Advertisements

Saturday, August 2, 2014

MALI URITHI WA BILIONEA WATOTO WAMGEUZIA KIBAO MAMA


Stori: Shakoor Jongo
LILE sakata la ugomvi wa mali zilizoachwa na bilionea maarufu Dar, Amir Tabu aliyefariki dunia hivi karibuni, limechukua sura mpya baada ya watoto wa marehemu kumvaa mama yao wa kambo, Mwanahamis Rajabu wakisema madai yake juu ya kudhulumiwa mirathi na mashemeji zake si ya kweli.

Wakizungumza katika mahojiano maalum walipoibuka kwenye ofisi za gazeti hili, Bamaga-Mwenge, Dar, watoto hao, Zainabu Amir, Ibrahim Amir, Ismail Amir, Bilali Amir, Ally Amir na Mohammed Amir walidai kwamba wanamshangaa mama yao huyo kudai kuwa alifukuzwa na baba zao wadogo, jambo ambalo halina ukweli wowote.

Walidai kwamba mama yao huyo alilenga kuichafua familia yao huku wakimuomba amuache baba yao apumzike huko aliko.“Wakati tukiwa msibani Bagamoyo tulikaa kikao cha familia zote yaani ya upande wa mwanaume na upande mwanamke, tena hadi baba yake mzazi alikuwepo, tulikubaliana kuwa mama akae Bagamoyo hadi arobaini itakapofika.


“Cha ajabu familia ya mama yetu ilikataa wakasema kuwa mtoto wao ataenda kukaa Mwananyamala Kisiwani (Dar) kwa wazazi wake.“Tulikubaliana na huduma zote zingekuwa zinatoka kwetu, sasa siku ya tukio wakati tunampeleka kwao ndipo mzozo ukaanza.

“Tulishangaa Afisa Mtendaji wa Kata ya Kawe, Mbezi Beach B (alikokuwa akiishi marehemu na familia yake kabla ya kurudishwa kwao Bagamoyo), Hamatton Bhao ghafla alitugeuka ndugu wa marehemu na kusema mjane huyo hawezi kwenda Mwananyamala wakati nyumbani kwake ni Mbezi Beach. Hapo ndipo tatizo lilipoanzia,” alisema Zainabu.

Watoto hao waliendelea kutiririka kwamba kilichofanya wasikubali kukaa Mbezi ni ubadhirifu wa mali za marehemu uliokuwa ukifanywa na mama yao.Walidai kabla ya tukio, walifanya uchunguzi wa kujua mali za marehemu ndipo wakakubaliana wafunge nyumba hadi arobaini itakapokwisha.

“Nadhani alijua kuwa uchunguzi wetu tutaibua ubadhirifu wa mali hivyo hakuwa tayari ndiyo maana akakimbilia kwenye vyombo vya habari kudai kuwa anadhulumiwa,” alidai Ibrahim.

Katika kujibu maswali waliyokuwa wakiulizwa wana mpango gani na mama yao huyo, watoto hao walisema kuwa kwanza wanamuomba asiwasingizie mashangazi na baba wadogo wao kwani kila kitu kitakuwa wazi baada ya arobaini ya baba yao.

Katika habari hiyo iliyoripotiwa na gazeti hili kwenye toleo lililopita, mama huyo alidai kwamba mali alizodhulumiwa na ndugu wa mumewe ni pamoja na magari ya kifahari, majumba, viwanja, hoteli na vitu vingine vya thamani.

GPL

No comments: