Mwenyekiti wa Kamati Nambari 10 wa Bunge Maalumu la Katiba, Salmin Awadh Salmin akizungumza na waandishi wa habari Dodoma jana. Picha na Emmanuel Herman
Dodoma. Mapendekezo mapya yanayopelekwa kwenye Kamati za Bunge Maalumu kwa ajili ya kurekebisha baadhi ya Ibara za Rasimu ya Katiba, yamezua mivutano mikali kiasi cha baadhi ya sura kuwekwa kiporo au kurukwa na kamati husika.
Habari zilizolifikia gazeti hili zinasema mapendekezo hayo ni yale yanayozigusa taasisi kubwa za nchi, zikiwamo Bunge la Jamhuri ya Muungano na Mahakama, pamoja na nafasi za Makamu wa Rais.
Katika baadhi ya kamati yamepelekwa mapendekezo ambayo yanataka Bunge liwe na sehemu tatu ili kutoa fursa kwa mambo ya Tanzania Bara kujadiliwa bila wabunge kutoka Zanzibar kuwapo.
“Mapendekezo yaliyopo ni kwamba wanataka Bunge liwe na sehemu tatu ambazo ni Bunge la Muungano kwa masuala ya muungano na humohumo linakuwa na sehemu mbili ambazo ni wabunge wa Zanzibar kwa ajili ya masuala ya Wazanzibari na sehemu ya Tanganyika kwa ajili ya mambo ya bara,” kilisema chanzo chetu kutoka katika kamati moja ya Bunge hilo.
Hata hivyo, habari zinasema baadhi ya wajumbe wa kamati walikosoa pendekezo hilo kwa maelezo kwamba linashabihiana na muundo wa muungano wa serikali tatu ambao ulipendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba lakini ukapingwa na baadhi ya wajumbe wakiongozwa na walio wanachama wa CCM.
Jana Mwenyekiti wa Kamati Namba 8, Job Ndugai aliwaambia waandishi wa habari kwamba kamati yake imeshindwa kuafikiana kuhusu muundo wa Bunge la Muungano hivyo kulazimika kuliacha suala hilo ili kulifanyia uchunguzi kwanza.
“Mbali na sura ya 5 inayozungumzia uraia pacha ambayo ilitusumbua, lakini pia suala la Muundo wa Bunge la Muungano na Mahakama ya Muungano vilikuwa tatizo katika kamati yangu,” alisema Ndugai.
Licha ya kwamba Ndugai hakuzungumzia suala hilo kwa undani, lakini taarifa zilizolifikia gazeti hili zinasema muundo wa kuwa na sehemu tatu katika Bunge moja ndio uliozua mtafaruku kiasi cha kamati hiyo kuliahirisha.
Katika kamati namba 5, sura ya 10 inayozungumzia suala la Bunge na Mahakama imerukwa. Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo alisema: “Tumeamua kuendelea na mambo mengine kwanza maana hilo limeonekana kuwa ni gumu kwa sasa.”
Habari zaidi zinasema katika kamati hiyo namba tano, mapendekezo ya kuwapo kwa makamu wa rais watatu yalizua mjadala mkali kiasi cha kusababisha kuwapo kwa wajumbe walioamua kuandaa maoni ya wachache.
“Wamekuja na mapendekezo kwamba awepo Makamu wa Kwanza wa Rais ambaye atakuwa mgombea mwenza, Makamu wa Pili wa Rais ambaye atakuwa Rais wa Zanzibar na Makamu wa Tatu wa Rais ambaye ni Waziri Mkuu,” kilisema chanzo chetu kutoka ndani ya kamati hiyo na kuongeza:
“Lakini wapo waliokataa kama watano au sita hivi na wameamua kwamba wataandika maoni ya wachache kwa mujibu wa Kanuni ya 32 (10)”.
Hoja hiyo inafanana kabisa na ile iliyowasilishwa katika Kamati namba 10 na kusababisha mgawanyiko uliozalisha kuwapo kwa maoni ya wachache ambayo kwa mujibu wa taarifa zilizolifikia gazeti hili yataandaliwa na Mbunge wa Mpanda Mjini (Chadema), Said Arfi na mwenzake kutoka kundi la 201 Adil Mohamed Ali.
Katika Kamati Namba 11, habari zinasema suala hilo pia lilizua mvutano baina ya wajumbe wanaounga mkono mfumo wa Serikali mbili na wale wanaotaka Serikali tatu na kwamba aliyeokoa jahazi ni Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud Othman ambaye alitoa mapendekezo kuhusu mifumo yote miwili.
“Katika kamati yetu wanasema eti tayari mfumo wa Serikali mbili umepitishwa maana ndiyo unaungwa mkono na wengi, lakini wengine wamekataa, kwa hiyo ndiyo maana masuala kama haya yanatupa shida kwelikweli,” kilisema chanzo chetu.
Hata hivyo, kwa mujibu wa habari hizo, kamati hiyo namba 11 iliunda kamati ndogo ya watu watatu akiwamo Naibu Waziri wa Kilimo, Godfrey Zambi ili kupitia mapendekezo ya Othman kabla ya kuyarejesha kwenye kamati nzima kwa ajili ya kufanya uamuzi.
Kaimu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk Christina Mnzava alipotafutwa jana kutoa ufafanuzi wa suala hilo alisema asingeweza kuzungumza kwani alikuwa kwenye kikao. Othman kwa upande wake naye alisema hakuwa katika nafasi ya kuzungumzia suala hilo kwani lipo kwenye mamlaka ya kamati.
Habari zaidi zinasema pia kumekuwa na mvutano pale kunapokuwa na mapendekezo ya kufutwa kwa maneno Tanganyika na Shirikisho, kwani baadhi ya wajumbe wamekuwa wakitaka yaendelee kuwapo kama yalivyopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, hadi pale Bunge zima litakapofanya uamuzi.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati Namba 10, Salmin Awadh Salmin, alikiri kwamba katika maeneo mengi ambako kulikuwa na maneno hayo wameyaondoa kwa kuzingatia kuwa ndiyo yalikuwa makubaliano ya wengi.
“Ingawa bado tuna watu ambao ni sehemu ya Ukawa, lakini ni wachache na pamoja na hoja zao za msingi, lakini zinaonekana kumezwa na wajumbe walio wengi ambao ndio wanaounga mkono Serikali mbili,” alisema.
Akizungumzia changamoto zilizowapata ndani ya kamati yake, alitaja kuwa ni suala la kutenganisha madaraka ya mawaziri na wabunge.
Kwa maelezo ya kiongozi huyo, jambo hilo lilitoa mvutano mkali ndani ya kamati yake na kuwa litaamuliwa Jumatatu ingawa wao kwenye uraia walipitisha uraia pacha.
Frederick Sumaye
Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye ameshauri kusimamishwa kwa Mchakato wa Katiba kutokana na mvutano kati ya wajumbe wa Chama Cha Mapinduzi na wale wa kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) akionya kuwa bila ya maridhiano hakuna katiba bora.
Akifungua Kongamano la Kuombea Katiba Mpya na Uchaguzi na Amani nchini lililoandaliwa na Free Pentecostal Church in Tanzania (FPCT) na kufanyika mkoani Kigoma, Sumaye amesema kuwa Bunge ni nyumba ya kujenga hoja na siyo nyumba ya mapambano wala ubabe.
“Pamoja na umuhimu huu wa kupata Katiba Mpya, Watanzania tungependa katiba itakayopatikana kwa maelewano na maridhiano ya pande zote husika. Bunge ni nyumba ya kujenga hoja na siyo nyumba ya mapambano wala ubabe. Kinachotakiwa wabunge wote washiriki na hatima ya yote ni wengi wape na wachache wasikilizwe,” alisema Sumaye na kuongeza:
“Kama inaonekana dhahiri kuwa hatutapata katiba nzuri kwa wakati uliopo, ni busara mchakato huu ukasimama, Watanzania tukajipa muda zaidi tukayatafakari haya ili tuje tupate katiba mwafaka kwa muda mwafaka. Itakuwa ni ushindi batili kama tutang’ang’ania kutengeneza katiba ambayo siyo ya manufaa kwa Watanzania wote.
Sumaye ambaye ni mmoja wa makada wa CCM waliojipambanua kutaka kuwania urais mwakani, alisema mchakato huo umetumia fedha nyingi za walipakodi ambazo zingetumika katika kuboresha huduma mbalimbali za jamii kama vile afya, elimu, maji na miundombinu.
Alisema licha ya sura nyingi katika Rasimu ya Katiba, sura zinazozungumzia Muungano ndizo zimekuwa ngumu licha ya kila upande kutoonyesha nia ya kuuvunja.
Hata hivyo, Sumaye alipendekeza muundo wa serikali mbili, kwani kuongezwa kwa idadi ya Serikali hakutakuwa suluhisho.
Huku akionyesha kutoamini kama mchakato huo kuwa suluhisho la mwisho la maendeleo ya Watanzania, Sumaye alionya kuhusu ulafi wa madaraka:
“Kama tumefika hapa kwa sababu kuna matatizo ya madaraka au utawala kwa vyovyote jawabu lake siyo Serikali tatu kwa sababu kufanya hivyo kutafanya tatizo liwe kubwa zaidi. Kama tumefika hapa kwa sababu ya mivutano ya rasilimali, basi kuwa na mfumo wa Serikali tatu kutafanya hali iwe ngumu zaidi,” alisema na kuongeza:
“Kwa maoni yangu kama kuna mvutano wowote kati ya Serikali ya Jamhuri na Serikali ya Zanzibar katika muundo wa Serikali mbili, na tukaanzisha Serikali ya Tanganyika kabla hatujatatua mivutano iliyopo, hiyo mivutano itaendelea kuwapo na tutazalisha mivutano mingine mipya.”
Imeandaliwa na Neville Meena na Habel Chidawali, Dodoma, Elias Msuya Dar es Salaam wa Mwananchi
No comments:
Post a Comment