ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, August 12, 2014

Shibuda: Mimi siyo kubwa jinga

Mbunge wa Maswa Magharibi (Chadema),John Shibuda.

Mbunge wa Maswa Magharibi (Chadema), John Shibuda amesema katika suala la Katiba Mpya hawezi kuitwa ‘kubwa jinga’ na hataweza kuunga mkono hoja za Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wa kutaka muundo wa serikali tatu.

Akizungumza na wazee wa mji mdogo wa Malampaka mjini hapa, Shibuda alisema haelewi maana ya neno Ukawa kama mnyama ama la, bali hatokuwa ‘kubwa jinga’ kwani hoja za serikali tatu hazina mashiko kwake.

“Nafahamu wajibu wangu kama mbunge, nitasimamia maslahi bungeni na kuunga mkono serikali mbili na kamwe si tatu zinazopigiwa kelele na Ukawa,” alisema Shibuda.

Alisema anarejea bungeni kuungana na wajumbe wa bunge hilo la katiba kuhakikisha anasaidia kuwapo kwa serikali mbili ambazo alidai zitasaidia hatma ya Zanzibar na kudumu kwa Muuganno wa Bara na Visiwani.

Alisema chanzo cha kuwapo kwa Ukawa ni kwa CCM kutokuwa wa wazi na wakweli kwa viongozi na wabunge wake hali ambayo imesababisha kuwepo kwa Ukawa inayong’ang’ania kuwepo kwa serikali tatu.

Shibuda alisema haungi mkono kuwapo kwa serikali tatu kwa kile alichodai kutowatendea haki Wazanzibar na ni bora kukawa na serikali moja kuliko tatu.

Katika kuhakikisha hilo, mbunge huyo ambaye ametangaza kujiondoa Chadema, alisema hatawatendea haki Wazanzibar iwapo atawaunga mkono Ukawa.

“Siyo kubwa jinga miye, siwezi kukubali kuwaumiza wazanzibar hao ambao ni ndugu zetu, kuna wanyamwezi, waha na wasukuma huko visiwani kabla na baada ya biashara ya utumwa,” alisema.

Shibuda alisema faida kubwa ya Ukawa ni mambo ya Zanzibar na siyo maslahi ya Watanzania ambao alisema kwa historia wanatoka Bara kabla ya biashara ya utumwa.

Akizungumzia misimamo yake baada ya kurejea katika bunge maalum la katiba, Shibuda alisema anapeleka nguvu mpya kwa wajumbe wa wanaotetea haki za wafugaji na wakulima ndani ya bunge hilo.
CHANZO: NIPASHE

No comments: