
Dar es Salaam. Uongozi wa Klabu ya Simba umeingia katika mgogoro wa kisheria na wachezaji wake 10 baada ya kuvunja mikataba yao na kuwapa barua ili wasajiliwe na timu nyingine msimu ujao.
Uamuzi huo umesababisha baadhi ya wachezaji kugoma kuchukua barua hizo kwa madai kuwa hazijaeleza fedha watakazolipwa kutokana na mikataba yao kusitishwa. Ni mchezaji mmoja tu ndiye aliyechukua barua hiyo, Edward Christopher aliyesajiliwa na Klabu ya Polisi Morogoro iliyopanda daraja msimu huu.
Wachezaji walioachwa ni Edward Christopher, Betram Mwombeki, Zahoro Pazi, Haruna Shamte, Abdulhaman Humud, ambaye kwa sasa anachezea Sofapaka ya Kenya, Gilbert Kaze, Abuu Hashim, Ramadhan Chombo ‘Redondo’, Ally Badru na Hassan Khatib.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wachezaji hao walisema wamefikia uamuzi wa kugomea barua kwa sababu hazielezi kama watalipwa fedha baada ya mikataba yao kuvunjwa.
Mwombeki, ambaye ni mshambuliaji alisema: “Sijaelewa kinachoendelea hadi sasa, sijapewa barua yangu na inaonekana wazi wanataka nirudi kuicheza Simba jambo ambalo sikubaliani nalo na hata nikirudi, basi nitatoa masharti yangu.”
Kwa upande wake Zahoro Pazi alisema: “Nimeambiwa barua ipo tayari, lakini haina malipo... nitakwenda kuchukua ingawa hadi sasa bado naidai Simba mishahara ya miezi minne.”
Naye Christopher alisema: “Wamevunja mkataba wangu bila malipo kwa madai sikuitumikia Simba, lakini nadai mshahara wa miezi mitano na fedha za usajili.
“Kama mtu hakuhitaji bora akuambie mapema utafute maisha sehemu nyingine, lakini sijui walikuwa na lengo gani na sisi, maana barua wanatukabidhi siku ya mwisho ya usajili, hawajafanya kitu kizuri,” alisema.
Akizungumzia suala hilo kuvunja mikataba ya wachezaji, makamu rais wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ alikiri klabu hiyo kudaiwa na wachezaji hao na kwamba wamevunja mkataba kwa makubaliano maalumu na wanajipanga kuwalipa.
“Kwa sasa tunajipanga, kuanzia wiki ijayo tutaanza kuwalipa malimbikizo ya mishahara yao kulingana na mikataba yao,” alisema Kaburu. “Nawashangaa Christopher na wenzake, walipewa nafasi ya kucheza soka wakashindwa kuitumia, walilewa sifa wakajisahau kwenye mkataba kuna kipengele kinasema ukishuka kiwango unapelekwa timu yoyote kwa mkopo ili urudishe kiwango, wao hawataki kwa kuwasaidia tumewapa barua ya kuwaruhusu kuwa wachezaji huru.”
Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura akizungumzia suala hilo, alisema wachezaji wengi wanaingia mikataba ‘kichwa kichwa’.
“Wanatakiwa kujitambua na kutafuta wanasheria wataowasaidia kuwatafsiria vipengele vya mikataba yao na kuhakikisha wanabaki na nakala pale wanaposaini mikataba,” alisema.
Imeandaliwa na Mwanahiba Richard, Oliver Albert na Vicky Kimaro.
mwananchi
No comments:
Post a Comment