ANGALIA LIVE NEWS

Monday, August 11, 2014

Shibuda maji ya shingo

Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda

Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda, amesema hatatetea kiti chake cha ubunge kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika uchaguzi mkuu mwakani kwa madai ya kuchoshwa na kauli za vitisho na kejeli zinazotolewa dhidi yake na baadhi ya viongozi wa chama hicho.

Alitoa kauli hiyo siku chache baada ya kudaiwa kuwa alijisajili kwa ajili ya kushiriki Bunge Maalumu la Katiba kinyume cha katazo na msimamo wa chama chake.

Pia amesema yeye si sehemu ya wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na kwamba hajawahi kuelimishwa juu ya Ukawa.

Shibuda aliyasema hayo kwa nyakati tofauti jana wakati akizungumza na wazee wa mji wa Maswa na Malampaka, Wilaya ya Maswa mkoani Shinyanga.

Wazee hao walitaka kujua hatima yake ya kisiasa ndani ya Chadema baada ya chama hicho kutishia kumfukuza kwa madai ya kushiriki vikao vya Bunge hilo vinavyoendelea mjini Dodoma.

Shibuda alisema alijiunga na Chadema kwa hiari yake akipinga dhuluma zilizokuwa zikifanywa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Alisema wakati anajiunga na Chadema, alidhani kuna demokrasia na ukombozi wa kweli, lakini alichokikuta ni tofauti kwani kila siku amekuwa akipata misukosuko kutoka ndani ya chama hicho.

Shibuda alisema amekuwa kimya muda mrefu na kwamba ilifika wakati baadhi ya vijana wa Chadema walimtukana matusi na kumdhalilisha kwa kumwita majina ya kuudhi, kama vile `msaliti' na `pandikizi wa CCM', huku viongozi wa ngazi ya juu wa chama hicho wakishindwa kuchukua hatua.

“Pamoja na shutuma zote zinazotolewa juu yangu na kupachikwa majina mbalimbali kuwa mie ni msaliti, mara ni pandikizi la CCM, lakini hata siku moja sijawahi kuitwa katika Kamati Kuu ya Chadema na kuhojiwa,” alisema Shibuda.

Aliongeza: “Nimekuwa nikitukanwa hadharani na vijana wa Chadema mbele ya viongozi wa juu wa chama, lakini hawachukui hatua. Mie mtu mzima. Hapo natafsiri kuwa wametumwa na viongozi hao ili kunifanyia fitina hizo.”

Akizungumzia madai ya kukiuka katazo la chama na Ukawa kushiriki Bunge hilo, Shibuda alisema hayana mashiko, kwani hajahudhuria kikao hata kimoja cha Bunge wala hajachukua posho.

Hata hivyo, alikiri kufika mjini Dodoma akitokea jijini Dar es Salaam akiwa njiani kuelekea jimboni kwake mjini Maswa.

Alisema alipita bungeni kufuatilia fedha za matibabu kutokana na kusumbuliwa na mguu.

Shibuda alisema akiwa katika ofisi za Bunge mjini Dodoma, alijaza fomu zinazohusiana na matibabu, kwani wabunge hutibiwa na serikali kupitia Ofisi ya Bunge kwa kipindi chote cha uhai wa ubunge wao.

Alisema tangu madai hayo yaanze kuandikwa na kutangazwa katika vyombo vya habari, hajawahi kuulizwa na kiongozi yeyote wa Chadema.

Hivyo alisema amesikitishwa na kauli ya Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu, ya kutishia kumfukuza katika chama hicho kwa tuhuma za usaliti na kwamba anaamini uongozi ni kutanguliza hekima na busara katika kufikia maamuzi.

“Uongozi si Magereza. Na hata magereza wafungwa wana haki zao. Tundu Lissu amekuwa nani katika nchi hii? Anaongea kama kasuku. Hafanyi utafiti. Anakurupuka na kuongea na kutoa matamko. Mie nitamtaka athibitishe tuhuma hizo anazozitoa dhidi yangu. Nasema Chadema si baba wala mama yangu,” alisema.

