Dk. Hamisi Kigwangala.
NIMSHUKURU Mungu kwa kunipa afya njema ya kuweza kuzungumza na nyinyi kupitia safu hii.
Niseme tu kwamba gumzo kubwa ambalo linatawala katika ‘viwanja’ vya siasa ni wagombea urais ambao watamrithi Rais Jakaya Mrisho Kikwete mwakani.
Tayari watu kadhaa wametajwa na wengine kutangaza nia yao ya kuwania nafasi hiyo ya juu ya uongozi hapa nchini. Japo kuna wengine hawathibitishi lakini tayari pilikapilika zao zinadhihirisha kujiandaa na mbio hizo.
Ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanatajwa Waziri Mkuu aliyejiuzulu na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki Samuel Sitta, Waziri Mkuu msaatafu, Fredrick Sumaye na wengineo kwamba watawania nafasi hiyo japokuwa wenyewe, hawajapaza sauti zao hadharani.
Ndani ya Chadema wanaotajwa ni Katibu Mkuu, Dk.Willibrod Slaa na wengine wamekuwa wakiogopa kujitokeza kwa hofu ya kuambiwa bado wakati wa kufanya hivyo.
Kwa CUF, inaeleweka wazi licha ya kusubiriwa kwa vikao rasmi vya chama kuidhinisha. Lakini sijajua kwa nini macho ya wengi katika kuwania nafasi ya urais yapo kwenye Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo watu ‘wazito’ wanatajwatajwa kama nilivyoainisha hapo juu.
Kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hakujawa gumzo kwa atakayegombea urais japokuwa Maalim Seif Shariff Hamadi wa CUF aliwahi kusema kuwa atawania nafasi hiyo kama atateuliwa na chama chake.
Kwa vyama hivi vitatu vinavyoonekana kuwa na ushawishi mkubwa kwa wapiga kura, mvutano mkali unaonekana kuwa ndani ya CCM. Huko tayari mizengwe, fitina na shutuma imeshaanza kujionyesha miongoni mwa wanaotajwa kuwania nafasi hiyo.
Lakini ukiwauliza hao wanaofanyiana mizengwe hiyo kama wana nia yoyote ya urais baada ya Rais Jakaya Kikwete, wanaruka kimanga huku wengine wakisingizia kuwa wanaombwa kufanya hivyo lakini muda wa kujitangaza wanadai bado.
Hivi karibuni, waziri mkuu mstaafu wa awamu ya tatu, Frederick Sumaye akizungumza na waandishi wa habari alikuja na rundo la malalamiko dhidi ya kada mwenzake Edward Lowassa akidai kuwa anamfanyia mbinu chafu katika safari yake ya kisiasa.
Siyo yeye tu, hata Waziri Membe amewahi kuulizwa, akasema eti hadi aoteshwe, nilijiuliza na nani? Mara nyingi Lowassa amekuwa akionekana makanisani na mara nyingine misikitini akiongoza harambee za kukusanya mamilioni ya pesa huku mwenyewe akidai kuwa fedha hizo huchangwa na rafiki zake.
Kutokana na kujifichaficha huko kwa watu nadhani vyama vya siasa vingewaruhusu tu wanaopenda kuwania nafasi hiyo wakawa huru kujitangaza ili wananchi waweze kuwapima.
Kuchelewesha zoezi la kujitangaza sidhani kama ni njia sahihi. Wangepewa uhuru kujitangaza ili kuwapa nafasi wananchi kuwatathmini.Kama kweli mtu ana nia ya kuwa kiongozi wetu, lazima hata chama alichomo kimfahamu na wapiga kura wamwelewe mapema na kumpima.
Naamini kwamba hakuna sababu ya msingi ya vyama vya siasa kuwazuia wanachama wao kujitangaza kwa sababu, mikakati ya kupata urais haianzii kwenye Halmashauri Kuu au Kamati Kuu za chama bali huanzia huko kwenye mashina kwani ndiko walipo wapigakura.
Wapiga kura wana haki ya kujua nani anataka kuwaongoza na kama ana sababu za msingi za kuwania nafasi hiyo pia kujua ikiwa ana uwezo wa kushika nafasi hiyo kubwa na nyeti nchini.
Kujulikana mapema kwa wagombea urais kuna faida nyingi, kwanza itawasaidia hata wao, kujirekebisha hapa na pale watakapokosolewa na wananchi ambao ndiyo wapiga kura wao.
Tabia ya vyama kuzuia watu kujitangaza ni kupalilia au kupanua mianya ya rushwa kitu ambacho ni hatari mno.
Niwapongeze tu wale wote waliochomoza shingo zao, Dk. Hamisi Kigwangala, Januari Makamba, Maalim Seif Sharif Hamadi kwa kutangaza nia mapema ya kuwania urais Tanzania na Zanzibar, ni wakati wa Watanzania kuwapima.
Naviuliza vyama, woga kwa nini kusita kuwaruhusu wanaotaka nafasi hiyo?
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.
CREDIT:GPL
2 comments:
Asante sana Chigwa. Huu ni ukweli mtupu. Ni kwanini Tanzania imekuwa na katabia ako ka kutokuwaweka wagombea wazi? Huu ni mwezi wa kumi tayari umenyemelea! Ikiwa imebakia mwaka mmoja unatarajia watakaoingia kwenye kinyanganyiro wasiendeshe biashara ya rushwa kuweza kukubalika? Hatuna budi kujifunza na kujaribu kuwa na uwazi kuanzia serikali za mitaa.
doctor kwanini umeamua kuingia katika siasa tena kwenye chama cha magamba?au ndo deal zipo huko
Post a Comment