ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, August 26, 2014

Seif: CCM ilinisukuma kwenda upinzani

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad.PICHA|MAKTABA 
Dar es Salaam. Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesema CCM ndiyo iliyomsukuma kwenda upinzani kama inavyofanya sasa kwa aliyekuwa kada wake, Mansour Yusuf Himid.
Akizungumza katika mahojiano maalumu yaliyofanyika Dar es Salaam hivi karibuni, Maalim Seif alisema CCM inajiundia mashujaa watakaokuja kuipindua siku za usoni.
“Mimi sikuamua kuja upinzani, CCM ilinisukuma kama anavyopitia Mansour sasa hivi. Kweli Mansour anapitia vilevile nilivyopitia. Nilifukuzwa CCM, ilitafutwa tu sababu nikakamatwa na kuwekwa ndani. Mansour naye hakutoka CCM, wamemfukuza,” alisema Maalim Seif.
Mansour ambaye kabla ya kutimuliwa CCM alikuwa waziri asiye na wizara maalumu na Mwakilishi wa Kiembesamaki, alivuliwa uwaziri na baadaye uanachama kwa madai ya kukisaliti chama hicho.
Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) alisema bado Mansour hajajiunga na upinzani, lakini hutoa mchango wake wa mawazo katika majukwaa yake.
“Baada ya kufukuzwa akaona watu walio karibu na msimamo wake ni CUF. Hajajiunga rasmi mpaka leo lakini huja kwenye mikutano yetu kujieleza. Sasa wamemtia ndani, ipo siku watamtoa,” alisema Maalim Seif na kuongeza:
“Lakini ‘they are making him a hero, they create heroes themselves’ (wanamfanya awe shujaa, wanatengeneza mashujaa). Nakumbuka Mwalimu Nyerere (Julius) aliwahi kuulizwa na Sauti ya Ujerumani kwamba mambo gani anayojutia katika uongozi wake. Moja alisema ni kuitambua Biafra na jambo la pili ni kuwafukuza kina Maalim Seif.”
Akifafanua zaidi jinsi alivyofukuzwa kutoka CCM, Maalim Seif alisema Mwalimu Nyerere alifuata ushauri wa Idara ya Usalama wa Taifa ya Zanzibar ambayo ilimtaka Seif na wenzake wafukuzwe mara moja, huku idara hiyo upande wa Bara ikimwonya Mwalimu kutochukua hatua hiyo.
“Kikao cha Dodoma kilichoitishwa, kilikwenda mpaka saa sita usiku maana siku inayofuata Mwalimu alikuwa anasafiri na ilikuwa ni lazima tufukuzwe tu. Utetezi tulioutoa, hata Job Lusinde na marehemu Jamal walisema ‘mnawaonea tu vijana hawa, hawana kosa lolote’,” alisema.
Hata hivyo, alisema baada ya kufukuzwa alijiona kuwa yuko huru zaidi, huku akifungua ukurasa mpya wa kuwa nje ya uongozi wa Serikali.
“Kufukuzwa kwangu hakukuniuma, kwani nilijiona nitakuwa huru kufanya mambo yangu na hasa nilipoona ninaungwa mkono na Wazanzibari. Nilijiona kama nimepata baraka ya kuwa huru, wamenitesa, lakini nikaona ni mapambano, hakuna kukata tamaa,” alisema.
Alipoulizwa iwapo ana mpango wa kurudi CCM siku za usoni, Maalim Seif alihoji:
“CCM? Hii ya kina Nape? Afadhali ile yetu sisi ya enzi hizo. Kwa kweli haiwezekani. CCM ilikuwa ile ambayo Mwalimu ni Mwenyekiti, Kawawa (Rashidi) ni Katibu Mkuu, kina Kingunge (Ngombale Mwiru), Moses Nnauye, Salim Ahmed Salim, Alfred Tandau, ndiyo iliyokuwa sekretarieti. Siyo CCM hii... Kwa nini hasa nijisumbue kurudi CCM wakati chama chetu kinaendelea kuimarika?” alihoji.

Akanusha kumsaliti Jumbe
Kuhusu suala la kutofautiana na Rais wa Pili wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Aboud Jumbe ambapo Maalim Seif anadaiwa kumsaliti katika Halmashauri Kuu ya CCM hadi akaondolewa kwenye nafasi ya urais mwaka 1984, Maalim Seif amesema siyo kweli.
“Mimi sikupinga Serikali tatu. Wakati ule, Wazanzibari katika chama tuligawanyika. Kuna wale wazee (waasisi) wakijiita ‘Liberators’ kwa maana ndiyo walioleta mapinduzi, wakati huo mimi ni kijana. Hata Aboud Jumbe alipoleta Katiba ya mwanzo waliipinga. Lakini sisi vijana tukijiita ‘Front liners’ tulimuunga mkono,” alisema na kuongeza:
“Hata katika kugombea nafasi za Nec kulikuwa na makundi, haya yalikuwa yanagombana. Liberators walitaka sisi vijana tusiiingie kwenye Nec. Hata hivyo, walikuta vijana wamekuwa wengi zaidi. Hii iliwashtua Liberators.
“Wakahisi hawa vijana watachukua madaraka yao. Walimlaumu sana Jumbe kutuingiza kwenye madaraka, sisi tulimsaidia Jumbe kupitisha Katiba. Sasa fitina zikaanza, wanasema Waswahili papo kwa papo.”
Kutokana na uhasama huo wa makundi, Maalim Seif alisema kundi la Liberators lilizusha uongo kuwa amemsaliti Jumbe kwa kukataa Serikali tatu:
“Baada ya kutokea uchaguzi mkuu wa chama, Jumbe akaitisha kikao cha Unguja na Pemba mjini Dodoma. Katika hotuba yake ndiyo ilitushtua kwani alizungumzia muungano na mgawanyo. Mwisho akasema tunakwenda kwenye ‘revolutionary justice’ (mapinduzi ya haki). Hiyo ilitushtua maana tulishaona watu wakipoteza maisha,” alisema na kuongeza:
“Sasa mimi, Dk Salim Amour, Salim Ahmed Salim, wakati huo ni wajumbe wa Nec, tutachukua majukumu kwa upande wa Zanzibar. Tujue maana ya hii ‘revolutionary justice’. Tukaenda kwenye sekretarieti ya chama tukalijadili.
“Sasa kwa sababu Liberators walishindwa kutuzuia, ndipo walipokuja na suala la serikali tatu kutuengua. Nakumbuka hata marehemu Sokoine (Edward) alimwambia Mwalimu, vijana hawa wakija kupoteza maisha utawajibika. Sokoine alikuwa wazi sana, alikuwa Waziri Mkuu mwenye maamuzi na anayejiamini na mwenye nguvu.”
Maalim Seif alisema walilazimika kumruka Jumbe kwa kuwa hakuwashirikisha kikamilifu katika mpango wa mapinduzi aliyotaka kuyafanya:
“Kama kweli Jumbe alikuwa anataka mamlaka zaidi ya Zanzibar, sisi Wazanzibari wenzake kwa nini hakutuita walau tujadili na tuwe sehemu ya madai hayo, ili tukija kwenye Nec tuwe pamoja? Anafanya chini kwa chini? Kwa nini?”

Msimamo kuhusu Muungano
Maalim Seif amesisitiza msimamo wake katika muundo wa muungano kuwa ni Serikali ya mkataba. Hata hivyo, licha ya muundo huo kutoingizwa kwenye Rasimu ya Katiba Mpya, anasema bado ameheshimu uamuzi wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
“Serikali ya Mkataba ni rahisi sana, Tanganyika inakuwa na Serikali yake na Zanzibar Serikali yake. Kisha mnakaa pamoja na kuangalia mambo gani mwendeshe pamoja. Jeshi, Polisi na mambo mengine mnayoona kwa masilahi yenu kuyafanya pamoja,” alisema na kuongeza:
“Halafu siyo kuvunja muungano, haiwezekani leo kusema muungano usiwepo kabisa. Miaka 50 hii siyo michache, watu wamefanya mengi, wameshaoana sana. Lakini Wazanzibari leo wamebanwa, koti la muungano limetubana sana. Sasa tunataka tupime ili tupate koti ambalo haliwabani Tanganyika wala Zanzibar.”
MWANANCHI

2 comments:

Anonymous said...

CCM ya Nape Nnauye. You spoke the truth young man!.

Anonymous said...

CCM ya Abrahim Kinana haijawahi kutokea. Nape hakupi usingizi ndio maana unamponda. Kina Mwingulu ni vijana wenye dira na msimamo.