ANGALIA LIVE NEWS

Monday, August 18, 2014

Mbatia asema kauli ya Werema imejaa unafiki

Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia (kulia) akizungumza na waandishi jijini Dar es Salaam jana. Kushoto ni Katibu Mkuu wa chama hicho, Mosena Nyambabe. Picha na Salim Shao

Dar es Salaam. Siku moja baada Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema kueleza kuwa hakuna mwenye mamlaka kisheria kuvunja au kusitiza Bunge la Katiba, mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi amesema kauli hiyo imejaa unafiki na kwamba upo uwezekano wa kuahirisha vikao kwa muda mpaka mwafaka wa kitaifa utakapopatikana.
Mwenyekiti huyo, James Mbatia amesema kuahirisha Bunge kunawezekana kama ambavyo iliwezekana kusitishwa vikao vya Bunge hilo Aprili mwaka huu kupisha Bunge la Bajeti na kubadilishwa kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kinyemela kwa kuongeza idadi ya siku za Bunge la Katiba kutoka 70 hadi 90 mpaka kuwa muda wowote ambao utaonekana unafaa.
Wakati Mbatia akieleza hayo, jana waliibuka wazee wa Jiji la Dar es Salaam wakiwataka Watanzania kuyaombea makundi yanayovutana na moja likisusia vikao vya Bunge hilo vinavyoendelea mjini Dodoma, ili yakutane na yakubali kufikia mwafaka kwa pamoja.
Kauli ya Mbatia
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mbatia alisema kauli iliyotolewa juzi na Jaji Frederick Werema imejaa unafiki.
Katika mkutano huo ambao Mbatia pia alieleza maazimio ya mkutano wa halmashauri kuu ya chama hicho uliofanyika Agosti 14, mwaka huu, alihoji kama Bunge la Katiba haliwezi kusitishwa, iliwezekana vipi kulisitisha kupisha Bunge la Bajeti.
Mbatia alisema ni jambo la ajabu kuona watu wakitunga sheria kwa ajili ya kukinufaisha kikundi cha watu wachache na akasisitiza kuwa kufanya hivyo ni sawa na kuwahadaa Watanzania.
“Kama katika awamu ya kwanza tuliweza kuliahirisha Bunge la Katiba kupisha Bunge la Bajeti bila kuwapo kwa sheria, pia tunaweza kulihairisha katika awamu ya pili ya Bunge hilo kupisha maridhiano. Mshikamao wa kitaifa ni zaidi ya Bunge la Bajeti na kitu chochote,” alisema.
“Tatizo la Watanzania ni kuwa na umaskini wa fikra uliobebwa na ujinga, fitna, umbeya, kusema uongo, kujenga chuki katika jamii na uvivu wa kufikiri. Maridhiano ya kitaifa ni njia pekee ya kunusuru mchakato wa Katiba.”
Alisema wajumbe wanaoendelea na vikao vya Bunge hilo mjini Dodoma wanakusudia kupitisha rasimu kwa ajili ya kukibeba chama kimoja cha siasa na siyo kwa ajili ya masilahi wa Watanzania.
“Dola inaundwa kwa msingi wa maridhiano, siasa inafuata baadaye. Hilo lilifanyika Zanzibar na nchi nyingi barani Afrika zilizokumbwa na machafuko ya wenyewe kwa wenyewe wakati wa kuandika Katiba,” alisisitiza.
Akizungumzia maazimio ya halmashauri kuu, Mbatia alisema: “Tumeitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuliweka hadharani Daftari la Kudumu la Wapigakura lililoboreshwa mwaka 2010, kutokana na hivi karibuni tume hiyo kueleza kuwa hakuna daftari. Tunajiuliza kama halipo hata walioshinda chaguzi zilizopita siyo halali.”
Alisema kwa kauli hiyo maana yake ni kwamba ukifanyika uchaguzi wowote nchini hakuna atakayeweza kupiga kura, kutaka mfumo wa uandikishaji wapigakura wa kieletroniki (BVR) uwekwe wazi na kusimamiwa na Tume Huru ya Uchaguzi yenye weledi, kutokana na kukiri hadharani kuwa iliyopo sasa imeshindwa kazi.
“Tunaitaka Serikali itamke wazi tarehe ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na usimamiwe na Tume Huru ya Uchaguzi kwa kutumia Daftari la Kudumu la Wapigakura lililoboreshwa,” alisisitiza.
Wazee wa Dar es Salaam
Wakati huohuo, wazee watano wa Dar es Salaam Yahya Ngoma, Kapteni mstaafu, Alhaji Mohammed Ligora, Ali Bakari Mukhi na Alhaji Omari Chiwaka wamewataka Watanzania kuyaombea makundi yanayovutana katika mchakato wa Katiba.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake katika Ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo, Alhaji Ligora alisema kitendo cha Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kususia vikao vya Bunge hilo na wenzao wakiendelea na vikao kinatakiwa kuombewa.
“Hakuna haja ya kuwazomea hawa na kuwafurahia wale au kinyume chake. Tunatakiwa kuwaombea ni shetani tu kaingia kati yao,” alisema Alhaji Ligora.
Mwananchi

No comments: