ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, August 28, 2014

Halima Mdee atoka machozi


Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (kushoto) akifuta machozi huku akiwa ameshika fomu za kuwania nafasi ya Uenyekiti wa Bazara la Wanawake wa Chadema (Bawacha) alizokabidhiwa na baadhi ya wanakwake makao makuu ya Chama hicho jijini Dar es Salaam jana. Picha na Ibrahim Yamola

Mchakato wa uchaguzi ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) umeendelea kupamba moto, baada ya wanawake zaidi ya 30 wa Chadema mkoa wa Dar es Salaam na Pwani, kujitokeza kumchukulia fomu Mbunge wa Kawe, Halima Mdee ya kugombea uenyekiti wa Baraza la Wanawake wa chama hicho Taifa (Bawacha).

Wanawake hao ambao ni viongozi wa mabaraza ya Chadema kwa ngazi mbalimbali na wanachama wa chama hicho, walianza kuwasili nje ya ofisi za Baraza Chadema zilizopo Kinondoni jijini Dar es Salaam jana, kuanzia majira ya saa 4 asubuhi.

Wanawake hao ambao walitoka katika maeneo ya Kinondoni, Kawe, Kigamboni, Mbezi na Kibaha, walisema lengo la kufika katika ofisi hizo ni kumchukulia fomu Mdee ili agombee nafasi hiyo baada ya kumshawishi bila ya mafanikio.

NIPASHE lilishuhudia majira ya saa 6:15 mchana kundi la wanawake hao, wakiingia katika ofisi hizo na baada ya kujitambulisha kwa mfanyakazi wa mapokezi na kueleza sababu zao za kufika hapo.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Katibu Mwenezi wa Chadema Jimbo la Kawe, Felister Njau, alisema wao kama wanawake wa Chadema wameshauriana na kuona anayeweza kuwa mwenyekiti wa Bawacha bila kuyumbishwa na yeyote Mdee.


“Tumekuja hapa kama wanawake wa Chadema, tumeona mwenzetu Mdee anaweza kushika nafasi ya uenyekiti Taifa, kabla ya kuja kuchukua fomu, tulimshawishi alikataa akidai ana majukumu mengi, lakini hatujakubaliana na sababu hiyo, ndiyo maana tumejikusanya ili tumchukulie fomu,” alisema Njau.

Aliongeza kuwa kuchukua fomu hiyo kutaambatana na kumtafuta Mdee ili wamkabidhi, azijaze na kurudishwa kwenye ofisi hizo ili awanie nafasi hiyo.

“Mdee tunaona anafaa kuwa kiongozi kwani tangu amekuwa kiongozi, Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani, tunaujua utendaji wake ni shupavu asiyeyumbishwa na mawazo ya watu wengine, hivyo tunaamini anaweza kushika nyadhifa hii,” alisema.

Baada ya wanawake kukabidhiwa fomu hizo, waliongozana hadi ofisi za Chadema makao makuu, ambako walielezwa Mdee alikuwa akiendelea na shughuli za chama hicho.

Baada ya kufika katika ofisi za Chadema na kujisajili, waliingia na kukaa kikundi huku wakipanga namna ya kumuita Mdee na kumueleza jambo hilo.

Baada ya kushauriana, walipendekeza afuatwe na wanawake wenye umri mkubwa kuliko wao waliokuwa kwenye ofisi hizo akamwite na kumpokea kwa vifijo na nderemo kitendo ambacho kilizua taharuki kwake kwa sababu ya kutofahamu sababu za shamrashamra hizo zilizokuwa zimeambatana na kuimbiwa nyimbo za Chadema.

Baada ya kumpokea na kukaa, mmoja wa wanawake hao, alisimama na kumueleza lengo la kumuita huku akimkabidhi fomu hizo, akimtaka azijaze.

“Jamani subirini kwanza, subiri subiri, nashukuru kwa kuniamini kwanza nashangaa.. nilikuwa naenda kwenye ziara zangu kukutana na wananchi wangu na kuwakuta wengi hivi, najua mnaniamini na mmenipa nafasi hii lakini naona kama sitaweza kuimudu,” alisema Mdee huku akishikwa na kigugumizi na kutikisa kichwa kuashiria kukataa ombi lao.

Wanawake hao walipinga kauli hizo za Mdee na kumtaka mwanamke mwingine mwenye umri mkubwa iliyekuwa karibu naye ambaye alikuwa Mwalimu wa Mdee wa siasa, Alfredina Malingumu, amshawishi akubali kuwania nafasi hiyo.

“Mdee nimekufundisha nakujua uwezo wako wa kisiasa ona wanawake wote hapa tumeakuamini na kukupa nafasi wewe, tunaomba utusikie,hatutakuacha peke yako tuko nyuma yako ndiyo maana tumeona tukuchukulie fomu,” alisema Malingumu huku akimshika Mdee mabega.

Maneno hayo yalimfanya Mdee kuanza kububujikwa na machozi na kuwashukuru wanawake hao kwa kumuamini.

Akifuta machozi Mdee, alisema amepatwa na uchungu mwalimu wake huyo kumsihi kukubaliana nao kwa uchungu.

“Jamani nimesikia, nimewaelewa ila naomba nikatafakari suala hili kwa kina ndipo nitoe majibu ya uhakika kuhusiana na nafasi hii, najua mnaona nafaa ila ninaongozwa na Mungu hivyo ngoja nitafakari ndipo nitawajibu,” alisema Mdee. Pamoja na kumshawishi kuchukua fomu hiyo, wanawake hao walichanga na kumlipia fedha ya fomu hiyo Sh. 50,000.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa sasa wa Bawacha, Suzan Lyimo, alisema mpaka sasa waliorudisha fomu za kuwania nafasi mbalimbali ndani ya umoja huo ni wanachama 21.

Alisema zoezi hilo la kuchukua na kurudisha fomu linaendelea nchi nzima.

“Watu wengi wanachukua fomu na asilimia 90 ya wanaogombea nafasi mbalimbali ni wageni kabisa kwenye uongozi na wanawake wamejitokeza sana isipokuwa kwenye nafasi za walemavu ambazo mpaka sasa hakuna aliyejitokeza,” alisema Lyimo.

Alizitaja nafasi ambazo wagombea wamerudisha fomu kuwa mwenyekiti (wanne), makamu mwenyekiti (watatu), katibu (wawili), naibu katibu (wanne), wajumbe wa baraza (wanne) na wajumbe wa mkutano mkuu (sita).

Alisema idadi hiyo imejumuisha wagombea wa jijini Dar es Salaam pekee na kwa upande wa mikoani na Zanzibar, wanarudisha fomu katika ofisi za mabaraza na kuwasilishwa makao makuu kabla ya Jumamosi ijayo (keshokutwa).

Kuhusu kuendelea kutetea nafasi hiyo, Lyimo, alisema anafikiria kuwania nafasi nyingine na kuwaachia wengine.

“Nafasi ziko nyingi ndani ya chama za kugombea sioni kama kuna umuhimu wa kuendelea kushikilia nafasi hii, ila nitagombea kama sitaona anayeweza kushikilia nafasi hii vema,” alisisitiza.

NIPASHE lilishuhudia wanachama mbalimbali wa Chadema wakiwa katika ofisi hizo, wakirudisha fomu na wengine wakichukua kwa ajili ya kuwania nafasi mbalimbali.

Mmoja wa wanachama ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, alisema kuwa kwa sasa uchaguzi umekuwa ni tofauti kwa sababu wanachama wengi ambao hawakuwa viongozi kipindi kilichopita wamejitokeza hivyo hali hiyo inaoonyesha kutakuwa na mchuano mkali wakati wa uchaguzi.

WAZEE Z'BAR WAMTAKA MBOWE
Katika hatua nyingine, Wazee wa Chadema visiwani Zanzibar wamemtaka Mwenyekiti wa Chama hicho, Feeman Mbowe achukue fomu ya kutetea wadhifa huo.

Akizungumza na waandishi wa Habari visiwani hapa, Mwenyekiti wa Wazee hao wa Mjini Magharibi, Idrissa Jumbe, alisema wanachama wa mikoa mitatu ya Unguja wamechukua uamuzi huo wa kumtaka mwenyekiti huyo kugombea tena uenyekiti kwa sababu ndiye mpambanaji, amekijenga chama hicho na kukiletea maendeleo.

“Tunahitaji kiongozi mpambanaji ambaye anaweza kusimamia chama na taifa zima la Tanzania hivyo tumeona Mbowe anafaa”.
Alisema wanachama na viongozi wa Chadema wa Zanzibar, wanaamini kuwa Mbowe ndiye aliyekiwezesha chama hicho kupiga hatua ya kusimamia serikali.

Alisema mwenyekiti wao wamemwita Zanzibar na jana na wapo tayari kumlipia fomu ya kugombea nafasi hiyo.
Uchaguzi ndani ya chama hicho unatarajiwa kufanyika kuanzia Septemba 9 hadi 13, mwaka huu baada ya wagombea kurejesha fomu Agosti 30, mwaka huu.
CHANZO: NIPASHE

No comments: