ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, July 8, 2014

Polisi wa `Tigo` rushwa kwa kwenda mbele

  Pikipiki zawa nyenzo ya kusanya bila huruma
  Sasa wajigeuza trafiki na kuvizia malori
Polisi wa doria wanaotumia pikipiki maarufu kama tigo wakiwa mtaani. Picha/ Maktaba yetu

Askari polisi wanaotumia pikipiki wanaofahamika kwa jina maarufu la Tigo Fasta, wamekuwa kero kubwa jijini Dar es Salaam, kutokana na kuacha kutekeleza jukumu lao la kupambana na uhalifu na kujiingiza katika vitendo vya kukamata magari ya mizigo na kudai rushwa.

Polisi hao wanalalamikiwa kwa kukamata malori ya mizigo zikiwamo Fuso na Pick Up, pamoja na kukamata magari mengine yanayokiuka sheria za usalama barabarani wakati ni jukumu la askari wa usalama barabarani.

Askari hao wanadaiwa kujiwekea utaratibu katika kila gari wanalolisimamisha kuwatishia madereva ili wawapatie kitu chochote.

Uchunguzi uliofanywa na NIPASHE katika jiji la Dar es Salaam, umebaini kuwa, kitengo hicho kilianzishwa wakati wa uongozi wa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Mstaafu, Said Mwema, kwa lengo la kukabiliana na matukio ya uhalifu hususani ujambazi, lakini kazi zinazofanywa na askari hao sasa ni kinyume cha malengo yaliyokusudiwa.

Imebainika kuwa askari hao ambao kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa awali na Jeshi la Polisi, wanatakiwa kutembelea maeneo ya makutano ya barabara, lakini mara nyingi hawafanyi hivyo, badala yake wanapenda kuzungukia maeneo ambayo yanakuwa na malori ya mizigo yanayosafirisha bidhaa kutoka jiji la Dar es Salaam kwenda mikoani na nje ya nchi.

MAENEO WANAYOPENDA
Maeneo ambayo mara nyingi askari hao hupenda kuzungukia ili kujipatia fedha kutoka kwa madereva wa magari na mizigo inayokuwa inasafirishwa ni barabara zinazotoka Kariakoo hasa eneo la Jangwani kuelekea Kigogo na barabara ya Morogoro.

Baadhi ya wafanyabiashara, wamiliki wa magari na wananchi kwa ujumla waliozungumza kwa nyakati tofauti na NIPASHE, walisema tangu kuanzishwa kwa kitengo cha askari wa pikipiki hakuna mafanikio yaliyopatikana katika kudhibiti kasi ya matukio ya ujambazi, badala yake wameongeza kero kwa kukamata magari ovyo na kulazimisha wamiliki wake watozwe fedha.

“Askari polisi wengi wanaotumia pikipiki maarufu kama Tigo Fasta utawakuta kibao maeneo ya Jangwani wakifuatilia magari (pick up) zinazoleta mizigo inayosafirishwa mikoani. Wanadai risiti za mizigo na kama hamna huwa wanadai kitu kidogo,” alisema Juma Mohamed, dereva wa maroli ya mizigo.

Mohamed alisema polisi hao ukiwaona wanavyozunguka eneo la Jangwani huwezi kuamini kama wanadhibiti ujambazi na kwamba wananchi huwa wanajiuliza kama wamepewa hizo pikipiki kwa kazi hiyo au kulinda raia na mali zao.

Mwananchi mwingine, Eliza Jonhson, alisema jukumu la kuanzishwa kwa askari polisi wa pikipiki ilikuwa ni kukabiliana na matukio ya ujambazi, lakini bahati mbaya waliopewa jukumu hilo wanatumia vibaya kwa kujihusisha na vitendo vya rushwa.

Alisema viongozi waandamizi wa jeshi hilo wanapaswa kutafakari upya kitengo cha askari hao kwa sababu wanalichafua jeshi kutokana na kufanya kazi ambazo haziwahusu kwa lengo la kujipatia fedha kwa njia haramu.

Uchunguzi zaidi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa Juni 23 mwaka huu, askari hao wakiwa katika pikipiki yao yenye namba za usajili PT 2743 walisimamisha pikipiki ya miguu mitatu (Bajaj) eneo la barabara ya Kigogo-Jangwani saa 4:30 asubuhi.

Juni 30, askari hao wakiwa katika pikipiki namba PT 1613 kwenye makutano ya barabara ya Nyerere na Mandela eneo la Tazara walikamata pikipiki tatu zenye namba za usajili T451 BJP T600 AQC na T326 CEG saa 4:00 asubuhi.

Askari hao hao walikuwa katika pikipiki PT 1613 katika eneo la Jangwani karibu na ofisi za klabu ya Yanga saa 7:00 mchana walisimamisha teksi yenye namba za usajili T788 BXX na kuanza kulikagua gari hilo pamoja na kumtaka dereva aonyeshe leseni yake.

Juni 24, mwaka huu saa 5:30 asubuhi eneo la Banana barabara ya kuelekea Gongolamboto, askari hao walionekana walisimamisha gali dogo la mizigo aina ya Pick Up yenye namba za usajili T 196 CLD na walifanya mazungumzo na dereva wa gari hilo kwa takribani dakika 20 kabla ya kumuachia.

Juni 29, mwaka huu katika eneo la Magomeni askari hao walionekana wakiwa wamesimamisha gari namba T 253 AGW Toyota Rav4 saa 3:00 asubuhi na kufanya mazungumzo na dereva wa gari hilo kwa muda mrefu.

Imebainika kuwa askari hao wanalenga zaidi magari ya mizigo hususani pick up ambayo yanachukua bidhaa za madukani kupeleka maeneo ambako kuna malori yanayosafirisha mizigo kwenda mikoani na nje ya nchi.

Uchunguzi umebaini kuwa katika kila gari wanalolisimamisha huanza kumtaka dereva aonyeshe leseni yake, awashe na kuzima gari, kukagua matairi na taa kama zinafanya kazi.

Katika ukaguzi huo ambao imezoeleka mara nyingi hufanywa na askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani, wakibaini gari lina kosa mojawapo humtoza dereva fedha kuanzia Sh. 50,000 na kuendelea bila kumpatia stakabadhi.

Aidha, askari hao wakishakamata magari mawili au matatu na kutoza madereva fedha, baadaye wanahama eneo hilo na kwenda eneo jingine na hufanya hivyo kuzunguka katika maeneo mengi ya Jiji la Dar es Salaam.

Kutokana na kiwango kikubwa cha fedha wanachotoza askari hao, wamiliki wa magari wamekuwa wakiwaogopa zaidi kuliko askari wa barabarani ambao kwa mujibu wa madereva wakikamatwa nao hutoa hata Sh. 2,000 na kuachiwa.

MSEMAJI POLISI
Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso, alisema wananchi wanapaswa kuwapongeza badala ya kuwalalamikia kwa sababu askari hao hawawezi kuona uhalifu halafu wasichukue hatua.

“Askari wanafanya kazi kama nyuki, wanapofanya kazi za kuzuia uhalifu, kuna sababu gani ya kuwalalamikia, tumeweka pikipiki sababu zinaweza kumfuata mhalifu kila mahali alipo,” alisema.

Alisema haiwezekani mfano mhalifu anafanya kosa la usalama barabarani halafu askari wa pikipiki asimkamate hadi aje trafiki.Senso alisema askari hao wa pikipiki waliwekwa nchi nzima na wanapopita mitaani wakiona mhalifu lazima wamchukulie hatua.

Wananchi wanachopaswa kujua kuwa askari hawezi kuona uhalifu unafanyika halafu mhalifu anachwa kusubiri askari anayehusika ndiye aje amkamate.

“Mbona raia tunamhimiza akiona mhalifu atoe taarifa polisi, mbona hatusemi ukimuona mhalifu wa barabarani usitoe taarifa isipokuwa kwa ujambazi tu, hicho kitu hakipo,” alisema.

Alisema kimsingi, watenda makosa wana tabia ya kulalamika kwa lengo la kudhoofisha utendaji kazi wa Jeshi la polisi.

KAMANDA TRAFIKI ANENA
Hata hivyo, kauli ya Senso inatofautiana na kauli ya Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga, ambaye hivi karibuni aliwaonya polisi wa pikipiki kuwa jukumu lao ni kudhibiti ujambazi na siyo kuwavizia madereva wa bodaboda na bajaj barabarani.

“Askari wa Tigo wanawajibika kwa Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, walikabidhiwa pikipiki hizo kwa maelekezo ya kudhibiti ujambazi,” alisema na kuongeza: “Kuwavizia bodaboda na bajaj ni makosa,” alionya Kamanda Mpinga.

Aliwataka polisi hao kuzingatia maadili ya kazi hasa pale wanapowakamata watumiaji wa vyombo vya moto.Mpinga alisema ingawa askari yeyote ana mamlaka ya kumkamata mhalifu, lakini lazima wazingatie maadili ya kazi zao na sheria za jeshi hilo.

Alisema iwapo askari wa ‘Tigo’ wamewakamata waendesha bajaj na bodaboda, wanatakiwa kuwafikisha kituoni na kuwatoza faini kulingana na makosa yao na kuwapatia stakabadhi halisi.

Kamanda Mpinga alisema kuwatoza wananchi fedha bila kuwapatia stakabadhi kwa makosa waliyofanya ni kosa kisheria, hivyo lazima wanaofanyiwa hivyo wawaone viongozi na kuwasilisha malalamiko yao.

Kitengo cha askari wa pikipiki kilianzishwa baada ya kuibuka kwa wimbi kubwa la ujambazi nchini ambalo lilenga zaidi kuvamia na kuiba kwenye benki.

Mkoa wa Dar es Salaam ulikuwa unaongoza kwa matukio hayo ndiyo maana pikipiki hizi zilianzia huku kabla ya kupelekwa kwenye mikoa mingine kwa nia ya kukabiliana na ujambazi.

Hata hivyo, pamoja na kuwekwa kwa askari hao, bado matukio ya uporaji katika maeneo kadhaa ya katikati ya jiji na mengine bado yanaendelea kwa kasi huku wahusika wakishindwa kukamatwa.
CHANZO: NIPASHE

No comments: