ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, July 12, 2014

Pinda: Serikali itajenga reli mpya Dar-Mwanza-Isaka hadi Burundi

Waziri Mkuu alipotumia usafiri wa treni kwenda na kurudi mji wa Reading kutoka London

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amesema serikali ina mpango wa kujenga reli mpya kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza kupitia mikoa ya kati kuelekea Isaka hadi Burundi ambapo ujenzi wake utazinduliwa rasmi Desemba, mwaka huu.
Alitoa kauli hiyo juzi wakati akijibu maswali ya Watanzania waishio Reading, nchini Uingereza.

Waziri Mkuu ambaye alitumia usafiri wa treni kwenda na kurudi
mji wa Reading kutoka London, alisema ni mara yake ya kwanza kufika kwenye mji huo na akaahidi katika siku za usoni kufanya mikutano ya aina hiyo kwa Watanzania waishio kwenye miji mingine ya Uingereza kulingana na ratiba ambayo watu wa ubalozini watakuwa wameipanga.

“Kuna mtu ameulizia kuhusu tatizo la usafiri nchini Tanzania, napenda kuwahakikishia kwamba serikali imeamua kuwekeza kwenye mradi mkubwa wa ujenzi wa reli ya kati. Reli hii itaanzia Dar es Salaam hadi Isaka, Isaka hadi Burundi; itatokea Tabora hadi Kigoma na Tabora hadi Mwanza pamoja na kipande cha Kaliua hadi Mpanda,” alisema.

“Mradi huu ni mkubwa ambao ujenzi wake utagharimu dola za marekani bilioni saba, na utatuchukua karibu miaka minne. Kwa hiyo ikiifika Desemba, mwaka huu utafanyika uzinduzi rasmi kwa njia zote hizi za reli,” alisisitiza Waziri Mkuu.

Alisema ili kufanikisha ujenzi serikali imeamua kujenga upya reli ya kati kwa standard gauge hali ambayo haitaathiri usafiri wa treni kwa kutumia njia ya zamani. “Safari hii tumeamua kujenga upya, na siyo kubanduabandua ili wakati reli mpya ikiendelea kujengwa na ile ya zamani inaendelea kutoa huduma kama kawaida,” alisema huku akishangiliwa.

Watanzania hao pia walimuuliza kuhusu ujenzi wa barabara ya Lindi-Mtwara, ujenzi wa hospitali ya Kagwa, ujenzi wa uwanja wa ndege wa Musoma, utaratibu wa utoaji wa mizigo bandarini na usumbufu wanaoupata, uraia wa nchi mbili, tatizo la walimu na hali ya elimu nchini ambayo yote aliyajibu na kuahidi kufuatilia masuala mengine akifika nyumbani.

Aliwataka Watanzania waishio nchi za nje (wana Diaspora) kufuatilia kwa makini mikutano ya uwekezaji ambayo hufanyika kwa kanda au kwa mikoa ili iwasadie kubaini fursa za uwekezaji zilizoko kwenye mikoa wanayotoka.
Leo anatarajiwa kukutana na Watanzania waishio Uingereza kwenye mkutano utakaofanyika kwenye ubalozi wa Tanzania, jijini London.
CHANZO: NIPASHE

No comments: