Advertisements

Wednesday, August 27, 2014

MBWEMBWE ZA YANGA ZITAMUWEZA MAXIMO

Haikunishangaza sana pale klabu ya Yanga ya Tanzania ilipoamua
kupeleka kikosi ambacho si cha kwanza katika michuano ya Kagame. Tena
ikaamua kupeleka kocha msaidizi badala ya kocha wake mkuu. Hiki kitu
kinafanyika Yanga pekee.

Sikushangaa pia pale shirikisho la vyama vya soka katika ukanda huu,
CECAFA lilipoamua kuiondoa Yanga katika michuano hiyo.

Hayo yote hayakunishangaza kwa sababu tabia za viongozi wa Yanga
nazijua na tabia za CECAFA zinafahamika.
Hawa wana mambo yao ya kitambo. Tangu Julai 2008, siku ile Yanga
walipogomea mchezo wa kumtafuta mshindi wa tatu katika michuano hii
hii ya kagame iliyofanyika hapa nchini.
Yanga walitia aibu ya karne siku hiyo. Wakiwa na kikosi bora kabisa,
wakaamua kukacha kucheza na Simba kwa madai kwamba wanaidai CECAFA
pesa zao. Sisi watu wa mpira tukaghadhabika vilivyo lakini siku chache
zilizofuata, ligi kuu ya England ikaanza. Tukahamia huko kama kawaida
yetu.

Hiyo ndio Yanga bwana.

Yanga wana mbwembwe kuliko timu zote za nchi hii. Wamegoma kupokea
pesa za udhamini wa Azam TV, wanasema ni kiduchu huku wakijua wazi
kwamba hawana mamlaka ya kuzuia michezo yao isioneshwe na kituo hicho.
Hii ina maana kwamba michezo yao itaoneshwa bure.

Pesa ambayo Yanga wanasema ni ndogo, ni nyingi kuliko zawadi ya
mshindi wa kwanza wa ligi kuu ambayo Yanga wanajiandaa kuishindania
kwa msimu mzima.

Hiyo ndio Yanga, timu maridadi na jeuri hapa nchini ambayo benchi lake
la ufundi linaongozwa na kocha kipenzi cha Watanzania, Mbrazil Marcio
Maximo.

Maximo ndiye kocha sahihi kabisa kwa soka la nchi kama Tanzania. Ndiye
aliyejenga msingi wa hapa soka letu lilipo leo ambao haukuwepo. Ndiye
aliyetuambia kwamba soka linafundishwa kwenye vilabu na siyo timu ya
taifa.

Maximo aliyasema hayo akiwa na timu ya taifa ya Tanzania.Ila leo Maximo yupo Yanga.

Yupo kwenye klabu ambako ndiko haswa wachezaji wanakopatikana. Tatizo ni
kwamba klabu hiyo ni Yanga na siyo Mtibwa Sugar wala Mbeya City.
Yanga ni klabu inayoamini kwamba tayari ipo peponi, wakati ukweli ni
kwamba hata hapa duniani tu haipo pazuri.

Akili ya shabiki wa yanga inaamini kwamba wao wana timu bora kabisa
inayoweza kuifunga Simba na kutwaa ubingwa wa Tanzania. Kutolewa hatua
ya kwanza katika kombe la shirikisho siyo aibu kwake kama ilivyo aibu
ya kufungwa na Simba.

Shabiki huyu imani yake ipo kwa Jaja, Okwi, Kiiza, Niyonzima, Twite na
majina mengine makubwa katika klabu.

Akili ya Maximo inalenga kutengeneza timu imara kwa kufuata misingi
sahihi. Timu yenye mchanganyiko wa damu changa na zilizopo ili Yanga
na taifa zima wafaidike. Hii ndio maana hasa ya klabu. Klabu yoyote
yenye kocha mwenye akili timamu ya soka huundwa hivi.

Akili ya shabiki wa Yanga inaamini benchi limewekwa kwa ajili ya Jerry
Tegete kukaa akimtazama Kiiza akicheza.
Siku Kiiza akiondoka tumlete Alan Wanga kwa mamilioni ya pesa aendelee
kutazamwa na Tegete.

Lakini akili ya Maximo yenyewe inaamini Tegete ameongezeka uzito tu na
atakuwa katika kiwango chake hivi karibuni.

Maximo haamini kwamba kuna pepo bila kufa kama tunavyoamini sisi. Yeye
bado ana mawazo kwamba Yanga inapaswa kutengeneza akina Tegete wengine
na akina Niyonzima wake. Na kama inawatamania akina Kipre Tchetche
basi iwatengeneze, wakiwa wengi iwauze pengine.

Hapa ndipo ninapopata shaka kwa sababu huu siyo utamaduni wa Yanga.
Kukuza vipaji na kuvitumia ni utamaduni wa Maximo lakini siyo
utamaduni wa Yanga.

Yanga haina muda wa kukuza vipaji kwa sababu kukuza vipaji hakuhitaji
mbwembwe. Yanga ina viongozi wenye mikogo. Hata Maximo mwenyewe
hawakumleta kwa sababu nyingine zaidi ya mbwembwe na mikogo ya pesa
zao.

Jambo kubwa na la maana kwao hivi sasa siyo kuibua kipaji pale
jangwani, wao wanatamani zaidi kumsajili Amisi Tambwe kutoka Simba,
hata kama hahitajiki ili tu wamvalishe jezi yao, wazunguke nae mji
mzima kisha watambe kwamba wao ni zaidi.

Walau Simba imewatoa akina Jonas Mkude.
Walau Azam imetufanya tumjue John Bocco, lakini Yanga haina utaratibu
huu, kama ulikuwepo basi ilikua enzi ya akina Keneth Mkapa na siyo
sasa..

Tayari nimemsikia Maximo akisema kwamba ana vijana wengi
wanaofundishwa na Salvatory Edward na Shadrack Nsajigwa na baadhi yao
atawajumuisha katika kikosi chake.
Nililitegemea hili kabla hata hajasema kwasababu hivi ndivyo alivyo Maximo.

Sasa naangalia zangu muvi tu mpaka ligi kuu ya Vodacom itakapoanza.
Najua kuna siku tu Kiiza au Okwi watachelewa kurejea klabuni kutoka
kwao Uganda. Najua Maximo ni aidha atawasimamisha au atawafukuza
kabisa lakini hatawapanga katika mchezo unaofuata.
Na katika hii mechi ndipo ambapo Maximo atawatumia vijana wake.

Naomba sana mechi hii iwe dhidi ya Simba halafu Yanga ishinde. Lakini
ikifungwa, kitakachotokea mtanipigia simu. Namba yangu ni 0766399341.

Richard Leonce Chardboy. SHAFFIHDAUDA


No comments: