Advertisements

Thursday, August 21, 2014

JAJA AFUNGUA AKAUNTI YA MABAO YANGA IKIICHARAZA CHIPUKIZI FC 1-0, MAXIMO ATUMIA VIKOSI VIWILI TOFAUTI

Na Baraka Mpenja, Dar es salaam

YANGA SC imeibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Chipukizi FC ya Zanzibar katika mchezo wa kwanza wa kirafiki uliopigwa uwanja wa Gombani kisiwani Pemba.

Bao pekee katika mchezo huo limefungwa na Mbrazil, Geilson Santos Santana ‘Jaja’ katika dakika ya 6 ya mchezo.
Hii ilikuwa mechi ya kwanza kwa kocha wa Yanga, Mbrazil, Marcio Maximo kuwaona wachezaji wake wakicheza mechi ya kirafiki.

Ili kuhakikisha anawaona wachezaji wote, Maximo alitumia vikosi viwili tofauti kwa kila kipindi.

Kipindi cha kwanza, aliwaanzisha Deogratius Munish ‘Dida’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondani, Mbuyu Twite, Hassan Dilunga, Haruna Niyonzima, Geilson Santos ‘Jaja’, Mrisho Ngasa na Andrey Coutinho.

Kipindi cha pili Maximo aliingiza kikosi kipya ambacho kilikuwa Juma Kaseja, Salum Telela, Edward Charles, Rajab Zahir, Said Juma ‘Makapu’, Omega Seme, Saimon Msuva, Nizar Khalfan, Hamis Kiiza, Jeryson Tegete na Said Bahanuzi.

Hata hivyo mabadiliko hayo hayakuweza kubadili matokeo katika mchezo huo.

Yanga ipo kisiwani Pemba ambapo imepiga kambi kujiwinda na msimu mpya wa ligi kuu soka Tanzania bara unaotarajia kuanza septemba 20 mwaka huu.

Nao mahasimu wao, Wekundu wa Msimbazi Simba wapo kisiwani Unguja kujiwinda na ligi kuu.

Msimu ujao wa ligi kuu (septemba 20), Yanga wataanza ugenini dhidi Mtibwa Sugar katika dimba la Jamhuri mjini Morogoro, wakati Simba wataanza na Coastal Unioni Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

No comments: