ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, August 13, 2014

Mjumbe afuatwa wodini kupiga kura

Dodoma. Mbunge aliyelazwa katika hospitali ya Mkoa wa Dodoma, Thomas Mgilo baada ya kupigwa na watu wasiojulikana amefuatwa hospitalini ili apige kura kupitisha baadhi ya sura za rasimu.
Tukio hilo limekuja kukiwa na taarifa kuwa baadhi ya kamati zinashindwa kupiga kura kuamua au kuchelewa kuanza vikao vyake kutokana na tatizo la akidi.
Kwa mujibu wa kanuni za Bunge Maalumu, idadi ya wajumbe wanaotakiwa ili kuruhusu kikao kuanza ni nusu ya wajumbe wote, wakati theluthi mbili inatakiwa wakati wa kupiga kura.
Jana, Makamu Mwenyekiti wa Kamati namba 12, Thuwayba Kisasi akiwa ameongozana na polisi walimpelekea karatasi za kupiga kura Mgilo na alipiga kura ya wazi kuamua kuhusu Ibara ya 39 ya Sura ya Nne ambayo pamoja na mambo mengine, inazungumzia haki za mtuhumiwa au mfungwa.
Ibara hiyo inataka kutoa ruhusa kwa wafungwa wenye ulemavu kuingia na magongo yao kifungoni, jambo ambalo Mgilo alilipinga. Alisema hawezi kuunga mkono wafungwa wenye ulemavu kwenda na magongo gerezani kwani wanaweza kuyatumia kuwadhuru wengine.
Mwenyekiti wa Kamati namba 12, Paul Kimiti alisema Mgoli aliomba kushiriki katika upigaji huo wa kura.
“Nilimtembelea mgonjwa (Mgoli) asubuhi akasema hali yake ni ahueni na akaomba kwa mwenyekiti ashiriki kupiga kura katika kamati,” alisema Kimiti.
“Kwa hiyo nilimtuma Makamu Mwenyekiti akaenda huko hospitali na kweli mgonjwa wetu amepiga kura na leo tulipigia kura Sura namba 2, 3, 4 na tano na tayari kamati yangu ilipata kura za kutosha kwa pande zote za muungano.”
Changamoto ya akidi
Kumekuwa na taarifa za ama kuchelewa kuanza kwa vikao vya kamati au kamati kuahirisha kufanya uamuzi kutokana na idadi ya wajumbe kutokidhi matakwa ya kikanuni, huku kamati nyingine zikiamua kutozingatia suala hilo.
Mwananchi

No comments: