Advertisements

Tuesday, September 9, 2014

LONGIDO; NJIA YA UTALII ISIYOWANUFAISHA WENYEJI.

Makala: Gabriel Ng’osha
Longido ni moja kati ya wilaya saba zilizomo katika Mkoa wa Arusha. Ni jimbo linalounganisha Nchi ya Kenya na Tanzania kupitia Mpaka wa Namanga. Kwa awamu nne sasa, jimbo hilo linaongozwa na Mheshimiwa Michael Lekule Laizer kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).



Sehemu kubwa ya jimbo hilo ni mbuga iliyotenganishwa na Barabara ya Arusha- Nairobi. Pamoja na mpaka wa Namanga kupitisha maelfu ya watalii wanaokwenda kutembelea mbuga za wanyama na kupanda Mlima Kilimanjaro, bado wananchi wa kawaida wa jimbo hilo wanaishi maisha ya ufukara wa hali ya juu.

Asilimia kubwa ya wananchi wa Longido ni kutoka jamii ya wafugaji ya Wamasai wanaoendesha maisha yao kupitia ufugaji ingawa kuna jamii nyingine zinazojishughulisha na kilimo.


Uwazi lilifanikiwa kuzungumza na wananchi kadhaa wa jimbo hilo lenye jumla ya wakazi 123,153 kwa mujibu wa sense ya watu na makazi ya mwaka 2012. Wananchi walioongea na Uwazi ni kutoka kata za Matale, Engarenaibo, Mundarara, Kamwanga, Olmolog, Tingatinga, Ketumbeine, Ilorienito, Gelai, Lumbwa,Getai na Orbomba.

MATATIZO YA WANANCHI
Baadhi ya wananchi waliozungumza na Uwazi, walilitaja tatizo lao kubwa kuwa ni ukame uliokithiri ambapo hulazimika kusafiri umbali mrefu na mifugo yao kufuata maji kwenye bwawa moja tu lililopo jimboni humo.

Mbaya zaidi, maji hayohayo yanayotumika kunyweshea mifugo, hutumika pia kwa matumizi ya nyumbani na kilimo, jambo linalohatarisha maisha ya wakazi wa jimbo hilo.Wananchi hao waliyataja matatizo mengine yanayowakabili kuwa ni ukosefu wa huduma bora za kijamii zikiwemo uhaba wa hospitali, madaktari, dawa na vifaa vya tiba.

Pia kiwango cha elimu bado ni kidogo sana na watoto wengi huachishwa masomo ili wakachunge mifugo, migogoro ya ardhi ya mara kwa mara kati ya wakulima na wafugaji inayoibua chuki miongoni mwa jamii, uwindaji haramu na wanyama wakali kuvamia makazi ya binadamu na kusababisha vifo vya watu na mifugo.

Ukosefu wa elimu bora ya ufugaji ni tatizo lingine linalowasumbua wakazi wa jimbo hilo kwani licha ya wengi kuwa na idadi kubwa ya mifugo, hawajui namna ya kuitumia kubadilisha maisha yao. Pia wanyama wengi hufa kipindi cha kiangazi kutokana na ukame mkali unaolisumbua jimbo hilo.

‘’Maji ya kutumia sisi na mifugo ni tatizo sana hapa kwetu, hasa kipindi cha kiangazi mifugo inakufa sana kutokana na ukame lakini milima yetu ina maji mengi sana,” alikaririwa mmoja wa wananchi wa jimbo hilo aliyezungumza na Uwazi.

“Mimi ni mkulima, nalima kilimo cha umwagiliaji na nategemea maji kutoka bwawani, tatizo langu kubwa ni mifugo kuachiwa holela na kula mazao yetu hasa kipindi cha kiangazi, kiukweli jambo hili linaweza kuzua ugomvi baina ya wakulima na wafugaji, tunaomba serikali ituletee maji,’’ alisema mkazi mwingine wa jimbo hilo.

Uingizwaji holela wa bidhaa kutoka nchi jirani ya Kenya, nyingi zikiwa hazina ubowa wala hazijathibitishwa na TBS, ni tatizo lingine linalowasumbua wakazi wa Longido. Pia wananchi hao wameiambia Uwazi kwamba kuna baadhi ya wahamiaji haramu kutoka nchi jirani, hupitia kwenye jimbo hilo wanapotaka kuingia Tanzania.

MAELEZO YA MBUNGE
Baada ya kuwasikia wananchi, Uwazi lilianza kumtafuta Mbunge Laizer ambaye alipopatikana kwa simu, alikiri kuwepo kwa matatizo hayo jimboni kwake lakini akaeleza kwamba amejitahidi na bado anaendelea kuhangaika kuhakikisha anawakomboa wananchi wake, hasa wa jamii ya wafugaji.

“Siwezi kuzungumza sana kwa sababu nipo njiani naelekea Dodoma lakini nimefanya kazi kubwa sana kuwatetea wafugaji wa Longido na wananchi wote. Mimi ndiyo sauti yao nikiwa bungeni kwani nawatetea kadiri niwezavyo, nitashughulikia kero zote zinazowasumbua,” alisema mbunge

2 comments:

Anonymous said...

kitu gani kinawanufaisha wenyeji/wazawa wa nchi hii tujiulize?

Anonymous said...

Na inashangaza kuona jinsi utalii unavyoingiza fedha nyingi kupitia ardhi yao kitu ambacho wenyeji hawanufaiki kabisa. Jamani hiyo sio aibu kubwa kwa serikali?? Je huu sio wizi wa wazi kabisa serikali kuwaibia wananchi wake hadharani. Na pia inashangaza sana kuona raisi Kikwete akipewa sifa nyingi kwa kuinua uchumi wa nchi. Je raisi Kikwete swali kwake ni je hao watu wengine hawastahili maisha bora? Kwa nini wao wabaguliwe? Je Tanzania umaskini na kutowajali watu wote ndio sera gani hizo. Mabadiliko yanahitajika. Kikwete kuja huku Washington, DC kupewa sifa zote kwa gharama kubwa eti kwa kazi nzuri anazozifanya, jua kuwa kuna watu wanakufa kule Arusha kwa njaa.