ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, September 9, 2014

Maalim Seif: Migogoro inayowakumba wakulima na wafugaji ni kwasababu ya kukosa sera sahihi

 Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad akihutubia mkutano wa hadhara katika uwanja wa Furahisha Kirumba, mjini Mwanza.
 Sehemu ya umati uliohudhuria kwenye Mkutano wa hadhara wakimsikiliza katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif  Hamad
Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad akihutubia mkutano wa hadhara katika uwanja wa Furahisha Kirumba, mjini Mwanza.
 
Na Khamis Haji, OMKR
 
Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF, Mhe. Maalim Seif Sharifa Hamad amesema migogoro inayowakumba wakulima na wafugaji na kusababisha mauaji inasababishwa na Serikali iliyopo chini ya Chama cha Mapinduzi kukosa sera sahihi ya Kilimo na Ufugaji.

 Maalim Seif ameyasema hayo katika mikutano tafauti akiwa katika ziara ya siku nne mkoani Mwanza kwa ajili ya kuzindua miradi ya maendeleo iliyo chini ya Kata zinazoongozwa na CUF pamoja na kuzungumza na wananchi katika mikutano ya hadhara.
Akizungumza na wananchi baada ya kuzindua daraja katika Kata ya Igogo amesema inasikitisha kuona kila siku wakulima na wafugaji wakiuana kwa kugombea maeneo ya kilimo na kulishia mifugo huku Serikali ikishindwa kudhibiti hali hiyo.
Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amesema kusingekuwa na mauaji kati ya wakulima na wafugaji iwapo Serikali ingekuwa na Sera thabiti inayoanisha maeneo maaluma kwa ajili ya ufugaji na maeneo maalum ambayo ni kwa shughuli za kilimo pekee.
“Kama Serikali ingekuwa na Sera inayoanisha haya ni maeneo ya ufugaji na haya ni ya kilimo tusingeshuhudia mapigano na mauaji haya, wakulima na wafugaji wangefanya kazi zao kwa utulivu na kazi zao zingewapatia maslahi makubwa”, amesema Maalim Seif.
Amesema Tanzania imejaliwa maliasili nyingi kuliko nchi nyingi duniani na iwapo tungeweza kuzitumia vizuri hakuna sababu nchi hii kuwa miongoni mwa nchi masikini.
Maalim Seif ameeleza kuwa mbali na maliasili zilizopo chini ya ardhi kama vile madini, gesi na mafuta, Tanzania imejaaliwa kuwa na hali ya hewa inayotafautina katika maeneo ambayo inaifanya nchi kuzalisha mazao tafauti tafauti.
Hata hivyo, amesema kukosekana kwa sera muafaka kuna sababisha wananchi walio wengi kushindwa kunufaika na neema hiyo na kutoa mfano, licha ya wananchi wa kanda ya Ziwa kuongoza kwa kilimo cha Pamba, lakini hakuna hata kiwanda cha nguo.
“Wananchi wa Kanda hii nyinyi ndio mnaozalisha Pamba, lakini pamba hiyo inasafirishwa Ulaya, wanatengeza nguo wanavaa na baadaye wanatuletea sisi ikiwa ni mitumba na sisi tunaivaa”, alieleza Maalim Seif.
Akihutubia katika mkutano wa hadhara katika uwanja wa Furahisha Kirumba, Maalim Seif amesema wananchi hawana budi kujiandaa kufanya mageuzi ya uongozi wa nchi kwa kuwaweka madarakani viongozi wenye uwezo na mtazamo mpya wa kuleta maendeleo ya wananchi.
Naye Mbunge wa Nyamagana kupitia CHADEMA, Ezekiel Wenje akihutubia katika mkutano huo amesema njia muafaka ya kuleta mageuzi ya kiuongozi nchini ni vyama vya upinzani kuendeleza ushirikiano na kuwa na mgombea mmoja katika ngazi zote.
Wenje amesema yeye binafsi yuko tayari kufadhili safari ya viongozi wakuu wa CHADEMA, CUF na NCCR Mageuzi wakajifungie nchini Sychelles ili waweze kupata mgombea mmoja ambaye watamsimaisha kuwania Urais katika uchaguzi mkuu wa mwakani kupitia Ukawa.
Hata hivyo, akilifafanua hilo, Maalim Seif amesema jambo hilo wala halihitaji kwenda kuamuliwa nje ya nchi, na badala yake viongozi hao wanaweza kutoa maamuzi hayo hapa hapa nchini

1 comment:

Anonymous said...

maalim wewe ndio mzalendo wa kweli,simba wa nyika.
magamba wanahaha kile pembe ndomaana sasa wanakimbilia marekani kuwazubaisha.

ccm/magamba kwishsa kiswa kabisa kifo cha mende,ndembe ndembe, mlalo wa chali.