
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif RashidSerikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, imesema imejizatiti kukabiliana na ugonjwa wa Ebola kwa kuweka uangalizi maeneo ya mpakani na viwanja vya ndege vya kimataifa nchini.
Taarifa iliyotolewa na msemaji wa wizara hiyo, Nsachros Mwamaja, ilisema wataalamu hao watatoa elimu juu ya ugonjwa huo na namna ya kukabiliana nao.
Mwamaja alisema serikali pia imepeleka wataalamu wa afya katika maeneo yote ya mipaka ili kukagua wageni wanaoingia na kutoa elimu kwa wananchi.
Alisema mwaka 2012 ilivyoripotiwa kuibuka kwa virusi vya ugonjwa huo katika nchi za Afrika Magharibi na Uganda, wizara kupitia Bohari Kuu ya Dawa (MSD), ilisambaza vifaa na mafunzo kwa wataalamu hao kusaidia kubaini ugonjwa huo.
Alisema awali ugonjwa huo ulianza nchini Guinea na kusambaa katika nchi ya Sierra Leone, ambapo jumla ya wagonjwa 1,323 walibainika na kati yao 700 walifariki dunia.
“Tunapenda kuueleza umma wa Watanzania kuwa hadi sasa nchini hakuna mgonjwa aliyethibitika kuwa na virusi vya ugonjwa huo, hivyo tumejiandaa kuongeza zaidi vitendea kazi ili vianze ngazi ya chini,”alisema Mwamwaja.
Alisema wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa afya imeandaa mkakati wa kuzuia ugonjwa huo kwa kuunda kikosi kazi kitakachoshirikisha Shirika la Afya Duniani (WHO), pamoja na Shirika la Uswisi la Kimataifa la Maendeleo na Ushirikiano (MDC).
Alisema mwezi Machi, wizara kupitia WHO, ilipata taarifa ya kuingia kwa virusi vya ugonjwa huo katika nchi za Magharibi.
Alisema, serikali ilianza kuchukua hatua madhubuti ili kukabiliana nao kwa kudhibiti njia zinazoingia wageni toka nje ili wasiweze kuingia na virusi vya ugonjwa huo.
Kwa mujibu wa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid, serikali inaendelea kuweka uangalizi kwenye maeneo ya mipaka kwa lengo la kuwabaini watu wenye ugonjwa huo wasiweze kuruhusiwa kuingia nchini.
Dalili za Ebola ni homa kali, kulegea mwili, maumivu ya misuli, vidonda kooni, kuharisha damu, figo na ini kushindwa kufanya kazi, pamoja na kutapika mara kwa mara.
Ugonjwa huo ambao mpaka sasa haujapata tiba, umeshaua watu zaidi ya 700 huko Guinea na Sierra Leone.
Virusi vya ugonjwa huo viliripotiwa kuingia kwa mara ya kwanza Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo mwaka 1972.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment