Wiki iliyopita tuliona jinsi mpishi anavyoweza kuukabili
ugonjwa wa kisukari kwa uhakika kabisa. Mpishi bado ana nafasi kubwa sana ya
kuokoa maisha ya walaji wake tena katika hali ya hatari ya kufa kwa maradhi
yasiyoeleweka kama homa. Kila mtu anaijua kwa uhakika sana homa. Hakuna hata
mmoja wetu ambaye hawahi kuugua homa kote ulimwenguni na kibaya zaidi homa
hutukumba zaidi watu tulioko kusini mwa jangwa la sahara na hushambulia zaidi
akina mama na watoto wenye umri chini ya miaka 15 Watanzania tukiwemo kundini.
Nikushangaze msomaji wangu kuwa homa sio ugonjwa! Ndio, homa
ni maumivu tu au ‘shabiki’ wa maradhi mengine yanayotukumba binadamu. Kwa
kawaida mwili ukikutana na shambulio lolote liwe la bacteria, virusi au hata
kisaikolojia basi joto litapanda na mtu atajisikia maumivu na hali hiyo ndio
kitaalamu inaitwa ‘Homa’
Ukiwa na homa, protini na virutubisho vingi sana hupotea
mwilini huku hamu ya kula nayo hukata na kupotea kabisa. Hii humfanya mgonjwa
kupoteza uzito na ikimlaza kwa muda mrefu hupooza na baadaye anaweza akapoteza
maisha asipotibiwa. Hali hii hutokana na kupoteza vitamins B complex na vitamin
C kwa wingi sana kupitia mkojo wa njano ambao wote tukiugua hukojoa hivyo.
Mgonjwa anapofikia hatua hii, Mpishi husaidia kuokoa maisha
yake kwa kumpa vyakula vyenye protini kwa wingi japo mgonjwa husumbua kidogo
kutokana na homa kumpotezea hamu ya kula ila kama atakuwa anatapika pia basi
kazi itakuwa ngumu sana na mpishi anaweza akaagiza mgonjwa apewe ‘vitamins
supplements’ za vidonge ili kujazia mlo wake kwa usahihi na haraka apone. Bado
Mpishi atatakiwa ahakikishe mdomo wa mgonjwa ni safi muda wote maana homa
huzalisha taka mdomoni na kumfanya mgonjwa akate hamu ya kula pia. Mpishi
anaweza akampa kachumbari mara kwa mara na akaona maajabu!
Homa huwa za muda mfupi, zipo za muda mrefu na zipo homa za
kujirudia mara kwa mara pia. Kwa homa za muda mfupi kama vile malaria, typhoid,
kuharisha n.k. Mpishi atampikia mgonjwa wake vyakula vya kimiminika tu kwa siku
mbili mfululizo ili kwenda sambamba na upotevu wa maji mwilini na pia mgonjwa
ataweza kula kwa urahisi. Juisi, maziwa, uji, supu, mtori n.k. vitamfaa sana
mgonjwa na endapo atakojoa mkojo kiasi cha lita mbili ni dalili wazi kuwa
anapona.
Kwa homa za muda mrefu zinazojishabikia katika maradhi kama
vile kifua kikuu, ukimwi, majeraha ya upasuaji, saratani, na hata ajali pia
Mpishi atahakikisha mgonjwa anapata vyakula laini na kidogokidogo walau milo
mitano kwa siku ili mgonjwa aweze kwenda sambasamba na uharibifu unaosababishwa
na homa. Msisitizo upo katika vyakula vyenye maji zaidi kwa sababu homa
hupoteza maji mengi kupitia jasho la stress, mkojo, kutapika nap engine hata
kuharisha pia. Hivyo Mpishi humpa mgonjwa vimiminika kwa wastani wa lita 2 hadi
3 katika mfumo wa lishe ili arudishe madini, vitamin na virutubisho vingine pia
na uhakika wa mgonjwa kupona ni mkubwa na uhakika.
Nadhani tumeelewa vizuri namna anavyoweza kuikabili homa.
Bado mpishi ana uwezo wa kuyakabili maradhi kibao! Usikose makala hii kila
jumanne kwani bado tunaendelea kukuletea pilikapilika za mpishi jikoni
akiwapikia wagonjwa wa maradhi tofauti. Unaweza ukawa na swali, hoja, maoni au
ushauri wa kina juu ya Mpishi. Usisite kutupigia na kutembelea tovuti yetu hapo
juu.
John Haule
0768 215 956
No comments:
Post a Comment