Waliofariki dunia papo hapo ni Sayi Otieno na mkewe Quenter Kweko ambao walikandamizwa na jiwe kubwa lililovunja nyumba waliyokuwa wakiishi huku mtoto wao (jina halikupatikana mara moja) mwenye umri wa miaka minne akinusurika.
Jiwe hilo pia lilisukuma jiwe jingine ambalo liliporomoka na kuipiga nyumba ya Joseph William na kuwaua watoto wawili papo hapo.
Waliofariki ni Keflin Masalu (14) na Emmanuel William (12) anayesoma darasa la tano. Mtoto mwingine Geophrey Joseph (14) wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Mbugani alinusurika.
Wakizungumza katika eneo la tukio, Juma Seleman mkazi wa eneo hilo alisema wakati mvua inanyesha saa 8:30 usiku, walisikia mtikisiko mkubwa baada ya radi kupiga na muda si mrefu zikasika sauti za watu kuomba msaada.
“Kelele hizo ziliweza kutuamsha majirani na kwenda eneo la tukio, hapo tuliwakuta watoto wawili wakiwa wamekandamizwa na jiwe kubwa na nyumba nyingine tukaona jiwe kubwa limeikandamiza nyumba na hakuna mtu aliyeonekana,” alisema Seleman.
Hassan Maulidi ambaye ni Mwenyekiti wa mtaa huo, alisema baada ya wananchi na kikosi cha zimamoto kufanikiwa kutoa miili hiyo, ilipelekwa kuhifadhiwa chumba cha maiti katika hospitali ya Rufaa Bugando.
Akizungumza na NIPASHE Jumapili, baba wa watoto waliofariki, Joseph William, alisema akiwa amelala chumba tofauti na watoto wake huku mvua kubwa ikinyesha radi kali ilipiga hivyo alitoka nje na kukuta taa zimezimika.
“Lakini nilipoingia ndani tu, nilisikia kishindo kikubwa kikitokea nyuma ya nyumba yangu na kuona jiwe kubwa limeingia na kuwakandamiza watoto wangu waliokuwa wamelala,” alisema William.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment