By FRANK SANGA (email the author)
Nikarudia kusikiliza katika redio jioni yake ya siku hiyo. Nikasoma magazeti siku inayofuata ili kujiridhisha, nikarudia kusoma magazeti karibu yote.
Sikumuelewa.
NILIMSIKILIZA Katibu Mkuu wa Yanga, Benno Njovu mwishoni mwa wiki akizungumza. Akataja sababu nane za klabu hiyo kujitoa katika mashindano ya Kombe la Kagame.
Nikarudia kusikiliza katika redio jioni yake ya siku hiyo. Nikasoma magazeti siku inayofuata ili kujiridhisha, nikarudia kusoma magazeti karibu yote.
Sikumuelewa.
Kwa sababu sikumuelewa, nikahisi labda nina tatizo ndiyo maana sijaelewa. Nikajaribu kurudia tena kusoma alichokisema, bado sikumuelewa.
Sikumuelewa kama ambavyo sijaelewa ninavyoambiwa kuwa uchumi wa nchi unakua wakati umaskini wa watu binafsi unaongezeka na hali inazidi kuwa mbaya kila siku.
Sikumwelewa kama ambavyo sijawahi kuelewa kwa nini Tanzania inakuwa maskini licha ya kuwa na ardhi nzuri, madini, vivutio vya kitalii na rasilimali kibao.
Sikumuelewa katibu wa Yanga kama ambavyo nimeshindwa kuelewa ilipoishia timu ya taifa ya maboresho katika mpango bomu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Sikuelewa sababu nane za Yanga kama ambavyo sijaelewa malengo ya TFF kuhama ofisi zao za Karume na kuhamia ofisi za bei mbaya pale Posta katikati ya jiji la Dar es Salaam.
Sijamwelewa mpaka sasa kama ambayo imekuwa shida kwangu kuelewa kwa nini jezi za timu ya taifa ‘Taifa Stars’ zimebadilishwa kiholela.
Sikuona la kushangaza kutoka kwa Katibu wa Yanga. Huu ni mwendelezo wa ubabaishaji wa viongozi wetu kuanzia kwenye soka mpaka sekta nyingine kama siasa.
Bado tunakumbuka jinsi Yanga ilivyojitoa katika mashindano ya Kombe la Mapinduzi ya Zanzibar mwishoni mwa mwaka jana na mwanzoni mwa mwaka huu kwa madai kuwa haikuwa na benchi la ufundi baada ya kumfukuza kocha wake Mholanzi Ernest Brandts.
Tunakumbuka jinsi Yanga ilivyokiri makosa baadaye na kutoa kifuta jasho cha Sh 10 milioni kwa waandaji wa michuano hiyo pamoja na kuomba radhi kwa kitendo hicho.
Tunakumbuka vizuri jinsi Yanga ilivyogoma kucheza mechi ya mshindi wa tatu baina yao na Simba mwaka 2008 katika michuano ya Kombe la Kagame kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.Yanga chini ya mwenyekiti wao, Iman Madega walisingizia kuwa waliahidiwa Sh 50 milioni na TFF ili wacheze mechi hiyo. Wengine tukabaki kujiuliza inawezekana vipi?
Siku za mwisho za kocha Dusan Kondic alikiri kuwa hakukuwa na ahadi yoyote kutoka TFF, ila siku hiyo Yanga ilikuwa na wachezaji wengi majeruhi kiasi kwamba hata benchi lake la akiba hakukuwa na mchezaji yeyote.
Sitaki kuzungumzia lolote kuhusu kocha Marcio Maximo kwa sasa, mpaka hapo ligi itakapoanza, lakini kwa jumla ni kuwa Katibu wa Yanga hakuwa na sababu ya msingi labda ningemuelewa kama angesema kuwa kocha wao hataki kujivurugia mapema kiasi hiki.
Ligi Kuu Bara ina mechi 26 tu, ilikuwa bahati gani kwa Yanga kujiweka fiti katika mashindano hayo ambayo yangewafanya wawe na u-tayari wa mechi zote zijazo.
Nadhani sasa nimeanza kuelewa kwa nini nchi hii haina maendeleo, kwa sababu tuna viongozi waoga, wanafiki, wenye majungu na wanaokwenda na upepo.
Credit:Mwanaspoti
1 comment:
Wewe wasema!
Umepasua jipu ambalo kila mtu analiona lakini limekuwa likifumbiwa macho.Yanga hata ikimleta Kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani iliyoshinda World Cup, bado watamfukuza tu, kama sio kumchapa bakora!. Muelekeo wa soka Tanzania, timu zinatakiwa kuchukua mafunzo toka Azam. Wanakoelekea, ndiko Yanga na Simba walitakiwa wawe wamefuzu zamani, lakini kilichobaki ni ubabaishaji tu, na ulozi mwiiingi!.
Mawazo mafupi, fikra duni na uroho wa kujitajirisha haraka haraka ni miongoni mwa udhaifu wa viongozi wengi tuliozungukwa nao.
It's time for Dual Citizenship!!
Post a Comment