Advertisements

Friday, August 29, 2014

UNAPOKUWA FARAGHA NA MWENZA WAKO, NI MAZUNGUZO GANI YANAFAA?

Ni matumaini yangu kwamba mpenzi msomaji wangu uko poa na unaendelea na majukumu yako kama kawaida.Ni wakati mwingine tunapokutana katika busati letu la mahaba, tukijuzana mambo mbalimbali yahusuyo uhusiano wa kimapenzi baina yako na mkeo/mumeo, mchumba au mpenzi.

Hivi mkiwa wawili na mpenzi wako, katika mazungumzo ya kawaida huwa mnazungumza nini? Yawezekana ukaliona swali hili kama jepesi lisilo na maana lakini ukweli ni kwamba mazungumzo ni kiungo muhimu sana kati yako na umpendaye.

Utafiti wa wataalamu wa mapenzi umebaini kwamba, wengi wetu huwa tunavunja mapenzi kati yetu na tuwapendao kwa kushindwa kuelewa nini tunapaswa kuzungumza na kipi hatutakiwi kabisa kuzungumza hata kama ni katika mazungumzo ya kawaida.

Naileta mada mezani, nataka tujadiliane nawe msomaji wangu kwani naamini mimi si mjuaji wa kila kitu, lazima na wewe utakuwa unajua kwani wengi wetu tunaishi katika uhusiano wa kimapenzi, kama siyo ndoa basi itakuwa uchumba au u-boyfriend na u-girlfriend.
Hebu niambie huwa unazungumza nini na mpenzi wako? Hakuna muda ambao huwa unahisi umeishiwa mada za kuzungumza na umpendaye?

WENGI WANAKOSEA HAPA
Ukitaka uhusiano wako uwe na furaha siku zote, mbali na mambo mengine, unapaswa sana kuuchunga ulimi wako! Usiwe mtu wa kuzungumza hovyo, mara umeanzisha mada hii haijaisha unahamia nyingine, huo siyo utaratibu mzuri na muda si mrefu utajikuta ukimchosha mpenzi wako.

Pia epuka kuwa unazungumzia mapenzi muda wote! Lazima umfanye mpenzi wako kuwa rafiki yako na jambo pekee linaloweza kuwavuta karibu ni mazungumzo ya kawaida. Upo muda wa kuzungumzia mapenzi lakini upo pia muda ambao mnatakiwa kuwa na mazungumzo ya kawaida.

Ni makosa kutumia muda wako kuzungumzia uhusiano wako na mpenzi au wapenzi wa zamani kwani ni jambo linaloweza kumharibia mudi mpenzi wako haraka. Pia epuka kuwa unazungumzia mapenzi ya watu wengine, iwe ni kwa mazuri au kwa mabaya.

Zingatia kutokuwa muongeaji peke yako mkiwa na mwenzako bali tumia njia shirikishi kwa kumuuliza maswali mepesi ili kumpa nafasi kila mmoja kushiriki kikamilifu katika mazungumzo yenu badala ya wewe kuwa mzungumzaji peke yako.

ZINGATIA HAYA
Zifuatazo ni mada mbalimbali unazoweza kuzungumza na mwenzako na akajisikia furaha kuwa na wewe, bila kujali mmekaa pamoja kwenye uhusiano kwa muda gani. Hata kama mtakaa siku nzima, hatakuchoka na atatamani muendelee kukaa karibu.
Tunajua kwamba kutoana ‘out’ hasa mwishoni mwa wiki ni jambo linaloimarisha sana mapenzi. Hebu muulize mpenzi wako, mtakapotoka kwa mara nyingine anataka muende sehemu gani ambayo ataifurahia.

Hata kama ndiyo kwanza Jumatatu na wikiendi ipo mbali, muulize tu kisha msikilize atakavyokujibu. Pangeni pamoja siku hiyo itakavyokuwa na hiyo itawasaidia nyote wawili kuimaliza wiki kwa shauku kubwa ya kuisubiri siku husika. Hatachoka kukusikiliza na hakikisha unatimiza ahadi hata kama ni kwa kiwango kidogo.

Muoneshe kwamba ana mambo mengi yanayokufurahisha. Mkumbushe mambo aliyokufanyia siku za karibuni ambayo bado unayakumbuka na kuyafurahia. Utamfanya ajisikie furaha ndani ya moyo wake na atakuwa na hamu ya kukusikiliza na kukufanyia mengine mazuri zaidi. Hata kama alikununulia soksi au kitambaa cha mkononi, mueleze jinsi ulivyokifurahia.

Muulize kuhusu vitu anavyoviogopa au vinavyomfanya akose amani (hasa wanawake). Hata kama akikwambia vitu vidogovidogo, mfano anamuogopa mbwa wa jirani kwani huwa anamtishia kila siku akipita, au anaogopa mende waliopo kwenye kabati lake la nguo, moyoni atafurahi kwa sababu atajua yupo mtu anayemjali na ambaye yupo tayari kumlinda.

Zungumzieni kuhusu kazi. Kama nyote mmeajiriwa, anza kwa kumueleza mambo yanayokukera kazini kwenu, mfano ukali wa bosi wako au umbali kisha utamsikia na yeye akizungumza yake. Kama mmoja wenu hafanyi kazi, jenga mazoea ya kumsimulia jinsi siku yako ilivyokuwa ukiwa kazini au nyumbani. Itamfanya ajihisi ana umuhimu mkubwa kwako.

Msimulie ndoto za maisha yako, labda kwa mfano unapenda kufikia wapi baada ya mwaka mmoja, miwili au mitano ukiwa naye. Hiyo itamjenga na kumuaminisha kwamba kumbe atakuwa na maisha marefu na wewe, jambo litakalozidi kumfanya akupende.

Tukutane wiki ijayo kwa mwendelezo wa mada hii nzuri. GPL

No comments: