Advertisements

Thursday, August 28, 2014

Shule inayoteswa na surua yafungwa

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk.Shukuru Kawambwa.

Siku moja baada ya NIPASHE kuripoti taarifa ya mlipuko wa surua Katika kijiji cha Mkoma 1, Kata ya Mnekachi, wilayani Newala, mkoani Mtwara, serikali imeifunga kwa wiki moja.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Awadhi Mkanapate, alisema shule hiyo ilifungwa baada ya Afisa Elimu wa wilaya hiyo kufika shuleni hapo na kuamuru kuifunga ili kuzuia maambukizi.

“Hali ni mbaya, maambukizi yanazidi kuongezeka, jana (Jumatatu) asubuhi watoto 17 waliongezeka, lakini mpaka jana (juzi) jioni watoto 33 walikuwa wameambukizwa, pamoja na mwalimu mmoja wa afya, Mwanahamisi Madidi. Kufuatia hali hiyo alikuja afisa elimu wa wilaya na kuamuru shule ifungwe ili kuzuia maambukizi,” alisema, Mkanapate.

Kwa mujibu wa Mkanapate, maambukizi hayo yanaendelea kuenea shuleni hapo kutokana na upungufu wa dawa.

“Jana (juzi) jioni nilikuwa na Mkunga Muuguzi wa Zahanati yetu akaniambia kuwa wameletewa Vitamini A, dawa ya macho na panadol, sasa mimi najiuliza hivi kweli hizi ni dawa za surua, nini hatma yetu kama dawa hazitapatikana?” alihoji Mkanapate.

Akizungumzia maambukizi kwa watoto wa darasa la saba ambao wanajiandaa na mitihani yao ya mwisho, Mwalimu Mkanapate, alisema awali wanafunzi 17 waliambukizwa na ugonjwa huo, na kwamba hali zao zinaendelea vizuri.

Aliongeza kuwa kama hali itaendelea hivyo, huenda darasa la saba pia wakashindwa kuendelea na masomo.Wakati shule hiyo ikifungwa, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, imesema Jumatatu ijayo inatarajia kutoa chanjo ya ugonjwa wa surua nchini, ikiwamo Wilaya ya Newala.

Chanjo hiyo itawahusu watoto walio na umri wa miaka mitatu hadi 15, ukiwa ni utekelezaji wa mipango ya Serikali ya kila baada ya miaka mitatu chanjo ya ugonjwa wa Surua.

Msemaji wa Wizara hiyo, Nsachris Mwamaja, aliyasema Serikali inatambua uwezekano wa ugonjwa huo wa mlipuko kutokea, hususani kwa wale ambao hawakupatiwa chanjo kipindi kilichopita mpango umeandaliwa wa kutoa kinga hiyo mara moja.

“Tunasikitishwa na mlipuko huo kutokea kabla ya mpango wetu kuanza, lakini hatua za haraka zitachukuliwa, ni kweli hakuna dawa ya surua, lakini zipo dawa za chanjo zipo na zitatolewa,” alisema.
CHANZO: NIPASHE

No comments: