Dodoma. Mjumbe wa Bunge Maalumu, Said Arfi amesema anakusudia kwenda mahakamani kupata ufafanuzi wa uhalali wa Bunge hilo kuachana na Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba na badala yake kufanya kile alichokiita kuandika rasimu nyingine.
Katika taarifa yake jana, Arfi alisema hatua yake ya kwenda mahakamani inatokana na ukweli kwamba baada ya Bunge Maalumu kukataa muundo wa serikali tatu uliopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, haiwezekani tena kujadili Rasimu ya Tume.
“Badala yake kinachofanyika kwa sasa ni kuandika rasimu nyingine ili iendane na muundo wa serikali mbili ambao ndiyo Chama cha Mapinduzi wanaoutaka,” alisema na kuongeza kuwa kinachofanyika sasa katika kamati ni mabadiliko makubwa ya Katiba ya sasa na siyo uandishi wa Katiba Mpya.
“Kimsingi, baada ya wabunge wanaotokana na vyama vinavyounda Ukawa kuondoka, ni kama sasa nyani amekabidhiwa shamba la mahindi lisilo na mlinzi. Kwa hali inavyokwenda kinachofanyika siyo kutengeneza Katiba Mpya, bali kufanya marekebisho makubwa katika katiba iliyopo,” alisema Arfi.
Alisema tayari amewasiliana na mawakili wake na kwamba mchakato wa kufungua kesi hiyo kwa hati ya dharura uko katika hatua za mwisho.
Arfi akiwa ni mbunge pekee wa Chadema ambaye amehudhuria vikao vya Bunge la Katiba baada ya chama chake kususia, alisema anakwenda kupinga kuendelea kwa Bunge hilo kwa sababu kinachoendelea kwa sasa ni kujadiliwa kwa rasimu ya CCM badala ya ile iliyowasilishwa na Tume ya Jaji Joseph Warioba.
Hatua ya Arfi imekuja wakati tayari imeshafunguliwa kesi kama hiyo katika Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam ikitaka tafsiri sahihi ya mamlaka ya Bunge la Katiba chini ya Vifungu vya 25 (1) na 25(2) vya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Namba 83 ya mwaka 2011.
Kesi hiyo imefunguliwa Ijumaa iliyopita na Mwandishi wa Habari, Saed Kubenea, kupitia kwa wakili wake, Peter Kibatala dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na kuwasilisha maombi ya kuitaka itoe zuio la muda la kusimamisha Bunge hilo ili kusubiri uamuzi wa kesi ya msingi.
Akizungumzia kesi hiyo iliyofunguliwa na Kubenea, Arfi alisema naye amesikia na kwamba atashauriana na mawakili wake ili kuona namna ya kufanya.
“Sifahamu kisheria kama kile ninachokusudia mimi kukipata ndicho kilichokusudiwa katika kesi ya Kubenea, kwa hiyo nitasikiliza ushauri wa mawakili wangu ili kuona kama tuendelee au vinginevyo,” alisema Arfi.
Msimamo wake
Katika taarifa yake, Arfi ambaye pia ni Mbunge wa Mpanda Mjini (Chadema) alitetea msimamo wake wa kurejea bungeni, tofauti na wajumbe wenzake ambao ni wanachama wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Alisema mambo yanayofanyika hivi sasa yamewezekana kwa sababu Ukawa wamesusa na kwamba: “Tungekuwepo wote ndani ya Bunge hili lisingewezekana kwa sababu tungepinga kwa nguvu zaidi na hata kuhakikisha Bunge haliendelei.”
Aliongeza: “Wenzetu wa kundi la 201 wanaangalia zaidi masilahi ya makundi yao na wananchi kwa jumla na muundo wa serikali kwao si jambo linalowashughulisha sana.”
Alisema baadhi ya mambo yamefanywa ili kujaribu kuwashawishi Wazanzibari kuendelea kuwa sehemu ya muungano wa serikali mbili ambayo ni pamoja na kuwepo kwa makamu watatu wa rais na kuanzishwa kwa mfumo wa mabunge matatu.
“Kimsingi tunarudi kulekule walikopendekeza tume kwa sababu ukichambua pendekezo hili unakutana na serikali tatu ambazo Tume imependekeza… huwezi kuwa na Bunge la Tanganyika bila kuwa na Serikali kwa sababu kazi kubwa ya Bunge ni pamoja na kuisimamia Serikali,” alisema Arfi.
Alisema pamoja na hayo yote kuna mambo mazuri ambayo yameingizwa kwenye rasimu hiyo zikiwamo haki za wakulima, wafugaji na wavuvi kumiliki ardhi, haki ya afya, chakula, maji safi na salama na hifadhi ya jamii na makazi.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment