna changamoto kubwa ambayo hataisahau kama siku alipoitwa kuhojiwa juu ya tuhuma hiyo.
Kigogo huyo wa RT alisema alijikuta akiingia matatani na kuhojiwa na kitengo cha kudhibiti dawa za kulevya hapa nchini kwa saa sita mfululizo juu ya kuhusika kwake na uuzaji na usafirishaji wa dawa za kulevya.
“Kiukweli watu wa kitengo cha kudhibiti  dawa  za kulevya walikuwa na vielelezo vyote vya namna  RT ilivyohusika kuwaombea visa watu waliokamatwa na dawa za kulevya ambao nakiri mimi ndiyo nilihusika kuwaombea, lakini sikujua kama ni wauza ‘unga’,” alisema Nyambui.
Watu hao walikuwa wadhamini wa RT na waliwasaidia wanariadha wa Tanzania kwenda Australia kushiriki mashindano ya kimataifa ya kutafuta viwango vya kushiriki Olimpiki ya 2008 huko Beijing, China.
“Kiukweli sikujua kama wanahusika na kusafirisha dawa za kulevya, hivyo hata waliposema wanakwenda kuipa sapoti timu huko sikuona ajabu kwa kuwa walionekana kupenda riadha hivyo RT tukafanya jitihada za kuwaombea Visa kwenye ubalozi wa Australia nchini Kenya,” alisema Nyambui.
Inaendelea Uk.31
Alisema waliondoka wanariadha watatu na wadhamini wao hao, lakini wakiwa uwanja wa ndege wa Australia, ujumbe huo wa Tanzania ulihisiwa kubeba dawa za kulevya ndipo walikaguliwa na kukutwa nazo.
“Nilipigiwa simu na askari wa Australia na ubalozi wa Australia Kenya juu ya watu hao hata hivyo wanariadha niliowaombea wakatufute viwango wao waliposachiwa hawakukutwa na dawa za kulevya isipokuwa wale wadhamini ambao walikutwa nazo,” alisema Nyambui.
Anasema alipata misukosuko ya hapa na pale japo ushirikiano alioutoa kwenye ubalozi na kitengo cha kudhibiti dawa za kulevya hapa kwa kueleza ukweli ndivyo vilimuweka huru japo alitakiwa kuripoti kila  Ijumaa makao makuu ya kitengo hicho kwa mahojiano zaidi hadi pale uchunguzi ulipopatikana.
“Siku ya kwanza nilipoitwa kwenye kitengo cha kudhibiti dawa za kulevya hapa nchini nilihojiwa kwa saa sita, hali ile iliniathiri na kuipa wakati mgumu familia yangu, nakumbuka kila baada ya dakika 10 niliomba ruhusa kwenda kujisaidia kutokana na kiwewe, lakini nasisitiza watu wale sikujua kama wanahusika na dawa za kulevya hivyo walipokuja kutusaidia ukizingatia na hali halisi ya chama hatujiuliza mara mbili, kama ‘ningetonywa’ mapema sidhani kama ningebeba msalaba huo.”
Kwanini anang’ang’ania madaraka RT
Nyambui ambaye amekuwa akilalamikiwa kung’ang’ania madaraka RT bila mafanikio alisema anaongoza riadha kwa mapenzi yake kwa kuwa ni mchezo ulioko kwenye damu yake tofauti na wengi wanavyodhani kuwa ana maslahi binafsi ndani ya shirikisho hilo.
“Kuna wakati uwa natamani kuacha kuongoza RT, lakini nashindwa kwa kuwa riadha hiko kwenye damu yangu, japo nafanya kazi katika mazingira magumu ila naamini katika maisha ya kawaida binadamu wote hawawezi kukupenda wapo wanaotambua mchango wangu kwenye riadha na wanaonichukia pia wapo.”
Fedha za IAAF zinatumikaje
“IAAF (Shirikisho la riadha la kimataifa) uwa linaipa nchi wanachama kiasi flani cha fedha ambapo kwa Tanzania inapata dola 15,000 kwa mwaka, fedha hizo ni kwa ajili ya shughuli mbalimbali za riadha,”
Anasema IAAF inatoa fedha hizo baada ya chama cha kitaifa kufanya aidha mashindano, kozi na vitu vingine vya riadha ambavyo vinakifanya chama kuwa hai.
“Mfano tumefanya mashindano ya taifa hivyo tukituma ripoti hiyo IAAF tunafuzu kupewa dola 5,000, tukifanya kitu kingine kama kozi tunapewa fedha nyingine ambazo fedha hizo ni kwa ajili ya mambo ya kiutawala, haturuhusiwi kutoa hata senti moja kwenye mashindano ya taifa kwa kuwa IAAF inasema mashindano ya taifa na ya kwetu wenyewe hivyo ikibainika tumetumia kwa ajili hiyo tunaweza tukanyimwa kabisa.”
Kwa nini wanariadha wanagomea timu ya taifa
“Wanariadha wengi wa Tanzania hawana elimu ya darasani, hili ni tatizo japo watu uwa wanaamini michezo ainahusiani na elimu, lakini si kweli, elimu inaendana na michezo kama wangekuwa wamesoma wangekuwa mbali.
“Wengi wanapelekwa pelekwa, mtu anafikiria fedha za haraka haraka lakini anashindwa kutambua kama akiiletea nchi medali anaweza kupata fedha zaidi ya zile anazopata kwenye mbio za fedha wanazokimbilia na kukataa kujiunga na timu ya taifa,”.
Anasema wanariadha wa Tanzania wangeweza kufanikiwa zaidi kupitia riadha kama wangekuwa na elimu kwani wanakosa ofa za kimasomo nje ya nchi kama ilivyo kwa Wakenya na Waganda kwa kuwa wengi wameishia darasa la saba na kidato cha nne.
Kupitia riadha alinunua nyumba Marekani
“Kupitia riadha nimefanikiwa kununua nyumba Marekani huko Texas ambapo anaishi mtoto wangu wa kiume nilizaa na mzungu, pia nimejenga Buzuruga na Bukumbi Misheni jijini Mwanza na hapa Dar es Salaam mbali na riadha mimi ni mfanyabiashara wa maduka,” alimaliza Nyambui.
MWANANCHI

No comments: