Dar es Salaam. Kete ya mwisho ya kuamua iwapo wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) watarejea katika Bunge la Katiba au la itachezwa leo katika kikao cha maridhiano baina ya umoja huo na CCM, chini ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi.
Kikao hicho kinafanyika siku nne kabla Bunge hilo kuendelea na vikao vyake Jumanne ijayo licha ya msimamo wa Ukawa wa kuendelea kuvisusia.
Kikao hicho kinachovikutanisha vyama vya NCCR-Mageuzi, Chadema, CUF na CCM ni cha mwisho baada ya kile cha kwanza kilichofanyika wiki moja iliyopita kumalizika bila mwafaka wowote.
Akizungumza na waandishi wa habari jana akiwa na wenyeviti wenzake, James Mbatia (NCCR-Mageuzi) na Profesa Ibrahim Lipumba (CUF), Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema hadi jana msimamo wao ni kutohudhuria vikao vya Bunge hilo labda ikitokea miujiza katika kikao cha leo.
Mbowe alisema ni miujiza kwa sababu kwa madai ya Ukawa, ni lazima mjadala huo ujikite kwenye Rasimu ya Katiba, ambayo imebeba mapendekezo ya wananchi na kutaka wajumbe wenzao, hasa kutoka CCM, kuacha kujenga hoja kwa kutumia kejeli, matusi na mizaha ambayo si rahisi wenzao kuyakubali.
Moja ya ajenda ya kikao hicho ambacho leo kitakuwa na wajumbe 20 kutoka kila chama, ni kuwashawishi Ukawa kurejea bungeni ili kuendelea na mchakato wa Katiba Mpya.
Ukawa walisusia vikao vya Bunge la Katiba hilo Aprili 16 wakipinga kubadilishwa Rasimu ya Katiba na wajumbe wa CCM kwa maelezo kuwa ni kinyume na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Mbowe alisema ni jambo la kushangaza kuona Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta wakitoa kauli za kuwashutumu Ukawa wakati wakijua wazi kuwa kuna mazungumzo kati ya vyama vya siasa na Jaji Mutungi vinaendelea.
Juzi pia, Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), liliisihi Ukawa kurudi bungeni ili kukamilisha mchakato wa kupata Katiba Mpya, lakini likasema mjadala huo uzingatie Rasimu ya Katiba.
“Hata viongozi wa dini nao wametoa matamko wakitaka Ukawa turejee bungeni, tunashukuru maoni yao. Ila wanatakiwa kujua sababu zilizotufanya mpaka tukasusia. Wanatakiwa kuwaonya CCM wanaokwenda kinyume na mchakato huo,” alisema Mbowe na kuongeza:
“Wakati tupo katika mazungumzo, Sitta anaanzisha kikao chake na kutoa tamko kuwa Bunge litaendelea wakati akijua Ukawa wapo katika kikao pamoja na viongozi wa chama chake cha CCM. Kauli hizi zinazokosa umoja zinaonyesha Serikali na timu nzima haiko tayari kutafuta mwafaka wa suala hili.”
Profesa Lipumba
Akieleza sababu nyingine za Ukawa kususia vikao vya Bunge la Katiba, Profesa Lipumba aliwataka viongozi wa dini kutambua kuwa CCM ndiyo chanzo cha mchakato huo kuingia dosari, kwamba wanatakiwa kukionya chama hicho kiheshimu maoni ya wananchi.
“Tuliondoka bungeni kwa sababu Sitta alishindwa kuwadhibiti wajumbe wa Bunge la Katiba waliokuwa wakizungumza lugha za matusi, kejeli, uchochezi na ubaguzi, alivunja kanuni za Bunge kwa kuruhusu Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba kuwasilisha Rasimu ya Katiba bungeni kabla ya Bunge kusikiliza hotuba ya ufunguzi ya Rais Jakaya Kikwete.”
Alitaja sababu nyingine kuwa ni kauli ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi kueleza kanisani kuwa nchi itaingia vitani iwapo muundo wa serikali tatu utapita, kwamba Zanzibar inataka serikali tatu ili kurejesha Waarabu visiwani humo.
“Lukuvi aliyasema hayo kanisani akimwakilisha Waziri Mkuu Pinda. Licha ya kutoa maneno ya uchochezi hakuna mamlaka iliyo juu ya Lukuvi iliyoomba radhi kwa kauli yake,” alisema.
Mbatia
Mbatia alisema rasimu inayotakiwa kujadiliwa ni ile iliyopendekezwa na Tume ya Warioba yenye muundo wa Serikali tatu.
“Hata kuhusu Tunu za Taifa zilizotajwa katika rasimu; yaani utu, uzalendo, uadilifu, uwazi, umoja, uwajibikaji na lugha ya taifa wenzetu wa CCM wameyakataa. Sasa sijui wanataka kulipeleka wapi hili taifa. Tutaendeleaje kujadili?” alihoji.
Hofu ya wajumbe
Katika hatua nyingine, baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo wamesema kutorejea bungeni kwa Ukawa kutaathiri upatikanaji wa Katiba Mpya yenye maridhiano.
Mmoja wa wajumbe hao, Charles Mwijage alipendekeza kusitishwa kwa mchakato huo kwa kuwa maridhiano ni jambo muhimu katika kutengeneza Katiba.
“Kukosekana kwa Ukawa bungeni kutaathiri upatikanaji wa Katiba Mpya kwa sababu suala hili linahitaji zaidi maridhiano ya pande zinazotofautiana kiitikadi,” alisema Mwijage ambaye pia ni Mbunge wa Muleba Kaskazini (CCM).
“Ningekuwa na uwezo, ningeamua mchakato huu wa Katiba usitishwe na tuendelee kutumia Katiba iliyopo kwa sababu suala hili linahitaji zaidi maridhiano,” alisema.
Mbunge huyo alisema, “Ukawa wanataka kujenga mazingira ya kuja kuikataa Katiba itakayopatikana ili watusababishie vurugu na mapigano.”
Alisema Rais aliona kwamba kundi la wajumbe 629 likikaa pamoja linaweza kutengeneza Katiba Mpya kwa maridhiano, lakini kama kuna kundi linajitoa ni wazi kwamba kutakuwa na dosari katika utengenezaji.
Mjumbe mwingine, Ezekiah Oluoch alisema iwapo wajumbe wa CUF kutoka Zanzibar ambao wanaunda Ukawa hawatarejea bungeni, Katiba Mpya haiwezi kupatikana kwa sababu theluthi mbili haziwezi kupatikana.
“Katiba haipatikani kwa ubabe au wengi-wape, bali inapatikana kwa maridhiano na mwafaka bila kujali idadi ya wingi wa wajumbe,” alisema Oluoch ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT).
Alisema Bunge hilo litatumia fedha nyingi za walipa kodi bila kupata Katiba Mpya, hivyo akashauri mchakato huo usogezwe mbele hadi baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Mbunge wa Mbeya Vijijini (CCM), Lackson Mwanjali alisema kitendo cha Ukawa kukataa kurejea bungeni ni pigo katika mchakato wa Katiba Mpya kwa sababu inatengenezwa kwa majadiliano na kufikia mwafaka.
“Tunapokuwa bungeni watu kutoka vyama na itikadi tofauti tunajadiliana, tunabishana na baadaye kufikia mwafaka na kufanya maridhiano, sasa wenzetu hawapo ni tatizo kubwa,” alisema.
Mwanjale alisema ingawa wanakwenda kwenye Bunge Maalumu la Katiba itakuwa vigumu kupata Katiba bora.
Hata hivyo, Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Diana Chilolo alisema wangependa Ukawa warejee bungeni lakini kama hawaendi watawakilishwa na wenzao.
“Wapo watu kutoka katika vyama vya upinzani pale ambao watawawakilisha. Yupo Mbunge wa Vunjo (TLP), Augustine Mrema na Mbunge wa Bariadi Mashariki (UDP), John Cheyo watawawakilisha na tutapata Katiba bora,” alisema Chilolo.
Mbunge wa Sikonge (CCM), Saidi Mkumba alisema Katiba inayotafutwa ni ya Watanzania wote hivyo kundi la Ukawa kukataa kurudi bungeni hakuwezi kusimamisha mchakato huo.
Mambo sita ya kuzingatia
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Khoti Kamanga amebainisha mambo sita yanayotakiwa kufanyiwa kazi kabla ya Bunge hilo kuanza vikao vyake Agosti 5.
Akizungumza katika kilele cha Siku ya Wanawake Afrika iliyoandaliwa na Shirika la Wanawake Katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika (WilDAF), Dk Kamanga alisema:
“Mosi, huu utaratibu wa wengi-wape ni mzuri lakini tusiung’ang’anie ingawa demokrasia inaruhusu na kinachotakiwa ni kuweka mbele masilahi ya taifa.”
“Kuna wachache wanakuwa na hoja za kutosha lakini kutokana na uchache wao demokrasia inawatupa. Katika suala la Katiba maridhiano ni jambo la muhimu na suala la wengi-wape liwekwe kando.”
Pili, alisema Sheria ya Mabadiliko ya Katiba inatakiwa kufanyiwa marekebisho hasa Kifungu cha 36 (5) kilichobainisha kuwa endapo mwafaka hautapatikana Katiba ya mwaka 1977 itaendelea kutumika.
“Unapoanza safari huwezi kushindwa na ukarudi nyuma, kwa kuwa kila mmoja amekiri kwamba Katiba ya sasa ina viraka 14 ambavyo ni vingi sana,” alisema.
Jambo la tatu, Dk Kamanga alisema kunahitajika ujasiri katika kubaini na kukubali ni wapi mchakato wa Katiba ulipojikwaa. Sheria ya Mabadiliko ya Katiba inatakiwa kuheshimiwa na si kukiukwa.
Jambo la nne ni kuwa, Bunge linatakiwa kujadili rasimu na kutokwenda kinyume na sheria ilivyo kama ilivyoandaliwa na Tume ya Katiba kwa mujibu wa sheria.
“Rasimu iliyopo ya Desemba 2013 iliandaliwa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba iliyounda Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokusanya maoni ya wananchi, hivyo sheria haitakiwi kuvunjwa, pia Bunge linatakiwa kuizingatia,” alisema.
“Tano, tunatakiwa kusoma rasimu ili unapochangia au kuona mtu akichangia uwe unajua anachokisema na jambo la mwisho ni ngumu kwa vyama kuweka kando masilahi yao lakini kwa jambo hili wanatakiwa kutanguliza mbele masilahi ya taifa,” alisema Dk Kamanga.
Imeandikwa na Fidelis Butahe, Raymond Kaminyoge na Ibrahim Yamola wa Mwananchi
No comments:
Post a Comment