ANGALIA LIVE NEWS

Monday, September 29, 2014

Manzese wakabidhiwa Sh100 milioni kuboresha makazi yao

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka akizungumza wakati wa kukabidhi hundi ya Sh100 milioni kwa wakazi wa Kata ya Manzese iliyotolewa na Benki ya Azania kupitia asasi ya Tanzania Financial Services for Underserved Settlement (TAFSUS), Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. Kulia ni Mkurugenzi wa bodi ya asasi hiyo, John Ulanga. Picha na Jennifer Sumi
Dar es Salaam. Wakazi wa Kata ya Manzese na Mtaa wa Mvuleni, jijini hapa wamepokea zaidi ya Sh100 milioni kutoka Benki ya Azania kwa ajili ya kuboresha makazi yao duni.
Fedha hizo zilizotolewa kwa udhamini wa asasi ya uboreshaji makazi duni ya Tanzania Financial Services for Underserved Settlement (TAFSUS), zitatolewa kwa mikopo ya kati ya Sh1.5 milioni hadi  Sh9 milioni  kwa kaya.
Akizungumza katika uzinduzi wa mradi wa makazi duni, uliofanyika mwishoni mwa wiki, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa  Anna Tibaijuka alisema mradi wa kuboresha nyumba hizo umeonyesha maboresho ya maisha ya wakazi hao.
“Ninafurahi kuwapo katika uzinduzi huu wa awamu ya pili na tatu ya mradi, kwani hii ni moja ya juhudi ambazo Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ingependa kuziona kote nchini katika  kuboresha makazi ya  Watanzania.
“Kama mnavyofahamu, namna bora ya kuboresha maisha ya mwanadamu, kwanza ni kuboresha makazi yake. Ukishakuwa na makazi bora, hata afya itakuwa bora zaidi, watoto wataishi na kukua katika mazingira bora,” alisema Profesa Tibaijuka.
Awali, Mkurugenzi wa Bodi ya Wakurugenzi ya TAFSUS, John Ulanga alisema taasisi yake ni chombo cha kitaifa kinachotoa huduma za udhamini wa kifedha ili kusaidia kuboresha makazi nchini hasa maeneo yenye changamoto.
“Lengo la msingi la TAFSUS ni kuhamasisha na kuwezesha taasisi za fedha kutoa mikopo ya kuboresha makazi pale ambako kwa taratibu za kawaida, isingetolewa. Mikopo hiyo hutolewa kuboresha makazi yakiwamo yale yasiyo rasmi na kuziwezesha jamii zenye kipato cha chini kuwa na maisha bora,” alisema  Ulanga.
Mkurugenzi wa Fedha wa Benki ya Azania, Lukwaro Senkoro alisema benki hiyo iliitikia wito wa kutoa mikopo ya riba na masharti nafuu kwa ajili ya kuunga mkono mradi huo wa kuboresha makazi ya wakazi hao.
Mwananchi

No comments: