Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Tuvako Manongi akiwa na Mwakilishi Mkazi wa MARIE STOPES TANZANIA Bi. Ulla E. Muller aliyefika Uwakilishi wa Kudumu na kisha kuwa na mazungumzo na Balozi. Bi. Muller pamoja na kuelezea shughuli za Shirika lake amesema anajivunia na kuridhishwa na ushirikiano uliopo baina ya Serikali na Shirika lake, ushirikiano ambao anasema amekuwa akiuelezea kila alipokutana na wafadhili wanaosaidia miradi mbalimbali nchini Tanzania.
Na Mwandishi Maalum, New York
Ushirikiano na uhusiano mzuri baina ya Serikali na Shirika lisilo la Kiserikali la Marie Stopes umeliwezesha shirika hilo kuwafikishia wananchi wengi zaidi huduma mbalimbali za afya zikiwamo za uzazi wa mpango
Hayo yameelezwa siku ya jumatatu na Mwakilishi Mkazi wa Marie Stopes nchini Tanzania, Bi. Ulla E. Muller wakati alipomtembelea na kufanya mazungumzo na Balozi Tuvako Manongi, Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa.
“ Tunafanya kazi kwa karibu sana na serikali na kwa kweli tumekuwa na uhusiano nzuri na ambao tunajivunia, uhusiano ambao pia nimekuwa nikiueleza kwa wafadhili wetu mbalimbali wakiwamo niliokutana nao hapa New York.”Akaeleza
Kama sehemu ya kudhihirisha uhusiano huo na serikali amesema Shirika lake kwa nyakati tofauti wamekuwa wakizitumia hotuba mbalimbali za Mhe. Rais Jakaya Mrisho Kikwete hususani zile zinazohusu masuala ya afya bora na uzazi salama.
Akabainisha kuwa matokeo hayo ya ushirikiano na maelewano na serikali, siyo tu yamewezesha kuwafikia wananchi wengi wanaohitaji huduma mbalimbali za afya hasa wale walio maeneo yasiyofikika, bali pia kumelifanya Shirika lake kuingia katika utekelezaji wa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa.
Bi. Muller ambaye kwa mara ya kwanza alifika nchini Tanzania mwaka 1994 na kurudi tena miaka miwili iliyopita anasema Tanzania inasonga mbele kimaendeleo jambo analosema ni la kujivunia.
Amesema. “ Nilifika mara ya kwanza mwaka 1994 na kuondoka lakini miaka 20 ya kuifahamu kwangu Tanzania ninaona mabadiliko makubwa kwa nchi hii mabadiliko ambayo kwa mtu au mgeni wa muda mfupi hawezi kuyaona, lakini mimi nimeona tofauti kubwa ya wakati huo na sasa”.
Pamoja na kujikita katika utoaji na usambazaji wa huduma za afya salama ya uzazi, uzazi wa mpango na huduma nyinginezo, Mwakilishi Mkazi, amemwambia Balozi kuwa Shirika lake pia linataka kuwekeza zaidi kwa vijana ambao ndio wengi nchini Tanzania.
Amesema takwimu za idadi ya watu zinaonyesha kuwa vijana ndiyo wengi zaidi kuliko kundi jingine la jamii. Ni kwa sababu hiyo anasema kuna kila sababu ya kuwekeza katika kuwasaidia vijana ili pamoja na mambo mengine kuongeza kasi ya kuupiga vita umaskini.
Kwa upande wake Balozi Tuvako Manongi amesifu na kushukuru mchango wa Marie Stopes katika kusambaza huduma zake kwa walengwa mbalimbali na kubwa zaidi kwa kufanya kazi kwa karibu na Serikali.
Balozi amesisitiza haja na umuhimu wa Mashirika hayo yasiyo ya kiserikali kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia vipaumbele vya Kitaifa kwa kuwa ndivyo vyenye maslahi zaidi kwa watanzania.
No comments:
Post a Comment