Advertisements

Friday, August 22, 2014

Ajira za upendeleo 228 Uhamiaji zafutwa

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi,Mbarak Abdulwakil.

Serikali imesitisha ajira za konstebo na koplo 228 walioajiriwa na Idara ya Uhamiaji hivi karibuni, baada ya kamati ya kuchunguza malalamiko ya wananchi kubaini kuwa zilitolewa kwa upendeleo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mbarak Abdulwakil, alisema kamati hiyo iliyofanya uchunguzi kwa siku 10, kuanzia Agosti Mosi, mwaka huu, imebaini upendeleo ulitumika katika mchakato wa ajira za watumishi wa ngazi hizo.

Alisema katika uchunguzi huo, baadhi ya wasailiwa waliolalamikiwa wamethibika kuwa ni watoto, ndugu au jamaa za watumishi wa idara hiyo kwa asilimia 100.

Aliyataja mengine, ambayo kamati hiyo ilibaini kuwa ni baadhi ya waombaji kuwa na umri mkubwa zaidi ya miaka 30 kusailiwa, waliopata alama za juu kutosailiwa na matangazo yaliyotolewa kuwa ya jumla.


“Baada ya kutafakari matokeo hayo, wizara imeona ajira za konstebo na koplo zifutwe na kutangazwa upya chini ya wizara, ikiwa ni pamoja na ajira 28 za Zanzibar,” alisema Abdulwakil.

Kamati hiyo iliundwa na Katibu Mkuu huyo Julai 31, mwaka huu, ili kuchunguza ajira hizo mpya baada ya kuwapo malalamiko mengi kutoka kwa wananchi.

Malalamiko hayo yalifuatia usaili uliowajumuisha waombaji zaidi ya 10,000 walioomba kazi katika idara hiyo.Usaili huo ulifanyika Juni 13, mwaka huu, katika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, waombaji wakikalishwa kwenye viti vya watazamaji mpira.

Katika tangazo la ajira, jumla ya maombi 15,707 yalipokelewa na idara hiyo, waombaji 1,005 waliitwa kwenye usaili na 200 walishinda na kuitwa kazini.

Pia alisema serikali inatambua kuwa idara hiyo inakabiliwa na uhaba wa watumishi, hivyo hatua za haraka zitachukuliwa ili kutoa huduma kwa wananchi.

Katika usaili huo wasailiwa wengi wakilalamikia mazingira ya mtihani huo kujaa rushwa na udanganyifu.Walieleza kuwa baada ya kufika uwanjani hapo, walipewa mtihani bila kuhojiwa kama ndiye mhusika halali au la na hawakuulizwa majina wala vitambulisho.

Baadhi yao walisema walikuwa na wakati mgumu baada ya kuingia uwanjani na kupewa mtihani huo wa maswali ya kujaza wakati wengine hawakuwa hata na kalamu.

“Tulijua tumekwenda katika viwanja hivyo kwa ajili ya kufanyishwa mazoezi na idara hiyo, ikiwa ni sehemu ya mtihani huo,” alisema mmoja wa waomba kazi.

Akizungumza na NIPASHE kwa masharti ya kutotajwa jina, mhusika mwingine alieleza kushangazwa na mtihani huo usiokuwa na maandalizi na usalama.

Alisema kuna uwezekano wa wengine kufanyiwa mitihani kwa vile hapakuwapo na ukaguzi wala uhakiki wa aina yoyote.Pia alisema wameshangazwa na kuwapo kwa idadi kubwa ya watu katika mtihani huo wakati wanaotakiwa ni 70 pekee.

“Kuna uwezekano wametuzuga ili tuonekane tumefanyiwa usaili kumbe tayari wameshapata majina ya watoto wa vigogo wanaopewa ajira hiyo,” alisema na kuwasikitikia wale waliotoka mikoani.

Wengine walilalamika kuwa walifanyia mitihani mapajani, kwani hakukuwa na meza uwanjani.

Aliongeza: “Kuna wengine hawakuwa na taarifa sahihi za mtihani huo, ndiyo maana wengine walijikuta wakitafuta peni wakati wenzao wakiendelea na mtihani.

Magreth Sanga akizungumzia mtihani, alisema ulifanyika vizuri, lakini changamoto iliyojitokeza katika zoezi hilo ni ukosefu wa uhakiki, hasa ukaguzi wa vitambulisho, hali ambayo iliwapa wasiwasi huenda pakawapo na watu walioingia bila ya kuwa wahusika.

Mwingine, ambaye hakutaka jina lake litajwe akihofia huenda atakatwa jina lake katika mtihani huo, alisema katika hali isiyo ya kawaida, mazingira yanaonyesha huenda pakawa na rushwa katika kupata kazi.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: