Advertisements

Friday, August 22, 2014

Baregu:Najuta

Aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Prof. Mwesiga Baregu

Aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Prof. Mwesiga Baregu, amejutia uamuzi wake wa kuendelea kuwa mjumbe wa Tume hiyo licha ya ushauri aliopewa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wa kujitoa.

Prof. Baregu ambaye ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (Saut) na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, amesema maamuzi yaliyotolewa na Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya kubariki Bunge Maalum la Katiba liendelee kujadili Rasimu ya Katiba mpya bila kupatikana maridhiano kwanza, ni mbinu za chama tawala kutokuwa na nia ya kulipatia Taifa Katiba yenye maslahi ya wananchi.

Aprili 6, mwaka 2012, Rais Jakaya Kikwete aliteua watu 30 kuwa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba akiwamo Prof. Baregu.


Tume hiyo pamoja na majukumu mengine, ndiyo iliyokwenda katika maeneo mbalimbali ya nchi kukusanya maoni ya wananchi kuhusu mambo waliyotaka yawekwe kwenye Katiba mpya.

Awali kulikuwapo na taarifa kwamba baadhi ya viongozi wa Chadema walimtaka Prof. Baregu kujitoa katika Tume hiyo ifikapo Aprili 30, mwaka 2012 kutokana na chama hicho kikuu cha upinzani nchini kuelezea hofu yake kutokana na mchakato wa Katiba wakati ule ulivyokuwa unakwenda.

Hata hivyo, Prof. Baregu alisimamia msimamo wake, akisema kuwa ni haki yake na ataendelea kutekeleza jukumu la kulipatia Taifa Katiba bora kwa kuwa kwake Tanzania ni ya kwanza na mengine yanafuata.

Akizungumza na NIPASHE jana, Prof. Baregu, aliliomba radhi taifa yeye binafsi na kwa niaba ya wenzake 30 waliokuwa kwenye Tume hiyo, ambao kati yao hiyo 15 kutoka Tanzania Bara na 15 Zanzibar.

Alisema hawanabudi kuomba radhi kwa kutekeleza mchakato wakiamini ni wenye lengo la kupatia Taifa Katiba mpya, kumbe walilaghaiwa wakatumika kuitumikia CCM kutafuta Katiba yake.

“Niligoma kujitoa kwenye Tume nilipotakiwa kufanya hivyo na chama changu (Chadema), nikiamini mchakato ulikuwa kwa maslahi ya taifa, kumbe tulilaghaiwa na sasa binafsi nimeamini Katiba inayotafutwa ni ya CCM na siyo ya Tanzania,” alisema Prof. Baregu.

Prof. Baregu alisema uamuzi wa CCM wa kubariki Bunge Maalum la Katiba liendelee siyo wa busara wala hekima bali umegubikwa na mihemko ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwakani.

Kwa mujibu wa Prof. Baregu, kinachoelezwa na chama tawala kuwa kuna maendeleo mazuri katika mchakato wa Katiba, ni kuondoa mambo yote yaliyo kwenye Rasimu ya pili, ambayo yalilenga kudhibiti nidhamu, uwajibikaji na utumishi bora kwa umma.

“Mgawanyo wa majimbo, ukomo wa mtu kugombea ubunge, miiko na maadili ya watumishi wa umma na mawaziri kutotokana na wabunge, vyote hivyo wanaviondoa kwenye rasimu wanataka kuunda utumishi au uongozi wa aina gani kama siyo unafiki?” alihoji Prof. Baregu na kuongeza:
“Hatunabudi kuomba radhi Watanzania tuliowaahidi kuwaletea Katiba Mpya.”

Alisema mpango huo una nia ya kufanikisha malengo ya muda mfupi na kuweka kando malengo ya taifa ya muda mrefu na kwamba unahatarisha usalama wa nchi kwani inaweza kuingia katika machafuko.

Kadhalika, alisema agizo la Kamati Kuu ya CCM kwa Katibu Mkuu wake, Abdulrahman Kinana, la kuendeleza usuluhishi kati ya makundi ya waliobaki bungeni na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ni unafiki.

Alisisitiza kuwa hata kama Ukawa wangeamua kurejea bungeni, ingemaanisha ni kuridhia mambo ambayo hawakushiriki kuyaamua.

DK. SLAA ANENA
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, amesema kimsingi maamuzi yaliyotolewa na Kamati Kuu ya CCM hayana ushawishi wa kuwagawa Ukawa bali yanaviimarisha.

“Turuhusu hayo majadiliano yafike mwisho ambayo Kinana (Katibu Mkuu wa CCM) ameagizwa na Kamati Kuu chini ya Rais Kikwete kwamba akutane na vyama na wadau wengine ili kupata muafaka kwa sababu hata hivyo, ukilitazama tamko lao haliko committed (uwajibikaji) kwa upande wowote…

Naamini CCM haijafikia hali ya kukosa busara kiasi kwamba wakamwacha Samuel Sitta aendelee na Bunge lisilo na uhalali wa kisiasa,” alisema Dk. Slaa.

MHADHIRI WA RUCo
Mhadhiri Mwandamizi wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Ruaha-Iringa, Rwezaura Kaijage, alisema uamuzi uliofanywa na CCM kubariki Bunge Maalum la Katiba kuendelea bila maridhiano, hauna tofauti na ubabe uliowahi kufanywa na baadhi ya viongozi wa Afrika wanaokumbukwa kwa ubabe wa kunyonga demokrasia.

“Huu ni ubabe ambao kimsingi hauna tofauti na wale viongozi wa Afrika wanaokumbukwa kwa kunyonga demokrasia, tusipoutazama kwa umakini zaidi uamuzi huo wa CCM hatutapata Katiba ya Watanzania ila tutapata Katiba ya CCM,” alisema Kaijage.

LHRC
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Hellen Kijo-Bisimba, alisema pamoja na maamuzi ya Kamati Kuu ya CCM, mwenendo wa Bunge Maalum la Katiba unaashiria kuwa Katiba yenye maslahi ya taifa haitapatikana.

Alisema watu wengi walijua tangu mapema kuwa Bunge Maalum linaloendelea halitakuwa na jipya kutokana na wajumbe kuweka mbele maslahi yao badala ya maslahi ya wananchi.

Dk. Bisimba alisema Bunge Maalum la Katiba, linahitaji watu kuelewana ili kujadili na kukubaliana mambo ya msingi na kuunda Katiba yenye maslahi kwa Taifa.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: