ANGALIA LIVE NEWS

Monday, September 29, 2014

IGP ERNEST MANGU NINGENG’ATUKA

Kwako Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Ernest Mangu.
Ni matumaini yangu kwamba hunifahamu na sitegemei kama kuna mazingira yanayoweza kunikutanisha nawe ndiyo maana nimeamua kutumia ukurasa huu kufikisha ujumbe wangu kwako.
Mimi si mtoto wa Mzee Jumbe Mangu na mama Mwanaidi Msengi kama wewe. Sikuzaliwa mwaka 1959 kwenye Kijiji cha Kihunadi, Tarafa ya Ilongero mkoani Singida wala sikusoma Shule ya Sekondari ya Tumaini kama wewe! Mimi ni raia wa kawaida tu, mlala hoi.
Nakuhakikishia kuwa sijawahi kupitia mafunzo ya Jeshi la Polisi katika Chuo cha Polisi Moshi (CCP) kama wewe, sikusomea mafunzo ya sheria kwa ngazi ya cheti pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na baadaye kutunukiwa Shahada ya Kwanza ya Sheria katika chuo hicho kama wewe wala sijawahi kwenda kusoma nchini Marekani.

Sijawahi kuwa Koplo wa Polisi, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Mkaguzi wa Polisi, Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Mrakibu wa Polisi na kuendelea kupanda ngazi hadi kuwa Kamishna wa Polisi mwaka 2013 kama wewe. Mimi ni mlala hoi tu, ambaye mlo wangu mmoja wa siku ni kitendawili.

Hata hivyo, licha ya ulofa wangu, ningekuwa kwenye nafasi yako, ya Mkuu wa Jeshi la Polisi kama wewe, kwa haya yaliyotokea na yanayoendelea kutokea, hakika ningeng’atuka!
Japokuwa nimeshakwambia kwamba mimi ni mlala hoi wa kawaida, angalau naijua kidogo katiba ya nchi.

Najua kwamba Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 27 (1)-(2) inasema waziwazi kwamba: “ Kila mtu ana wajibu wa kulinda mali asilia ya Jamhuri ya Muungano, mali ya mamlaka ya nchi na mali yote inayomilikiwa kwa pamoja na wananchi, na pia kuiheshimu mali ya mtu mwingine. 
“Watu wote watatakiwa na sheria kutunza vizuri mali ya mamlaka ya nchi na ya pamoja, kupiga vita aina zote za uharibifu na ubadhilifu (kama unaoendelea kwenye Bunge Maalum la Katiba), na kuendesha uchumi wa taifa kwa umakini kama watu ambao ndiyo waamuzi wa hali ya baadaye ya taifa lao.”

Najua pia kwamba katiba hiyohiyo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, sura ya kwanza, Ibara ya 20 inasema kwamba: “Kila mtu anao uhuru wa kukutana na watu wengine kwa hiyari yake na kwa amani, kuchanganyikana, kushirikiana na watu wengine, na kwa ajili hiyo kutoa mawazo yake hadharani (kama Chadema walivyotangaza kuitisha maandamano ya amani nchi nzima).”

Kwa vipengele hivyo viwili tu, ningekuwa katika nafasi yako, nisingekubali kuwanyima Watanzania, bila kujali itikadi ya vyama, haki yao ya msingi ya kuandamama kwa amani, kupinga ubadhirifu mkubwa wa fedha za umma unaoendelea kufanywa na Bunge Maalum la Katiba ilihali kila mmoja akijua wazi kwamba lengo la kupata katiba mpya halitatimia.

Najua maandamano yangewafanya wajumbe wote wa bunge hilo kuona haya na hatimaye kulisitisha na fedha ambazo wangelipwa, zingetumika kununulia dawa za hospitali, madawati, vitabu, maabara au kujengea madarasa kwenye shule nyingi za nchi hii ambazo zinatia huruma.
Badala ya kuwaamuru polisi kufanya doria usiku na mchana kuzuia maandamano, ningewaamuru doria hizo wazifanye kuanzia mikoa ya Kanda ya Ziwa ambako vitendo vya mauaji ya walemavu wa ngozi (albino) na vikongwe vimekithiri.

Ningeelekeza nguvu kupambana na ujambazi ulikithiri kwenye maeneo mbalimbali ya nchi hii, kama katika Mji mdogo wa Tunduma, mpakani mwa Tanzania na Zambia ambapo kila jioni maduka yanaporwa kweupe na majambazi wenye silaha nzito.

Ningeelekeza nguvu kupambana na wahalifu wanaovunja sheria za nchi kwa kuuza madawa ya kulevya, kupora wananchi mali zao kama wafanyavyo Mbwa Mwitu na Panya Road na kufanya mauaji ya watu wasio na hatia.

Kamwe nisingewaagiza wakuu wa vituo vya polisi wawanyime vibali vya kuandamama wananchi wa maeneo yao, ningehakikisha wanawapa ulinzi ili wandamane kwa amani kwani ni haki yao ya kikatiba hata kama ni kwa masilahi ya watu fulani.

Nisingefumbia macho vitendo vya polisi wangu kuwabonda waandishi wa habari wakiwa kazini bila huruma, ningejenga uhusiano mzuri baina yaj eshi, waandishi wa habari na wananchi na kama ningeshindwa kutimiza hayo kama ulivyoshindwa wewe, hakika ningeng’atuka.
Kwa bahati mbaya mimi nitabaki kuwa mimi na sitaweza kuwa wewe lakini kama ningekuwa mimi kwenye nafasi yako, kwa jinsi hali ilivyo sasa, narudia tena kusema bila kumung’unya maneno kwamba ningeng’atuka.

Wasalaam.
credit:GPL

No comments: