Mwenyekiti wa CCM Taifa ,Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiongoza kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kwenye ukumbi wa NEC, Makao Makuu ya CCM Dodoma Agosti 19, 2014
Wakati Kamati Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ikikutana jana kujadili mchakato wa Katiba, makada zaidi wa chama hicho wameendelea kutoa kauli zinazodhihirisha kuwa kuna kazi ngumu ya kupata katiba mpya kama maridhiano katika Bunge Maalumu la Katiba hayatapatikana. Jana CC ilifanya kikao chake cha siku moja ikiwa na ajenda moja ya kupeana taarifa kuhusu mwenendo wa Bunge Maalum la Katiba, huku kada wake, ambaye ni Mbunge wa Kahama, James Lembeli, akisema ni kazi bure kwa Bunge hilo kuendelea bila kufikiwa maridhiano baina ya makundi yanayohasimiana.
Makundi hayo ni la wajumbe wa CCM na wanaotokana na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) linaloundwa na vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi.
Lembeli amesema busara iliyotumika kuahirisha Bunge hilo Aprili, mwaka huu, kupisha Bunge la Bajeti, itumike pia kuahirisha la sasa na fedha kuelekezwa kwenye miradi ya maendeleo.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya viwanja vya Bunge, mjini Dodoma, Lembeli alisema kuendelea kwa Bunge hilo ni kuharibu fedha za umma zinazotokana na kodi ya wananchi wa kawaida na kwamba, msimamo huo ni wake binafsi na kwa niaba ya wananchi wake.
“Kweli tuko hapa, tunalipwa posho. Lakini mwisho wa siku sidhani kama tutapata katiba mpya. Theluthi mbili ya wajumbe kutoka Zanzibar haitapatikana. Hapa tunakula nchi, huku wananchi wanaumia...fedha tunazotumia sasa zingeelekezwa kwenye ujenzi wa maabara, ambazo wananchi wanachangishwa,” alisema Lembeli.
Alisema hekima na busara zingetumika kusitisha Bunge hilo kwa muda wakati mambo yanawekwa sawa na pande zote kukaa pamoja na kujadiliana na kuwekana sawa.
Mathalani, alisema baba na mama wanapogombana ndani ya nyumba kwa masuala ya nyumba ili hali ya amani irejee, ni lazima wakae na kujadiliana na kwamba, suala la katiba ni lazima pande zinazosigana zikutane na kujadiliana.
Alisema yeye ameendelea kuwapo ndani ya Bunge hilo na mwisho wa siku atapiga kura kwa mujibu wa maoni ya wananchi wa jimbo lake.
“Iwapo wananchi watapiga kura kinyume cha kile tulichokiazimia ndani ya Bunge la Katiba ni wazi kuwa tuliotengeneza katiba hiyo tutatakiwa kuwajibika na kubeba lawama hiyo, ikiwamo kujiuzulu nafasi au kutochaguliwa tena kwenye majimbo,” alisema Lembeli.
Alisema ameshaishauri CCM juu ya suala hilo na kwamba, ameamua kubaki na msimamo wake na atautetea daima.
Hata hivyo, alimuunga mkono mjumbe Mwigulu Nchemba, kuwa maridhiano ni jambo la msingi kuliko kuendelea kutengeneza katiba, ambayo mwisho wa siku itakosa utashi au kukubaliwa na makundi yote.
Kuhusu kauli ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Fredrick Werema, kuwa wakati wa kupiga kura mwishoni theluthi mbili zikikosekana litaitishwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufanya marekebisho ya 15 ya katiba ya mwaka 1977, Lembeli alisema si sahihi kwa kuwa ni kusubiri kumaliza mabilioni ya shilingi na baadaye kushindikana ndiko wabadili sheria kwa ajili ya kufanya marekebisho ya baadhi ya vifungu kwenye katiba ya sasa.
“Tunafanya dhambi kubwa, siyo masuala ya imani. Lakini hii siyo sawa kutumia fedha kwa mambo yasiyo na tija na mwisho tusipate katiba. Siyo jambo jema kabisa,” alisema Lembeli.
Kauli hiyo ya Lembeli imetolewa wiki chache, baada ya wajumbe wenzake wa Bunge hilo, Mwigulu Nchemba, Ester Bulaya, Ally Keissy, Deo Filikunjombe, Ignas Malocha na Charles Mwijage, kushauri suala hilo.
MWIGULU NCHEMBA
Nchemba ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha, alilitaka Bunge hilo lijitathmini kama lina ulazima wa kuendelea wakati hakuna uhakika wa kupatikana kwa theluthi mbili.
Alisema kitendo cha Bunge hilo kukaa kwa siku 84 bila uhakika wa kupatikana kwa theluthi mbili kwa pande zote mbili inayohitajika kupitisha rasimu ya katiba mpya, hakiwezi kueleweka kwa Watanzania.
Nchemba alisema ni vyema kujua idadi ya wanaoshiriki awamu ya pili ya Bunge hilo ili kutoa uthibitisho kimahesabu kama uamuzi wa kuendelea kwa Bunge unaweza kuwa na maana.
Alisema anatambua jinsi walipakodi watakavyoumia, rasimu hiyo itakapokwama kupita kutokana na kukosekana kwa theluthi mbili ya pande zote. Mbali na Lembeli na Mwigulu wajumbe wengine wa bunge hilo kutoka CCM wameshatoa kauli za kupinga bunge hilo kuendelea bila kufikia maridhiano.
`ALLY KEISSY
Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), Ally Keissy, alisema msimamo wa Nchemba ndiyo msimamo sahihi, ambao unapaswa kufuatwa kuliko kuendelea na Bunge wakati wakijua kuwa theluthi mbili haitapatikana.
ESTER BULAYA
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Esther Bulaya, alisema kiukweli kutoka moyoni mwake anamuunga mkono Mwigulu Nchemba na kuwa wao wamepewa dhamana ya kulinda umoja wa kitaifa.
Bulaya aliongeza kusema Katiba ni maridhiano, huwezi kuwapuuza wanasiasa (Ukawa) , ambao wakienda kwenye mikutano ya hadhara wanapata watu kama sisi (CCM).
Alisema kusitishwa kwa vikao vya Bunge hilo hakutatafsiriwa ni ushindi kwa kundi lolote, iwe ni Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) au CCM, ambao ni wengi.
IGNAS MALOCHA
Ignas Malocha, Mbunge wa Kwela (CCM), aliunga mkono hoja Mwigulu kwa asilimia 100 akihoji haraka ya nini kutegeneza katiba ambayo haina maridhiano.
Alisema haiwezekani wabunge walipwe Sh. 300,000 kwa siku kutunga katiba, ambayo haina maridhiano, huku wananchi vijijini wakiishi bila majisafi, maabara, zahanati na wakati mwingine wakichangishwa kupata huduma hizo.
Malocha alisema wabunge wa CCM hawataki Bunge liendelee, lakini wanakwama kufanya hivyo kwa sababu ya umaskini na kuiogopa CCM isije ikawawajibisha kama wataonyesha msimamo tofauti.
DEO FILIKUNJOMBE
Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM), alisema kitendo cha wabunge wa CCM kuendelea na mkutano wa Bunge Maalumu la Katiba ni matumizi mabaya ya wingi wao ndani ya Bunge hilo.
Alisema haungi mkono hatua iliyofikiwa ya kitendo cha wajumbe wenzake wa CCM kuendelea na mchakato wa katiba mpya kwa sababu suala la katiba halina mshindi.
CHARLES MWIJAGE
Mbunge wa Muleba Kaskazini (CCM), Charles Mwijage, alipendekeza kusitishwa kwa mchakato huo kwa kuwa maridhiano ni jambo muhimu katika kutengeneza katiba.
“Alisema kukosekana kwa Ukawa bungeni kutaathiri upatikanaji wa katiba mpya kwa sababu suala hili linahitaji zaidi maridhiano ya pande zinazotofautiana kiitikadi.
Aliongeza kuwa angekuwa na uwezo, angeamua mchakato huu wa katiba usitishwe iendelee kutumika katiba ya sasa kwa sababu suala hilo linahitaji zaidi maridhiano.
JOSEPH BUTIKU
Kwa upande wake; aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Joseph Butiku, amesema kinachoendelea sasa katika mkutano wa Bunge Maalum la Katiba mjini Dodoma ni utoto huku akiwaonya Watanzania kutokuwa tayari kupokea katiba mpya ambayo haikutokana na maoni yao.
Pia amewataka Watanzania kutotishwa na mtu yeyoye bila kujali nafasi aliyo nayo pale anapoonekana kuhamisha maoni waliyoyapendekeza katika Rasimu ya Katiba na kwamba yeye yupo tayari kufa kwa ajili ya kutetea maoni yao yaliyomo kwenye rasimu hiyo.
Butiku ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam wakati akizindua wimbo na filamu iliyopewa jina la ‘Taifa ni Letu, Katiba ni Yetu’ ambayo imetengenezwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kwa ajili ya kutoa elimu kwa Watanzania kuhusu mchakato mzima wa katiba mpya.
Alisema kinachoendelea sasa katika mkutano wa Bunge Maalum la Katiba ni cha kitoto na kwamba katiba haiwezi kuundwa huku kundi moja la wajumbe wa bunge hilo wakiwa ndani na wengine nje na kuhoji uhalali wa katiba itakayoundwa iwapo itakuwa ya Watanzania wote au ya wanasiasa.
Tangu Aprili 16, mwaka huu, wajumbe kutoka Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), walisusia bunge hilo kwa hoja kadhaa ikiwamo kuwekwa kando kwa Rasimu iliyowasilishwa na Tume ya Jaji Warioba na kujadili rasimu iliyoandaliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Kinachoendelea pale bungeni ni mambo ya kitoto. Wengine wapo ndani na wengine wapo nje. Mtatengenezaje katiba? Hivi unatengeneza katiba ya nani? Katiba ni yetu msije mkakubali ikawa ya mtu mwingine, hilo msikubali, wala msitishwe na mtu hata akiwa nani,” alisema Butiku na kuongeza:
“Katiba ni yetu na siyo ya wanasiasa, Watanzania wameshasema, unawezaje kuhamisha mambo ya wananchi, bora nife nachochea maana wamesema sisi tunachochea. Msikubali katiba yenu mliyoandika ikavunjwa na yeyote maana hiyo ni sheria mama ya kukulinda wewe, mama na mtoto.”
Aidha, Butiku alieleza kusikitishwa na kauli zinazoendelea kutolewa na baadhi ya viongozi waandamizi wa vyama vya siasa kikiwamo CCM, kwamba yeye na wenzake waliokuwa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, walikusanya maoni ya uongo.
“Sisi kidogo tunafedheheka tunapoambiwa kuwa sisi ni waongo, tumekusanya uongo. Hivi kweli sisi na uzee wetu huu, uongo huu unaosemwa tutaenda wapi?” Alihoji Butiku Aliongeza: “Suala la Katiba lilianza zamani.
Karume alitaka kuwapo kwa nchi moja na serikali moja, Nyerere aliona vema kuwapo serikali mbili na nchi moja, Karume akakubali, lakini leo tuna serikali mbili na nchi mbili. Nchi moja imepatikana kwa kuvunja katiba. Kama ndiyo hivyo, sisi wazee hatumo, fanyeni ninyi wenyewe.”
Kwa mujibu wa Butiku, kumekuwapo mazungumzo ya muda mrefu kutoka kwa Watanzania wengi wakitaka katiba mpya na siyo yenye viraka kama ya sasa ilivyo na viraka 14 na kwamba Rais Kikwete aliridhia hilo kwa kuweka saini ikiwa ni pamoja na kwenye sheria ya kusimamia mchakato mzima, mara mbili, kabla na baada ya kuboreshwa.
“Rais alitengeneza utaratibu mzuri ili kuwahusisha Watanzani wote kutoa maoni yao kupitia Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Sheria pia ilitungwa, ikafanyiwa marekebisho, Rais akatia saini kwa mara ya kwanza na mara ya pili ili kuwaruhusu wananchi wote waweze kutoa maoni yao,” alisema.
Aliongeza: “Sheria hiyo haikueleza kwamba Rais alikuwa na nafasi maalum. Sheria ikaruhusu kuundwa kwa makundi mbalimbali pamoja na mabaraza. Pia uliwekwa utaratibu wa kuwafuata viongozi wetu wakuu akiwamo Rais wa Jamhuri ya Muungano, kutokana na utaratibu huo, tukapata rasimu ya kwanza na ya pili.”
Kutokana na hilo, Butiku, alisema, katiba ni ya wananchi na wala hakuna yeyote aliyepewa nafasi ya upendeleo maalum katika mchakato huo kwani tangu mwanzo walisisitiza asitokee mtu atakayevuruga utaratibu uliowekwa.
Butiku aliwapongeza LHRC kwa kutengeza filamu hiyo kwani inatoa elimu kwa Watanzania kuhusu umuhimu wa katiba mpya na ni ya wote.
Hivi karibuni, Butiku na wajumbe wenzake wa iliyokuwa Tume hiyo, akiwamo mwenyekiti wake, Jaji Warioba, wamekuwa wakishashambuliwa na baadhi ya wanasiasa wakiwamo wajumbe wa Bunge la Katiba na viongozi wa siasa hususani CCM, kwamba hawapaswi kuzungumzia chochote kuhusu mchakato huo kwa madai kazi yao ilimalizika baada ya kukabidhi rasimu ya pili.
CHANZO: NIPASHE

2 comments:
Ukweli bila wajumbe wa Ukawa kutoka Zanzibar 2/3 ya kura hazipatikani, namshangaa Ndugu Samia anaposema 2/3 ya wajumbe wa Zanzibar 145 hii sijui ni hesabu ya wapi! ! Wajumbe wa Zanzibar jumla ni 248, hivyo hesabu sahihi 2/3 ni wajumbe wasiopungua 165. Kuendelea kudanganya wananchi kuwa katiba itapatikana bila wajumbe wa Ukawa ni uongo na niubadhilifu wa pesa za wa lipa kodi.
Wacha wabunge wa CCM kutoka Zanzibar wazunguruke mbuyu wao Dodoma. Hawajui wanafanya nini na wanataka nini kwa Zanzibar. Aibu!!
Post a Comment