Kocha Patrick Phiri ametua tena nchini kuinoa timu ya Simba ambayo imekosa michuano ya kimataifa kwa misimu mitatu baada ya kufanya vibaya katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara
Kocha Patrick Phiri ametua tena nchini kuinoa timu ya Simba ambayo imekosa michuano ya kimataifa kwa misimu mitatu baada ya kufanya vibaya katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, VPL.
Hii ni mara ya tatu kwa Mzambia huyo kuinoa klabu hiyo yenye maskani yake mtaa wa Msimbazi jijini Dar e Salaam baada ya kuiongoza pia 2004-2005 kabla ya kuipa taji la kihistoria la VPL msimu wa 2009-2010 aliomaliza bila kupoteza hata mechi moja, rekodi ambayo ilifikiwa na Azam FC msimu uliopita.
Phiri, ambaye anakuwa kocha wa 18 kuinoa Simba ndani ya miaka 16 tangu 1998, si kocha peke aliyewahi kuifundisha Simba katika misimu tofauti kwani gwiji wa zamani wa klabu hiyo mwenye rekodi pekee ya kufunga mabao matatu peke yake katika mechi moja ya watani wa jadi, Simba na Yanga, Abdallah ‘King’ Kibadeni aliwahi kuifundisha timu hiyo msimu wa 2000 ambao Mtibwa Sugar walitwaa taji la Ligi Kuu kabla ya kuinoa tena msimu uliopita aliotimuliwa bila sababu za msingi.
Kocha Mserbia Milovan Cirkovic naye aliwahi kuwa kocha mkuu wa Wanamsimbazi kwa misimu miwili tofauti 2008/9 na 2011/12 alipowapa ubingwa, tena kwa kuifunga Yanga mabao 5-0 katika mechi ya mwisho.
Watani wao wa jadi, Yanga ambao kwa sasa wako chini ya Kocha Mbrazil Marcio Maximo ambaye anakuwa kocha wa 24 kukinoa kikosi chao ndani ya miaka 23 tangu 1991, nao wana tabia hiyo hiyo ya kutimua makocha na baadaye kuwarudisha kunoa timu yao huku wakiwa hawana jipya zaidi ya kuzipa mafanikio ya ubingwa wa ndani tu.
1991-1993 Syllersaid Mziray alikinoa kikosi cha Wanajangwani na alirejea tena kukiongoza 2004 na mwaka uliofuata alikiacha chini ya Kenny Mwaisabula.
Kocha Jack Chamangwana raia wa Malawi alikuwa Kocha Mkuu Yanga 2002, akirejeshwa tena 2006, na 2007, mwaka ambao Yanga ilipita chini ya makocha watatu ikianza na Mserbia Milutin Sredojevic ‘Micho’, Mkenya Razack Ssiwa kabla ya kuwa mikononi mwa Mmalawi huyo – Chamangwana.
Kocha mzawa Boniface Mkwasa, kabla ya kuwa kocha msaidizi wa Yanga chini ya Kocha Mkuu, Mholanzi Hans van der Pluijm msimu uliopita, aliwahi kuwa kocha mkuu wa timu hiyo 2001.
Mserbia Kostadin Papic anafunga orodha ya makocha walioajiriwa na kutimuliwa Yanga kisha kurejeshwa alipofanya hivyo 2010, mwaka uliofuata klabu ikamwajiri Mganda Sam Timbe ambaye pia hakudumu kwani mwaka huo huo (2011) uongozi huo wa Jangwani ulimrudisha.
Hata hivyo, Papic hakudumu tena baada ya kutimuliwa na kuletwa Mbelgiji Tom Saintfiet (2012) ambaye pia alitimuliwa mwaka huo huo licha ya kuipa Yanga ubingwa wa Kombe la Kagame la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati na kukiacha kikosi chini ya Mholanzi Ernie Brandts ambaye pia alitimuliwa licha ya kuwapa taji la VPL lakini akafungwa mabao 3-1 dhidi ya Simba, tena katika mechi ya ‘ndondo’ ya ‘Nani Mtani Jembe’.
Makocha Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ na Felix Minziro kwa nyakati toafuati wamekuwa wakizinoa kwa muda timu za Simba na Yanga baada ya makocha wakuu kutimuliwa, lakini nao wamekuwa wakikumbana na ‘dhahama’ hiyo ya kuharibiwa wasifu (CV) wao na klabu hizo kongwe nchini.
Tofauti na ilivyo kwa klabu kubwa ulimwenguni ambazo zimekuwa zikiwarudisha makocha zilizowahi kuwatimua kwa kuzingia rekodi nzuri za timu wanazokwenda kuzinoa baada ya kutimuliwa, viongozi wa Simba na Yanga wamekuwa wakiwarejesha bila kuzingatia vigezo muhimu.
Mbaya zaidi, baadhi ya makocha wanaorejeshwa na klabu hizo zilizoanzishwa miaka ya 1936 na 1935, wanaletwa kuzifundisha klabu hizo wakiwa ni makocha huru (hawana timu kwa wakati husika).
José Mourinho alitua Chelsea ya Ligi Kuu ya England (EPL) 2004 na kukaa na timu hiyo hadi 2007 akitokea FC Porto lakini akapishana lugha na mmiliki wa Chelsea akamua kwenda Internazionale Milan ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A) 2008 ambako alikaa hadi 2010 akifanya kazi nzuri ya kutwaa mataji matatu ya Serie A, Kombe Ligi ya Italia ‘FA’ na Klabu Bingwa Ulaya (UEFA Champions League).
Mreno huyo alihamia jijini Madrid na kuiongoza Real Madrid 2010 hadi 2013 ambako licha ya kutwaa mataji makubwa, alifanikiwa kuumaliza utawala wa Barcelona katika Ligi Kuu ya Hispania (La Liga) na kumshawishi mmiliki wa Chelsea, Roman Abramovich kumrejesha tena Darajani.
Viongozi wa Simba wamemrejesha Phiri pasipo kuzingatia ubora wake wa ukocha kwa kipindi hiki. Ni maamuzi ambayo yanaonekana ni ya kukurupuka yenye lengo la kuwahadaa wanachama na mashabiki wao ambao Jumamosi walishuhudia kikosi chao kilifungwa 3-0 na Zesco ya Zambia katika mechi ya kirafiki jijini Dar es Salaam.
Phiri, aliyetwaa taji la kocha bora wa VPL msimu wa 2010/11, ameweka rekodi ya kuwa kocha wa 12 kutimuliwa katika Ligi Kuu ya Zambia yenye timu 16 baada ya kikosi cha NAPSA Stars kumaliza mbele ya timu mbili tu za mkiani mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo.
Makocha wote waliowahi kuajiriwa, kuondoka na kisha kurejesha Simba na Yanga hawajaleta tija kwa klabu hizo kwani hakuna hata mmoja wao aliyefanikiwa walau kucheza hatua ya robo fainali za Klabu Bingwa Afrika.
Wengi wao wamefanikiwa kutwaa taji la Ligi Kuu. Hiyo ni sawa na kuwa na mwanafunzi bora aliyepata alama za juu katika darasa lenye wanafunzi wajinga wengi maana akipelekwa kwenye darasa la wanaojua, anakuwa wa mwisho.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment