Advertisements

Thursday, July 24, 2014

Simba kumrudisha Okwi

Dar es Salaam. Wakati Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) likisogeza muda wa usajili, Yanga inahaha kufanya uamuzi wa kuondoa mmoja kati ya wachezaji wawili Waganda, huku Simba ikikaribia kumalizana na beki kutoka Lipuli na kumrejesha Emmanuel Okwi.
Tayari Simba imemalizana na beki huyo wa kati wa Lipuli, Joram Mgeveke, ambaye yupo katika kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, baada ya kumpa mkataba wa miaka miwili jana.
Beki huyo alishaweka kibindoni Sh8 milioni za usajili za awali, huku klabu yake ya Lipuli ikivuna Sh20 milioni baada ya kukubali kumuuza.
Licha ya usumbufu wa mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Okwi, miamba hiyo ya Msimbazi pia inasuka mipango ya kumrudisha mshambuliaji huyo Mganda kutoka Yanga.
Habari za uhakika kutoka ndani ya klabu ya Simba zinadai kuwa uongozi umeshaanza mazungumzo na mshambuliaji huyo, ambaye aliikacha Yanga kabla ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu kumalizika.
“Tunafanya mchakato wa kumrudisha Okwi. Ni msumbufu lakini tunaamini atatusaidia kuimarisha kikosi chetu, msimu ujao,” alisema kiongozi huyo ambaye aliomba jina lake lisitajwe.
Yanga bado haijaamua iache mchezaji gani kati ya Okwi na Hamisi Kiiza baada kuwa na wachezaji sita wa kigeni. Kanuni zinataka klabu zisajili si zaidi ya wachezaji watano wa kigeni.
Hata hivyo, kuna uwezekano mkubwa klabu hiyo itamuachia Okwi, ambaye katika kipindi cha miaka mitatu amechezea klabu nne za nchi nne tofauti.
Yanga imejikuta kwenye hali hiyo baada ya kusajili Wabrazili wawili, kiungo Andrey Coutinho na mshambuliaji Geilson Santos Santana ‘Jaja’.
Tayari timu hiyo ina wachezaji wageni wanne ambao ni Kiiza (Uganda), Haruna Niyonzima (Rwanda), Okwi (Uganda) na Mbuyu Twite (Rwanda)
Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji alishaweka wazi msimamo wake wa kuwasajili wachezaji bora zaidi kuliko Okwi na tayari Wabrazili wamemwaga wino wa miaka miwili kila mmoja.
Hata hivyo, ofisa habari wa Yanga, Baraka Kizuguto alipoulizwa kuhusu suala la Okwi, alisema: “Hatuvunji mkataba wa Okwi.”
MWANANCHI

No comments: