Advertisements

Monday, September 8, 2014

Askofu Kakobe: Kinachoendelea Katika Bunge la Katiba ni Uhuni Mkubwa

Kabla ya mahubiri ya Neno la Mungu katika Ibada Kuu ya leo Jumapili 7.9.2014, Mwenge, Dar-Es-Salaam; Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Askofu Zachary Kakobe, alianza kwanza kusoma kwa waumini wote Tamko zima la Jukwaa la Wakristo Tanzania kuhusu Mchakato wa Katiba. Alisema kwamba Kanisa la FGBF linaunga mkono tamko hilo, siyo kwa asilimia 100%, bali kwa asilimia 200%. "Tamko hili limekuwa likisomwa katika Makanisa ya Katoliki, KKKT, na mengineyo kuanzia Jumapili iliyopita, na leo nitalisoma kwenu, neno kwa neno. Wakati umepita wa Wakristo kugawanywa, ili Shetani atawale. Tofauti zetu Wakristo tunaziweka pembeni, tunaunganishwa na msalaba. Jukwaa la Wakristo Tanzania linawaunganisha wote wanaoamini juu ya msalaba - TEC, CPCT, CCT na SDA. Hivyo kauli ya Jukwaa la Wakristo Tanzania, ni kauli ya FGBF, kwa sababu sisi tuko ndani ya CPCT."
Aliendelea kusema,"Kama tamko la Jukwaa la Wakristo Tanzania linavyosema, Rasimu ya Pili ya Katiba ni Waraka halali na rasmi, na ndiyo mawazo ya Watanzania. Katiba ni ya Wananchi na inahitaji maridhiano, na siyo ubabe. Huu ndiyo pia msimamo wa Kanisa la FGBF. Kinachoendelea sasa katika Bunge Maalum la Katiba, ni uhuni tu wa mchwa wanaotafuna fedha za Watanzania bila huruma kwa wananchi wasio na uwezo hata wa kununua dawa ya Malaria", alisema Askofu Kakobe. Baada ya kusoma tamko la Jukwaa la Wakristo Tanzania, la Agosti 28, 2014, aliwauliza waumini,"Anayeunga mkono tamko hili asimame na kupunga mikono yake." Ndipo wote Kanisani maelfu kwa maelfu waliposimama na kupunga mikono yao huku wakishangilia. Kisha Kakobe akasema, "Pamoja na umuhimu wa maombi, haitoshi tu kuomba. Baada ya kufunga na kuomba, Esta alichukua hatua ya kumwambia ukweli Mfalme. Pamoja na maombi, hatua ya Jukwaa la Wakristo Tanzania kutoa sauti ya Kinabii kama hii, ni muhimu, ili mwenye masikio asikie."

Alimaliza kwa kusema,"Wapuuzeni watu wanaosema kwamba kufanya hivi ni kuchanganya dini na siasa! Katiba siyo siasa, ni zaidi ya siasa. Siasa imo ndani ya Katiba, lakini ndani ya Katiba kuna mambo mengi pia ambayo siyo siasa, kama vile Dini, Majeshi, Mahakama, Elimu, Kilimo, Ardhi, Ufugaji, Haki za binadamu n.k. Kwa ujasiri wote, kila Mkristo apaze sauti yake kukemea uhuni unaoendelea katika Bunge la Katiba, mpaka masikio ya walioko huko yazibuke!"

1 comment:

Anonymous said...

Angelisema mzanzibari angeitwa gaidi na kupelekwa gerezani keko akachumishwe mboga na polisi. Sema askofu usiogope.