Alisema amechoka kusikia hukumu dhidi yake kila siku kupitia vyombo vya habari zinazotolewa na viongozi wake wa Chadema.

Alitoa mfano akisema alipounga mkono nyongeza ya posho ya vikao vya Bunge, aliitwa msaliti, lakini leo wabunge wote wakiwamo wa Chadema waliogomea, wanachukua posho hiyo.

Alisema yeye si sehemu ya Ukawa na wala hajawahi kuelimishwa juu ya umoja huo, bali anachokumbuka ni kuwa kupitia viongozi wa juu wa vyama vya upinzani vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi, walikubaliana katika kikao kuwa wabunge wa vyama hivyo kususia Bunge hadi hapo rasimu iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba itakapojadiliwa.

“Mwislamu hawezi kutetea Uislamu kama hajui nguzo tano za Uislamu. Na pia huwezi kuwa Sheikh bila kupitia madrasa. Na hata katika Ukristo, huwezi kuutetea Ukristo kama hujui Biblia na hukusoma mafundisho. Na mie siwezi kuwa Ukawa wakati sijaelimishwa juu ya kundi hilo,” alisema Shibuda.

Akijibu moja ya maswali ya wazee ni chama gani ambacho atagombea ubunge katika uchaguzi mkuu ujao, alisema wakati ukifika atasema.

Alisema kwa sasa bado anatimiza wajibu wake wa kuwatetea wapigakura wake ambao wengi wao ni wakulima na wafugaji na kwamba yuko tayari kufukuzwa Chadema kwa kuwatetea (wapigakura wake).

Wakati Bunge Maalumu la Katiba likiendelea na vikao vyake mjini Dodoma, baadhi ya wajumbe wanaodaiwa kutoka Ukawa wamehudhuria vikao hivyo lakini wamekanwa na vyama vyao na wengine kuonywa kwa usaliti.

Ijumaa wiki iliyopita, Lissu aliwaambia waandishi wa habari kuwa Kamati Kuu (CC) ya Chadema itawachukulia hatua wasaliti wote.

Alisema hatua za wasaliti wa Ukawa kwenda bungeni zitatolewa wakati wowote na CC kwa kuwa haimuogopi mtu.

Pia alisema CC haichezewi wala haipendi makaidi, hivyo muda utakapofika maamuzi dhidi yao yatafanyika.

Wakati Lissu akitoa kauli hiyo, tayari wajumbe sita wanaounda Ukawa wakiwamo wa Chadema, wameripotiwa kushiriki katika vikao vya Bunge hilo.

Akijibu kuhusu wabunge wanaounda Ukawa kuendelea kumiminika bungeni na kuonekana wakisaini posho za vikao vya Bunge, Lissu ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki, alisema CC ndiyo yenye kutoa adhabu dhidi ya wanaohudhuria vikao hivyo.

“Hatumuogopi Shibuda, Leticia wala nani kwa sababu hatuna tabia ya kulea Yuda Iskariote, na kama watakimbilia mahakamani kama mwenzao ni vyema kuwa wabunge wa mahakama,” alisema Lissu.

Aliongeza: “Leticia Nyerere, Saidi Arfi na John Shibuda tunafahamu wamesaini posho zao, watatueleza muda ukifika.”

Katibu wa Bunge Maalumu, Yahaya, alisema kuwa hadi kufikia Alhamsi wiki iliyopita, tayari kulikuwa na ongezeko la wajumbe wa Ukawa kutoka wawili hadi kufikia sita; watatu wakitoka Chadema na wengine kutoka makundi mengine.

Wajumbe kutoka Chadema wanaodaiwa kukaidi maamuzi ya Ukawa kwa kujiandikisha kwa ajili ya kuhudhuria vikao vya Bunge hilo, kuanzia Agosti 5, mwaka huuni Shibuda, Mbunge wa Viti Maalum, Leticia Nyerere na Said Arfi, ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa zamani wa Chadema, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mpanda Kati.
CHANZO: NIPASHE

No comments: