Advertisements

Wednesday, August 27, 2014

Ebola imetua DRC, sisi tumejipanga vipi?

Habari za kuzuka kwa ugonjwa hatari wa ebola katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) ni za kutia hofu. Serikali ya DRC imesema watu wawili walioambukizwa virusi vya ugonjwa huo kaskazini mwa nchi hiyo wamefariki dunia, huku kukianza kujitokeza wasiwasi mkubwa kwa nchi zilizoko katika eneo la Afrika Mashariki kuhusu uwezekano wa kukumbwa na ugonjwa huo ambao mpaka sasa hauna chanjo wala tiba.
Ni habari ambazo bila shaka zimepokewa kwa mfadhaiko mkubwa na serikali zote zilizo katika ukanda huo kutokana na ukweli kuwa, hadi kufikia juzi ugonjwa huo uliozuka mwezi uliopita ulikuwa umeua watu 1,427 katika nchi za Guinea, Sierra Leone, Liberia na Nigeria.
Hivyo, DRC inakuwa nchi ya tano barani Afrika kukumbwa na ugonjwa huo, ingawa nchi hiyo kwa mara ya kwanza ilikumbwa na ugonjwa huo mwaka 1976 kabla ya kuingia Uganda mwaka 2012. Serikali ya DRC imesema huo ni mlipuko wa saba wa homa ya ebola kuwahi kuikumba nchi hiyo na kwamba uzoefu walioupata katika milipuko sita iliyopita, utatumika kukabiliana na maambukizo ya homa hiyo.
Hata hivyo, hofu imetanda katika ukanda mzima wa Afrika Mashariki siyo tu kutokana na milipuko ya mara kwa mara katika DRC, bali pia ugonjwa huo kuenea kwa kasi kubwa ambayo hata Shirika la Afya Duniani (WHO), limekiri kwamba ni vigumu kuidhibiti kama ilivyotokea katika nchi hizo nne za Afrika Magharibi.
Kama ugonjwa huo umetua katika nchi hiyo jirani, basi Serikali ya Tanzania sasa haina budi kujipanga upya kwa kuchukua hatua madhubuti, ikiwa ni pamoja na kufanya uamuzi mgumu ili ugonjwa huo usiingie nchini. Hakuna asiyejua kwamba kuna mwingiliano mkubwa wa watu kati ya nchi hizi mbili, kwani wafanyabiashara wengi kutoka DRC wanakuja nchini kununua bidhaa mbalimbali na kuzipeleka makwao. Kuna haja ya kudhibiti mwingiliano huo na ikibidi Serikali isione aibu kufunga mpaka au kuweka karantini.
Kenya, Zambia na nchi nyingine kadhaa zimefanya uamuzi mgumu wa kupiga marufuku ndege zinazotoka katika nchi zilizokumbwa na ugonjwa huo, ingawa hatua hiyo imezikasirisha nchi hizo. Serikali ya Tanzania nayo lazima itambue kwamba jukumu lake la kwanza ni kulinda usalama wa raia na mali zao, hata kama kufanya hivyo kutawakasirisha baadhi ya watu.
Nchi nyingi za Afrika zimeonyesha kutokuwa na uvumilivu wala simile katika kuhakikisha ugonjwa huo hauingii katika nchi zao. Nchi hizo zimeweka mkakati wa pamoja kuhakikisha zinadhibiti ugonjwa huo.
WHO imesema mlipuko wa sasa wa ugonjwa huo ni wa kihistoria kutokana na kasi ya kuenea na idadi ya watu waliopoteza maisha.
Ni katika misingi hiyo tunaitaka Serikali kujipanga upya kulidhibiti ‘joka’ hili ambalo limeingia katika nyumba ya jirani kabla halijatuvamia na kutuangamiza. Tunatambua hatua ambazo Serikali ilikuwa imeanza kuzichukua katika kudhibiti ugonjwa huo wakati ulipoibuka Afrika Magharibi mwezi uliopita. Hata hivyo, kwa kuwa ugonjwa huo sasa upo jirani, Serikali haina budi kuongeza kasi ya kuudhibiti ili kupunguza uwezekano wa ugonjwa huo kujipenyeza katika nchi yetu.
Tunarudia kuishauri Serikali kwamba isisite wala kuona haya kufanya uamuzi mgumu katika kufanikisha juhudi za kudhibiti ugonjwa huo.
Mwananchi

No comments: