Advertisements

Wednesday, August 20, 2014

Habari kamili ya Mabasi yagongana, yaua zaidi ya watu 16

Wananchi wakiangalia mabasi mawili yaliyogongana uso kwa uso eneo la Mkolye, nje ya mji wa Sikonge, mkoani Tabora jana, iliyohusisha basi la Sabena toka Mbeya kwenda Mwanza na basi la A.M. toka Tabora kwenda Katavi. Na Mpigapicha Wetu

Tabora.Zaidi ya watu 16 wamefariki dunia baada ya mabasi mawili kugongana uso kwa uso jana saa 9:30 alasiri umbali wa kilomita tatu kutoka Sikonge.
Basi la Sabena likitokea Mbeya kwenda Tabora liligongana uso kwa uso na jingine la AM Coach lililokuwa likitoka Tabora kwenda Mbeya.
Miongoni mwa waliofariki dunia, ni dereva wa Sabena aliyefahamika kwa jina moja la James ambaye kichwa chake kilitengana na kiwiliwili na hadi jana jioni kilikuwa kikitafutwa katika eneo la ajali.
Dereva wa AM Coach alikuwa amekwama kwa zaidi ya saa mbili ndani ya basi hilo na hadi tunakwenda mitamboni, jitihada za kumtoa kwa kukata basi zilikuwa zikiendelea.
Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Sikonge, Dk John Buswelu alisema hadi jana saa 12:30, walikuwa wamepokea maiti 16 kutokana na ajali hiyo na majeruhi 75 kati yao wanaume 45 na wanawake 30.
Inasemekana kuwa idadi ya waliofariki ni kubwa kutokana na mabasi hayo kung’ang’aniana na Sabena likiwa limeharibika zaidi kwa kupondeka karibu nusu yake.
Majeruhi wengi walikuwa wamevunjika viungo mbalimbali ambavyo baadhi vilionekana vikiwa vinatolewa kwenye mabasi hayo.
Mmoja wa abiria aliyenusurika kwenye ajali hiyo, Nuru Mtafya aliyekuwa amepanda Sabena kutoka Mbeya akielekea Shinyanga, alisema:
“Tulikuwa tumeongozana na basi la Sasebosa na kulikuwa na vumbi jingi, hivyo dereva wa AM alishindwa kuliona basi letu.”
Abiria mwingine Ally Hamis, alisema alikuwa ameanza kusinzia baada ya kutoka Sikonge na kuamshwa na kishindo kikubwa na vilio vya watu... “Ninachoweza kusema nimepona kutokana na kukaa nyuma kabisa ya basi, vinginevyo nisingetoka mzima.”
Mwananchi

No comments: