Kepteni Mstaafu Alhaji Mohamed Ligora (katikati) akisisitiza umuhimu wa kupata Katiba bora ya nchi wakati akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam. Kushoto ni Mzee Sheikh Yahaya Ngoma na kulia ni Mzee Alhaji Sheikh Bakari Chiwaka.
Kepteni Mstaafu Alhaji Mohamed Ligora akisisitiza (katikati) umuhimu wa kupata Katiba bora ya nchi wakati akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam. Kushoto ni Mzee Sheikh Yahaya Ngoma na kulia ni Mzee Alhaji Sheikh Bakari Chiwaka.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Assah Mwambene akiwasikiliza
Wazee wa mkoa wa Dar es salaam mara baada ya mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam. Picha zote na Eleuteri Mangi-MAELEZO
Na Immaculate Makilika –MAELEZO_DAR ES SALAAM
WAZEE wa Mkoa wa Dar es salaam wamewaomba Umoja wa Katiba wa Wananchi (UKAWA) kurudi Bungeni ili kuendelea na mchakato wa majadiliano ya Rasimu ya Katiba Mpya yanayoendelea.
Wazee hao wamesema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati wakizungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya siasa nchini pamoja na Bunge la Katiba Mpya linaloendelea mjini Dodoma.
Akizungumza kwa niaba ya Wazee wenzake Kepteni Mstaafu Alhaji Mohamedi Ligora , amesema kuwa Tanzania ni nchi nzuri na watu wake ni wazuri ni vema UKAWA na wenzao wakarudi Bungeni kujadiliana ili watimize matakwa ya kidemokrasia.
Amesema kuwa wananchi wa Tanzania hawataki kufananishwa na nchi zingine zilizofanya makosa na kupata matatizo kutokana na mambo kama haya ambayo yalisababisha wananchi wao kuzikimbia nchi zao kwa mambo ambayo wangeweza kukaa chini na kumaliza wenyewe kwa ajili ya maslahi ya umma.
Kapteni Mstaafu Alhaji Ligora amesema kuwa suala la mchakato ni suala la kidemokrasia, hivyo ni vyema UKAWA wakatumia fursa hiyo waliyonayo kwa kurudi Bungeni na kuendelea na majadiliano kuhusu Rasimu ya Katiba hali itakayosaidia kupatikana kwa Katiba Mpya ambayo itakuwa na manufaa kwa wananchi wa Tanzania.
Aidha, amewaomba wajumbe walio Bungeni na wale walio nje ya Bunge kuacha kuwazomea UKAWA badala yake wawasihi warudi katika chombo rasmi cha kuboresha Rasimu ya Katiba Mpya.
Naye Mzee Ali Bakari Muki, amewataka UKAWA kuheshimu misingi ya demokrasia lakini pia amewapongeza wabunge walioitikia wito wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kurudi Bungeni na kuendelea na majadiliano kuhusu Katiba kwani ndio Jukwaa pekee la kuwapatia wananchi Katiba bora.
Kwa upande wake Mzee Yahaya Ngoma amewataka viongozi wote hasa UKAWA kuheshimu na kudumisha jitihada zilizofanywa na waasisi wa Taifa hili akiwemo Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere pamoja na Sheikh Abeid Amani Karume kwa kuzingatia misingi na kanuni za uongozi bora kwa kutumia njia ya majadiliano pale panapokuwa na mawazo tofauti baina yao.
Halikadhalika, Alhaji Sheikh Bakari Chikawa amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuridhia kuanza kwa mchakato wa Katiba Mpya na kusisitiza ni moja ya tunda la uongozi bora na demokrasia nchini.
Aidha, ameongeza kuwa UKAWA ni vema wakatumia fursa hiyo ya demokrasia kwa kuwawakilisha vema wananchi wa Tanzania ili kuhakikisha wanapata Katiba Bora.
Alhaji Chikawa amewaomba UKAWA kurudi Bungeni kwani kunyume na hivyo ni watakua wametenda dhambi na madhara yake ni makubwa sana, na kusisitiza kuwa mazungumzo ni muhimu na yakipuuzwa basi kuna madhara.
No comments:
Post a Comment