ANGALIA LIVE NEWS

Monday, August 11, 2014

Maalim Seif afunga kazi

  Aapa kamwe katiba mpya mpya haitapatikana kwa usanii
  Asisitiza hakuna mbunge CUF atarudi bungeni
Viongozi waandamizi wa Chama cha Wananchi (CUF) wamesema kinachoendelea katika Bunge Maalumu la Katiba mjini Dodoma ni usanii na kwamba hakuna katiba mpya itakayopatikanana bila ya wajumbe wa Bunge hilo wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Viongozi hao walisema hayo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Demokrasia Kibandamaiti, visiwani hapa.

MAZRUI
Akizungumza katika mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Nassor Ahmed Mazrui, alisema sababu zilizowatoa Ukawa ndani ya Bunge bado zipo palepale na kwamba, wasijidanganye kwamba, watarejea bungeni.


“Huu ni usanii. Ni kama mtu kujitekenya mwenyewe kisha akacheka mwenyewe na CCM ndiyo wanaofanya hivyo,” alisema Mazrui.

Aliwaonya watu wanaohoji takwimu zilizotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ambayo ndiyo iliyopewa mamlaka ya kisheria na siyo mtu mwingine.

RIYAMI
Mjumbe wa Kamati ya Maridhiano ya Umoja Kitaifa, Iddi Riyami, alilitaka Bunge hilo lisitishwe, kwani Wazanzibari hawako tayari kuona likiendelea.

Aliwataka mawaziri, Stephen Wasira (Ofisi ya Rais-Mahusiano na Uratibu) na William Lukuvi (Ofisi ya Waziri Mkuu-Sera, Uratibu na Bunge) kuondokana na dhana kwamba, katiba mpya inaweza kupatikana, huku Wazanzibar wakitengwa na kwamba, wanataka Serikali ya Zanzibar yenye meno na siyo iliyopo sasa.

Alisema mchakato wa katiba unaoendeleo Dodoma unaendeshwa kibandia na kwamba, hakuna katiba mpya itakayopatikana bila ya kuwapo na maridhiano.

JUSSA
Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa CUF, Ismail Jussa Ladhu, alisema Wazanzibari wanataka serikali tatu kama ilivyoainishwa katika rasimu ya katiba.

Alisema hakuna mjumbe wa CUF aliyerejea katika Bunge hilo kwa kuwa sababu zilizowatoa bado zipo palepale.

Jussa alisema kitendo cha Bunge hilo kuendelea kufanya usanii na maigizo kinamuondolea Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta, ndoto za kuwania urais mwaka 2015.

Alisema safari ya mamlaka kamili ya Zanzibar inakaribia na hakuna wa kuizuwia na kwamba, msimamo wa Wazanzibari kudai mamlaka hayo ipo palepale.

MAALIM SEIF
Katibu Mkuu wa CUF, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, alisema Wazanzibari wanahitaji amani na siyo fujo ili kuishi kwa upendo bila ya kubaguana.

Kuhusu mchakato wa katiba mpya, Maalim Seif alisema Sitta anacheza na kanuni ambazo zilitungwa na wajumbe wa Bunge hilo ili kuharibu mchakato huo.

Alisema Sitta amekuwa akisimamia mijadala bungeni inayolenga kuwajadili watu na kutoa matusi badala ya kujadili rasimu iliyopo mbele yao.

Alisisitiza kwamba hakuna mjumbe kutoka Ukawa atakayeshiriki na kupitisha katiba ambayo haina uhalali kisheria.

Akizungumzia kuhusu sakata la Mansour Yussuf Himid, aliyekamatwa na polisi kwa tuhuma za kumiliki silaha kinyume cha sheria, alisema ni ishara nzuri kwake.

“Kwenda jela ni ishara nzuri hata mitume walikwenda jela yaliyomkuta Mansour ni ishara nzuri ya kupata mamlaka kamili ya Zanzibar,” alisema Maalim Seif.

Mkutano huo ulihudhuriwa na maelfu ya wananchi visiwani Zanzibar na kwamba, viongozi wa CUF visiwani humu walitoa msimamo kwamba wajumbe wao hawatashiriki Bunge hilo.

CHIMBUKO LA MGOGORO
Aprili 16, mwaka huu, wajumbe wa vyama vinavyounda Ukawa walisusia kikao cha Bunge hilo kwa madai ya upendeleo na ubaguzi uliokuwa unafanywa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) dhidi ya vyama vingine.

Wajumbe hao wanaounda umoja huo kutoka vyama vya CUF, Chadema, NCCR-Mageuzi na wa vyama vingine, walichukua hatua hiyo pia wakituhumu kauli ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, waliyodai kuwa ni za ubaguzi na vitisho akiwa kanisani kwamba, Wazanzibari wanaotaka serikali tatu wanataka ijitenge ili iwe nchi ya Kiislamu.

Msimamo huo ulitolewa siku hiyo jioni na Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, Profesa Ibrahim Lipumba, ambaye alisema Lukuvi alitoa kauli hiyo mkoani Dodoma katika Kanisa la Methodist wakati wa sherehe za kumsimika Askofu Joseph Bundara wa Jimbo la Dodoma.

Profesa Lipumba alisema Lukuvi aliyemwakiisha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alizungumza lugha ya vitisho ndani ya kanisa kwamba, kama serikali tatu zitaundwa na serikali ya Muungano ikashindwa kuwalipa mshahara wanajeshi, jeshi litachukua nchi.

Alisema kauli hizo zilisababisha Askofu Bundara kusema kwamba, ni vema Katiba ya Zanzibar ikafutwa na kuundwa katiba moja.

Profesa Lipumba alisema Bunge limegeuka kuwa Interahamwe akimaanisha wanamgambo waliochochea ubaguzi na kusababisha mauaji ya kimbari nchini Rwanda mwaka 1994.

Hata hivyo, Profesa Lipumba alikaririwa akisema wanaweza kurudi bungenin endapo tu mambo yatakayokuwa yakijadiliwa ni yale tu yaliyomo katika rasimu iliyopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba, ukiwamo muundo wa Muungano wa serikali tatu.

MADHARA KWA THELUTHI MBILI
Ikiwa hawatarejea bungeni wataathiri upitishaji wa katiba kwa sababu kanuni namba 36 (1) bila kuathiri masharti ya sheria na kanuni hizi, mapendekezo ya marekebisho, au mabadiliko yaliokidhi matakwa ya na masharti ya kanuni hizi kuhusu sura za rasimu ya katiba zinazohusika yatajadiliwa na kupigiwa kura ibara kwa ibara katika kipindi kisichozidi siku moja.

Ibara ya 2 inasema mapendekezo ya marekebisho au mabadiliko yaliyowasilishwa kwa mujibu wa fasili ya (1) yatapigiwa kura na kupitishwa kwa kuungwa mkono kwa wingi wa theluthi mbili ya wajumbe wote kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili ya wajumbe wote kutoka Tanzania Zanzibar.

Ibara ya 3 inasema: “Pale mapendekezo ya marekebisho, maboresho au mabadiliko yatakubaliwa, ibara inayohusika ya rasimu ya katiba itahesabiwa kuwa imepitishwa pamoja na mabadiliko yake isipokuwa kwamba pale ambako mapendekezo ya marekebisho, maboresho au mabadiliko yatakataliwa, ibara inayohusika ya rasimu ya katiba itapigiwa kama ilivyokuwa kwa kufuata masharti ya fasiri ya (2).

Ibara ya Nne iansema: “Endapo baada ya kupigiwa kura, theluthi mbili ya wajumbe wote kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili ya wajumbe wote kutoka Tanzania Zanzibar haikufikiwa, basi ibara hiyo itapelekwa kwenye kamati ya mashauriano ili kupata muafaka.

”Sheria ya Mabadiliko ya Katiba inawatambua wajumbe wote waliokula kiapo na ndiyo sababu baadhi ya kamati miongoni mwa 12, zilizochambua rasimu zilishindwa kupitisha maamuzi kutokana na kukosa theluthi kwa pande zote wakati wa kupiga kura kutokana na baadhi ya wajumbe kutokuwapo.
 
CHANZO: NIPASHE

2 comments:

Anonymous said...

KATIBA IPATIKANE ISIPATIKANE WEWE NI DIKTETA UNATUMIWA KAMA KIBARAKA WA WAARABU WALA HAWANA UBAVU WA KURUDI ZANZIBAR KWANZA WEWE CHOKA MBAYA STAAFU SIASA HUNA JIPYA NAWASHANGAA VIJANA WALIOKO NYUMA YAKO LABDA NA KESHOKUTWA UTAWAONGOZA

Anonymous said...

wewe uliyeandika comment hapo juu wewe semeya huko huko kwenu bara na mambo yenu huku hujui cheo cha maalim. yeye kama kibara wawarabu wewe ni kibaraka wa nani, si wawazungu anayekuzungusheni na kukufanyeni wajinga kila siku na nyinyi bado mko chini ya makalio yao.

get a life looser wa bibara