ANGALIA LIVE NEWS

Monday, August 18, 2014

MeTL GROUP YAPATA MKOPO WA BILIONI 300/- KUTOKA RMB

speech
Afisa Mtendaji Mkuu wa MeTL GROUP, Mohammed Dewji (MB) akisoma risala yake kwenye hafla ya utiliaji saini wa mkopo wa Bilioni 300 za kitanzania kutoka Benki ya Rand Merchant ya Afrika Kusini (RMB) iliyofanyika kwenye hoteli ya Saxon jijini Johannesburg Afrika Kusini.

Na Mwandishi wetu.
Kampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited (MeTL) imetiliana saini mkataba na benki ya Rand Merchant (RMB) ya Afrika Kusini utakaoiwezesha kupata mkopo wa zaidi ya sh bilioni 300.
Mkataba huo umetiwa saini nchini Afrika Kusini na Ofisa Mtendaji Mkuu MeTL GROUP, Mohammed Dewji.
Akizungumza kabla ya kutiwa saini kwa mkataba huo,Dewji alisema kwamba mkataba huo wa kihistoria unatokana na RMB kuiamini kampuni yake ya MeTL tangu walipoanza mahusiano ya kibiashara mwaka 2007.
“MeTL na RMB tulianza mahusiano yetu mwaka 2007, wakati RMB ilipotukopesha dola za Marekani milioni 7.5million. Wakati huo MeTLilikuwa na bidhaa mbili tu,ngano na sukari! Toka wakati huo, MeTL imekuwa ikikua na kuongeza bidhaa zaidi.” Alisema Dewji na kuongeza kuwa mwaka jana 2013, uwezo wa MeTL wa kukopa sasa umefikia dola milioni 100.
signing deal
Ofisa Mtendaji Mkuu wa MeTL GROUP, Mohammed Dewji (Mb) (wa pili kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Rand Merchant Bank (RMB), Bw. Bruce Macfarlane (wa pili kulia) wakitiliana saini ya mkopo huo wa bilioni 300 za kitanzania. Kushoto ni Makamu wa Rais wa MeTL GROUP, Vipul Kakad na kulia ni Gregory Havermahl wa RMB wakishuhudia tukio hilo la utiliaji saini wa mkopo baina ya RMB na MeTL Group.

Dewji ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Singida Mjini amesema kampuni yake imekuwa na mafanikio makubwa kibiashara mpaka kuaminiwa na benki mbalimbali za ndani na nje ya nchi.
Pamoja na mkopo huo kwa MeTL hivi karibuni kupitia kampuni yake dada ya kuingiza, kuhifadhi na kusambaza mafuta nchini ya Star Oils Ltd, ilipata mkopo wa sh. bilioni 100 kutoka kwa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC).

“Mwaka 1999 wakati najiunga katika kampuni hii ya kifamilia biashara yetu ilikuwa ni ya dola za marekani milioni 26 na sasa tumejiongeza mara zaidi ya 60 kwani sasa pato letu litafikia dola za Marekani bilioni 1.5 ifikapo mwishoni mwa mwaka”, alisema Dewji.
Alisema mafanikio yalkiyopatikana ya kulipa mikopo husika yamewezesha yeye kusaini mkataba wa mkopo wa dola za Marekani milioni 200 ikiwa ni mwaka mmoja tu tangu wafikie uwezo wa kukopa dola milioni 100 za Marekani.
“Ninataka kusema kwamba maendeleo makubwa ya MeTL yasingelifikia hapa bila RMB kutuamini katika hatua za awali” alisema ofisa mtendaji huyo ambaye pia alielezea kazi mbalimbali zinazofanywa na MeTL.
Alisema kampuni yake inafanya shughuli anuai kwenye sekta mbalimbali, ikiwemo kilimo na viwanda, lojistiki, huduma za fedha,majumba ya biashara, petroli,vinu vya kusindika nafaka,vifaa vya plastiki, usambazaji na masuala ya simu.
Toast
Afisa Mtendaji Mkuu wa MeTL GROUP, Mohammed Dewji (Mb) na Mkurugenzi Mtendaji wa Rand Merchant Bank (RMB), Bw. Bruce Macfarlane wakinywa shampeni baada ya kufanya "Toast" kama ishara ya kutakiana kheri na mafanikio kwenye biashara zao.

Akisaini mkopo huo, Dewji aliwashukuru wote waliohudhuria hafla hiyo ya kusaini kati ya kampuni yake MeTL na RMB huku ikijivunia kufanya biashara katika nchi za Ethiopia, Malawi, Msumbiji, Zambia, Dubai, Uganda, Rwanda, Burundi, Congo, Sudan Kusini na Kenya.
Alisema kwamba kampuni hiyo inataka kujiimarisha zaidi katika sekta mbalimbali.MeTL kwa sasa ina viwanda zaidi ya 31 nchini Tanzania pekee; huku ikiwa imetawanyika katika nchi 11 zilizopo Kusini mwa jangwa la Sahara.
"Tumejitanua katika nchi mbalimbali barani Afrika, nashukuru kwa ushirikiano mzuri ambao umechangia mafanikio makubwa ya kampuni yetu", alisema Dewji.
Dewji maarufu kwa jina "MO" anasema elimu aliyoipata katika Chuo Kikuu cha Georgetown nchini Marekani ndio iliyomfumbua macho na kuona umuhimu wa kutumia fursa za ushindani wa kibiashara duniani.
“Nia yetu ni kuwa na nguvu kubwa ya kibiashara Afrika Mashariki na Kati tukipania MeTL kuwa na pato la zaidi ya dola za Marekani bilioni 5 kwa mwaka ifikapo mwaka 2018 na kutengeneza ajira za watu 100,000.” Alisema Dewji
Alisema katika hotuba yake hiyo kuwa siri ya mafanikio ya kampuni ya MeTL ya kukua kwa zaidi ya mara 60 katika kipindi cha miaka 15 tangu alipojiunga nayo kuwa ni kutumia vyema fursa zilizopo na pia hamu yangu ya kuwatumikia na kuboresha maisha ya watanzania.
“Falsafa yangu kama mfanyabiashara sio kuridhika na mafanikio niliyonayo bali kuendelea kufanyakazi kwa bidii na kufanikiwa zaidi.” Alisema.
Chat
Afisa Mtendaji Mkuu wa MeTL GROUP, Mohammed Dewji (Mb) (katikati) akibadilishana mawazo na Mkurugenzi Mtendaji wa Rand Merchant Bank (RMB), Bw. Bruce Macfarlane (kulia). mara baada ya kutiliana saini mkopo wa Bilioni 300 za Kitanzania.

No comments: