ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, July 1, 2014

Ukawa wabisha hodi kwa Msajili

Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), umekutana na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, na kumweleza msimamo wao wa kutorejea ndani ya Bunge Maalum la Katiba hadi mapendekezo yaliyopo kwenye Rasimu ya Katiba yatakapoheshimiwa.

Msimamo huo ulitolewa na Mwenyekiti wa Ukawa, Freeman Mbowe, alipokutana jana na kujadiliana na Msajili, Jaji Francis Mutungi.

Katika mkutano huo wa faragha, Mbowe alimueleza Jaji Mutungi kuwa wajumbe wa Ukawa waliosusia bunge hilo Aprili 16, mwaka huu hawatarejea wakati Bunge la Katiba litakapoanza awamu ya pili Agosti 5, mwaka huu hadi hapo Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na Tume ya Jaji Joseph Warioba itakapojadiliwa kama ilivyo.

Mbowe hakuwa tayari kuzungumza na vyombo vya habari baada ya mazungumzo hayo yaliyofanyika ofisini mwa msajili, lakini alielekeza aulizwe Afisa Habari wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tumaini Makene, ambaye aliongozana naye.

“Siwezi kuzungumza lolote juu ya tuliyozungumza baina yangu na Msajili, yote muulizeni Makene,” alisisitiza Mbowe pale alipotakiwa kueleza kiini cha mazungumzo hayo.

Makene alithibitisha kufanyika kwa mazungumzo hayo na kusema kuwa kikao hicho kilitokana na kuitikia wito wa Msajili kukutana na Kiongozi wa Ukawa, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema Taifa.

Makene alisema kikao hicho kimetokana na ombi la Msajili wa Vyama vya Siasa kukutana na Kiongozi wa Ukawa, kujadili mustakabali wa Ukawa kurudi bungeni na mchakato wa Katiba.

Alisema pamoja na mambo mengine, Ukawa ilisisitiza msimamo wake mbele ya msajili huyo kuwa hawatarejea Bungeni hadi maoni ya wananchi yatakapoheshimiwa na kuwapo kwa maridhiano baina ya pande zinazovutana.

“Iwapo maoni ya wananchi yatawekwa mbele na maridhiano kupatikana, tutakuwa tayari kurejea, lakini kwa sasa hatuko tayari kwa namna yoyote ile,” alisema Makene.

Naibu Msajili, Sisty Nyahoza, alithibitisha kufanyika kwa mazungumzo hayo wakati akizungumza na NIPASHE ofisini kwake.

Alisema kikao hicho ni cha kawaida kama vikao vingine kwa msajili kushauriana na vyama vya siasa kwa jambo lolote.

Nyahoza alithibitisha kuwa Ukawa walisisitiza na kuweka wazi msimamo wa kutorejea Bungeni mbele ya Msajili.

“Ni kweli msimamo wao ni huo hawatarejea na walisema hivyo hivi karibuni katika mkutano mkuu wa Chama cha wananchi (CUF),” alisema.

Ukawa walitoka bungeni Aprili 16, mwaka huu, na hadi Bunge hilo linaahirishwa Aprili 25, mwaka huu, walikuwa nje ya bunge.

Bunge hilo limeongezewa siku 60 baada ya siku 70 za awamu ya kwanza kumalizika likiwa limejadili sura mbili tu za rasimu.

Mei 1, mwaka huu, Rais Jakaya Kikwete alisema ikiwa siku 60 za nyongeza zitamalizika bila mchakato huo kumalizika, hakutakuwa na siku za nyongeza.

Sura ya kwanza inayohusu jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na sura ya sita inayozungumzia muundo wa Muungano ndizo zilizozua mvutano baina ya Ukawa na wajumbe wengine wengi wao kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Ukawa wanataka jina la shirikisho na serikali tatu wakati wajumbe wengine wanaoongozwa na CCM wakitaka jina la Jamhuri ya Muungano liendelee sambamba na muundo wa serikali mbili.

Hali hiyo ndiyo iliwalazimu wajumbe wa Ukawa kususia wakidai kuwa kuna mbinu za kuchakachua Rasimu ya jaji Warioba.

Viongozi mbalimbali wa kitaifa wamekuwa wakitoa kauli za kuwasihi Ukawa warejee bungeni lakini wamekataa na kuweka masharti kwamba watarejea ikiwa itajadiliwa Rasimu ya Warioba yenye maoni ya wananchi.
CHANZO: NIPASHE

No comments: