ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, August 14, 2014

TANZANIA YAADHIMISHA MIAKA 100 TANGU KUANZA KWA VITA KUU YA KWANZA YA DUNIA

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akiwa na Wawakilishi wa Nchi zilizoandaa hafla hiyo
Mhe. Ramadhan M. Mwinyi, Kaimu Mwakilishi ... asilisha hotuba yake kwenye hafla hiyo

NA MWANDISHI MAALUM, NEW YORK, 13 Agosti 2014

Katika kuadhimisha miaka 100 ya kuanza kwa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, Tanzania, Ubelgiji, Ugiriki, Iraki, Kenya, Nigeria na Afrika Kusini zimeungana na India katika hafla iliyoendana na uzinduzi wa kitabu cha picha za kumbukumbu za wapiganaji waliofariki kwenye vita hiyo kuanzia mwaka 1914 – 1918.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, iliyofunguliwa na Mhe. Ban Ki-moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Mhe. John W. Ashe, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kuhudhuriwa na Wawakilishi wa nchi mbalimbali Wanachama wa Umoja wa Mataifa, Mhe. Ramadhan M. Mwinyi, Kaimu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania amesema kitabu hicho ni mchango muhimu katika historia ya vita hivyo, vilivyosababisha maafa makubwa katika mabara ya Ulaya, Asia na Afrika, ambapo jumla ya watu milioni 16 walifariki dunia na wengine milioni 20 kupata majeraha makubwa.


Balozi Mwinyi alitumia fursa ya hafla hiyo kuikumbusha jumuiya ya kimataifa, wajibu wa kizazi cha sasa, kuendelea kusisitiza umuhimu wa utatuzi wa migogoro kwa njia ya mazungumzo kama ilivyoainishwa kwenye Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa mwaka 1945.

Akizungumza kwa hisia kali, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alisema hata baada ya athari kubwa za Vita Kuu mbili za Dunia, Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa hazijajifunza umuhimu wa kuepusha vita na migogoro. Matokeo yake, dunia imeendelea kugubikwa na migogoro mbalimbali ambayo imesababisha vifo, majeruhi, uharibifu mkubwa wa miundo mbinu na mazingira.

Naye Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa alihoji kama Vita hivyo vilipaswa kuitwa Vita Vikuu, badala yake alisema vingeitwa Janga Kuu la dunia. Rais huyo alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa nchi zote za Umoja wa Mataifa katika kuzuia na kutatua migogoro.

Tanzania bara, wakati huo ikiwa chini ya himaya ya wakoloni wa Kijerumani, iliguswa na vita hivyo vilivyopiganwa na watawala wa Kijerumani na Waingereza katika maeneo ya Afrika Mashariki. Inakadiriwa kuwa, wanajeshi na raia takriban elfu hamsini wa eneo hilo walipoteza maisha katika vita hivyo. Miongoni mwao ni wanajeshi wa Kihindi ambao walipigana upande wa Waingereza. Minara ya kumbukumbu pamoja na makuburi ya wanajeshi hao ipo Dar es Salaam, Taveta naTanga.

Tanzania ilisisitiza kuwa, ni vyema kuwakumbuka wengine wengi ambao walipoteza maisha wakati na baada ya vita, kutokana na maradhi na njaa. Pia ilitaja maeneo mengine ambayo ni kumbukumbu ya vita hivyo kama vile sanamu ya askari (Askari Monument) iliyopo katikati ya jiji la Dar es Salaam na Kariakoo, ambako waliishi wanajeshi wa Kihindi waliojulikana kwa Kiingereza kama “Carrier Corps”.

No comments: